JUMA hili, katika shule ya msingi ya Melvin Jones, Kaunti ya Nakuru, wanafunzi wa shule ya Upili ya Wasichana ya Butere walitua kuwasilisha mchezo wao wa kuigiza maarufu kama “Echoes of War”. Wanafunzi hao walitarajiwa kuuwasilisha mchezo wao ukumbini saa mbili asubuhi, jambo walilopinga kutokana na sababu kuwa hawakuwa na mwelekezi wao na nyenzo za kutumia wakiigiza. Badala yake, waliamua kuimba wimbo wa taifa, wakatulia kimya kwa muda wa dakika moja kisha wakaondoka ukumbini. Hata hivyo, jambo lililozua mtafaruku ni kisa cha askari cha kuwarusha wanafunzi wale vitoza machozi. Wanafunzi hao ambao huenda walikuwa wa chini ya miaka kumi na minane (18), walidai kuruhusiwa kuwasilisha mchezo huo chini ya uongozi wa mwelekezi wao na mwandishi wa mchezo huo, aliyekuwa Seneta, Cleopas Malala. Kukosa kwa mwelekezi huyo ndiko kuliwafanya kuteta wakishangaa alikokuwa. Kwa kawaida, hili halikuwa jambo la kutumia nguvu kupita kiasi kwa wanafunzi hao. Lilikuwa ni suala tu la kuwasikiliza wanafunzi watoe malalamishi yao kisha waigize au wakose kuigiza maana hao wenyewe hawasababishi fujo. Uhalali wa mchezo huo ulikuwa umethibitishwa na mahakama ambayo ilikuwa imeruhusu mchezo ufanyike kama ilivyopangwa. Ingawa kuna vipengele vya mchezo huo ambavyo huenda vilikashifu serikali, mwandishi wa mchezo hakuwa mwanafunzi wala mwalimu. Ilistahili kumkabili yeye mwenyewe ikiwa alikuwa amefanya makosa na afikishwe mahakamani kujibu mashtaka. Wanafunzi walikuwa tu wakitekeleza wajibu wao wa kuwasilisha igizo kulingana na mafunzo waliyokuwa wamepewa. Kabla ya igizo hilo kufika kiwango hicho cha kitaifa, bila shaka lilikuwa limekaguliwa mara kadhaa na wakaguzi ambao pia ni walimu. Vile vile, wanafunzi hao walikuwa wakifanya mazoezi shuleni mwao, thibitisho kuwa hata mwalimu mkuu wa shule yao alikuwa na ufahamu kamili kuhusu mchezo wenyewe. Hao ndio walistahili kurekebisha mambo mapema kama kulikuwa na dosari.
TUME ya Kuwaajiri Walimu (TSC) ikishirikiana na Wizara ya Elimu imeanza kufunza walimu wakuu wa shule za sekondari namna ya kusaidia wanafunzi wa Gredi ya Tisa wanaotarajiwa kujiunga na Sekondari Msingi kuchagua taaluma wanazoazimia kufanya. Aidha, walimu hao watakuwa na jukumu kubwa la kuwasaidia wanafunzi hao kuchagua mkondo wao wa maisha wakiwa shuleni. Mwaka ujao, 2026, zaidi ya wanafunzi 1.2 milioni watajiunga na shule za upili kulingana na taaluma wanaotazamia kufanya. Kwa mfano, shule za kitaifa zinatarajiwa kuchukua mikondo mitatu, ikiwemo spoti na sayansi. Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Bi Nancy Macharia, alisema mafunzo hayo yatasaidia walimu wakuu kusaidia wanafunzi kuchagua taaluma zao. “Watachagua taaluma kulingana na uwezo wao wa kimasomo na matamanio yao. Lakini tunawapa haya mafunzo kuhakikisha mnawasaidia kuchukua mkondo wao wa maisha,” alisema Bi Macharia. Bi Macharia aliwakilishwa na mkurugenzi wa walimu Bi Antonina Lentoijoni kwenye kongamano la zaidi ya walimu 1000 wa shule za upili kutoka kaunti saba ikiwemo Muranga, Kiambu, Nyandarua, Nakuru, Machakos, Makueni, Tharaka Nithi na Laikipia. Kote nchini TSC na Wizara ya Elimu zinawapa walimu 7,000 mafunzo hayo sehemu kadhaa. Bi Lentoijoni alisema warsha hiyo imejiri wakati mwafaka Kenya inapopitia mageuzi ya elimu kutoka mfumo wa 8-4-4 hadi ule wa CBC unaonuia kubadilisha maisha ya wanafunzi nchini. Aliwapongeza walimu wakuu kutoka Murang'a kupitia chama chao cha KESSHA kwa kuandaa hafla hiyo. “Kenya imepiga hatua kubwa sana katika sekta ya elimu, mwakani (2026) tutashuhudia mageuzi kabambe wakati watoto wetu watakapojiunga na shule za upili yaani Gredi ya 10 inayolenga kukuza talanta zao,” alisema Bi Macharia.
KUTOKANA na ongezeko la vifaa vya kielektroniki, watoto sasa wanatazama vitabu kwenye vifaa bebe. Ni rahisi kuelewa mvuto wa vifaa hivi kwani hadithi zinachanganywa na picha za kupendeza pamoja na muziki wa kuwavutia watoto. Lakini je, mbinu hizi za kisasa za kusimulia hadithi zinaboresha ufunzaji wa watoto? Kulingana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Vanderbilt, sehemu muhimu zaidi ya hadithi si jinsi mtoto anavyoiona, bali jinsi anavyoipitia na kuielewa. Kwa kusoma vitabu ana kwa ana na mtoto wako, mzazi hupata nafasi ya kuchambua hadithi na wahusika waliomo. Aina hii ya kusoma inaitwa Usomaji wa Mazungumzo. Inawashirikisha watoto wadogo katika mchakato wa kusoma na hufaa watoto wa rika zote. Usomaji huu huwasaidia watoto wadogo kuwa wanafunzi wepesi kuelewa. Kupitia maswali na mitazamo mbalimbali inayoibuka anaposhirikiana nsa mzazi kusoma, watoto wana uwezo mkubwa wa kufikiria kuhusu wanachokiona, kuunda uhusiano, kukuza ujuzi wa msamiati mpya, na kupata uzoefu wa hadithi. Hata hivyo, aina hii ya ushirikishaji huwa nadra zaidi watoto wanapotazama hadithi kwenye vifaabebe.Katika utafiti uliohusisha wazazi 81 na watoto wao wa miaka mitatu, watafiti waliwapa watoto hao video za DVD zenye hadithi watazame kwa wiki nne. Watoto walifanya mitihani miwili - kabla na baada ya majaribio, kuhusu msamiati na uelewa wa hadithi hizo. Katika matokeo ya utafiti, wazazi waliojadili hadithi hizo za DVD na watoto wao waliwafanya kupata alama za juu zaidi kwenye mtihani wa baada ya majaribio, kuliko watoto wa wazazi waliotazama tu video hizo bila kutoa maoni au kuuliza maswali. Kwa kuwa hadithi za kielektroniki sasa zimekuwa sehemu ya elimu na maisha kwa jumla, kuna mambo ambayo wazazi wanaweza kufanya ili mbinu hii iwe ya maana zaidi na yenye manufaa kwa watoto wao — wachanganye Usomaji wa Mazungumzo na Masomo Dijitali.
Na Malima Lubasha, Serengeti Jumla ya watumishi wastaafu serikalini 123 katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wameshauri benki ya Azania kupunguza asilimia ya riba kwa mikopo inayosomeka tarakimu mbili na kupendekeza isomeke tarakimu moja ili kuwapa nafuu ya kukopa. Ushauri huo umetolewa na wastaafu hao wakati wakipata elimu juu ya mikopo na fursa za kifedha […]
Na Mwandishi Wetu, Berlin-Ujerumani Mfuko wa Dunia wa Watu wenye Walemavu (Global Disability Fund – GDF) umezikutanisha nchi zaidi ya 23 Mjini Berlin nchini Ujerumani huku wakijikita katika kuzungumzia masuala yanayohusu Watu Wenye Ulemavu katika nyaja mbalimbali ikiwemo Elimu, Mabadiliko ya Tabia Nchi, Uchumi, kukabiliana na kurejesha hali wakati wa maafa pamoja na masuala ya […]
MIRADI mikubwa ya afya ya thamani ya mabilioni ya pesa imekwama kote nchini, na kuwaacha wagonjwa mahututi na chaguo chache au ghali kupata matibabu. Kukwama kwa miradi kama vile Kituo cha Dharura cha Watoto na Usimamizi wa Majeruhi wa Moto katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Kituo cha Saratani cha Kisii, na Kituo cha Ubora cha Taasisi ya Figo Afrika Mashariki kumesababisha msongamano mkubwa hospitalini, vifo vinavyoweza kuzuiliwa, na kuzidisha mgogoro wa afya nchini Kenya, na kuwaacha wagonjwa wengi bila huduma za msingi za matibabu. Watoto wanaohitaji huduma za haraka za matibabu wanakabiliwa na hatari kwa sababu Kituo cha Dharura cha Watoto na Usimamizi wa Majeruhi wa Moto katika KNH hakijakamilika. Mradi huo ulipangwa kukamilika mwaka wa 2020 lakini haukuwa umekamilika kufikia Juni 2024, licha ya zaidi ya Sh1.1 bilioni kutumiwa tayari. Kituo cha majeruhi wa moto kitakuwa na vitanda 82 katika wodi ya kawaida, vitanda 14 vya ICU, na vitanda sita vya wodi ya HDU, huku kituo cha watoto kikiwa na vitanda 82 vya wodi ya kawaida, vitanda 24 vya ICU, na vitanda sita vya huduma maalum. Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, kwa mwaka wa kifedha ulioishia Juni 2024 ilibainisha kuwa ucheleweshaji huo umesababisha gharama zisizohitajika za Sh68 milioni – fedha ambazo zingetumika kununua vifaa muhimu vya matibabu, kuajiri madaktari, au kuboresha huduma nyingine za afya. "Pia, thamani ya kazi iliyofanyika inajumuisha riba ya malipo ya kuchelewesha ya Sh68, 043, 601 ambayo ingeweza kuepukwa. Hii ni kinyume na Kifungu cha 151 (2) (c) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma 2015, ambayo inahitaji taasisi kulipa madeni yake kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba," alisema mkaguzi mkuu. Hali ni mbaya vilevile kwa wagonjwa wa Saratani Kisii na maeneo jirani. Ujenzi wa Kituo cha Saratani cha Kisii, ambacho kingetoa matibabu maalum ya Saratani, umekwama licha ya ufadhili kupatikana miaka tisa iliyopita. Mradi huo ulipangwa kukamilika mwaka wa 2016, lakini haujakamilika hadi sasa. Ingawa kandarasi ilitolewa Januari 2024, ujenzi haukuwa umeanza kufikia Juni 2024, na kuwaacha wagonjwa bila huduma muhimu za kuokoa maisha. Ripoti ya mkaguzi mkuu ilibaini kuwa licha ya malipo ya awali ya Sh283 milioni, hakuna kazi yoyote ya ujenzi iliyoanza, huku mamilioni mengine yakitumika kununua vifaa vya matibabu na samani ambazo bado hazijatumika kutokana na ukosefu wa jengo lililokamilika. Wakati huo huo, wagonjwa wa figo nchini Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla bado wanasubiri kukamilika kwa Kituo cha Ubora cha Taasisi ya Figo Afrika Mashariki cha thamani ya Sh3.7 bilioni, ambacho hakijakamilika miaka sita baada ya tarehe yake ya kukamilika iliyopangwa 2019. Mradi huo, unaojumuisha jengo la ghorofa tano la shule ya matibabu lenye wodi, maabara, vyumba vya upasuaji, vitengo vya uangalizi maalum, vyumba vya ushauri wa matibabu, na sehemu za maegesho, bado haujakamilika licha ya Sh2.79 bilioni kutumika tayari. Katika Kaunti ya Kitui, miradi kadhaa ya thamani ya Sh404.58 milioni haijakamilika, baadhi yake ikiwa imekwama tangu 2017, ikiwa ni pamoja na jengo la wodi ya uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kitui (Sh242.78 milioni), jengo la X-ray katika Hospitali ya Kauwi (Sh2.20 milioni), na kiwanda cha gesi ya Oksijeni (Sh14.5 milioni). Katika Kaunti ya Pokot Magharibi, miradi mikubwa imesimama, ikiwemo hospitali ya wanawake katika Chuo cha Walimu cha Chesta (Sh37.40 milioni) na jengo la ofisi huko Kapenguria (Sh52.45 milioni). Kaunti ya Bomet ina miradi ya thamani ya takriban Sh300 milioni ambayo imecheleweshwa au kutelekezwa. Hii inajumuisha Kituo cha Afya ya Mama na Mtoto cha Dkt Laboso Memorial (Sh296.93 milioni) na chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Sigor Sub-County (Sh3.99 milioni.
SHULE zikifungwa wiki hii kuashiria kumalizika kwa muhula wa kwanza, changamoto bado zinaendelea kukabili sekta ya elimu nchini ikiwemo miundomsingi, ufadhili wa elimu ya bure na karo. Kwa kipindi cha miezi minne sasa walimu wakuu wamekuwa wakiishinikiza wizara ya elimu kuwaruhusu kuongeza karo hasa katika shule za sekondari baada ya serikali kushindwa kutimiza jukumu lake kikamilifu kufadhili sekta ya elimu. Hii imewaacha walimu wakuu kwenye njia panda huku wakidaiwa malimbikizi ya madeni. Wanafunzi watasalia nyumbani kwa kipindi cha wiki tatu wakitarajiwa kurejea shuleni mwisho wa mwezi huu wa Aprili. Baraza la Kitaifa la Mtihani Nchini (KNEC) imekamilisha usajili wa wanafunzi watakaofanya mtihani wa kidato cha nne pamoja na wale wa Gredi ya tisa ili kujiunga na shule za sekondari. Mwenyekiti wa Muungano wa Wazazi Nchini Bw Silas Obuhatsa, Jumatatu, Machi 31, 2025 alisema wazazi wanafaa kuwahamamisha zaidi ya wanafunzi 1.2 walioko Gredi ya tisa wanaotarajiwa kujiunga na shule za sekondari kuanzia mwaka ujao, 2026. “Katika likizo hii tunawasihi wazazi hasa wale wenye watoto katika Gredi ya Tisa kuanza kuwahamasisha kuhusu Shule ya Juu (Senior School) itakayoanza mwaka ujao ili wajitayarishe mapema,” akasema Bw Obuhatsa. Aliwasihi wazazi wawalinde watoto wakati wa likizo ili wasijiingize kwenye vikundi vya uhalifu, mihadarati au unywaji pombe pamoja na kuozwa mapema na kufanyiwa tohara ya lazima. “Watoto walindwe dhidi ya walanguzi wa mihadarati na dhidi ya wale wanaowanyemelea kingono. Wazazi wahakikishe hawarandarandi mtaani,” alisema Bw Obuhatsa. Alisema dhuluma za kijinsia dhidi ya wanawake inaongezeka akimsihi Rais William Ruto kuagiza vyombo vya usalama kukabiliana na washukiwa. “Watoto wa kike wanafaa kulindwa zaidi kwa sababu visa vya dhulma za kijinsia vinaendelea kuongezeka, tuna wasiwasi kama wazazi,” alisema mwenyekiti huyo. Aliwashtumu wazazi kwa kushindwa kutimiza majukumu yao ya ulezi na kuchela. Bw Obuhatsa alisema watoto wengine wamekosea vielelezo bora kwa sababu wazazi wao wanajihusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya miongoni mwa maovu mengine. Alielea wasiwasi wake kuhusu usalama wa watoto msimu huu wa mvua. Mwaka jana sekta ya elimu iliathirika pakubwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kupelekea kuahirishwa kwa ufunguzi wa shule, sababu zingine zilisombwa na maji ya mafuriko. Zaidi ya watu 100 waliaga dunia na mamia ya wengine kusalia bila makao kufuatia mvua hiyo. “Mvua imeanza, utabiri wa hali ya hewa umeshatangaza kuhusu msimu huu, tuwe makini. Tulinde watoto wetu,” alisisitiza Bw Obuhatsa. Waziri wa Elimu Bw Julius Ogamba alisema serikali imejitayarisha kuhakikisha hakuna changamoto wanafunzi wa Gredi ya tisa wanapojiunga na shule za sekondari.
KUTUMA ujumbe mfupi huwapa watoto na watu wazima njia ya haraka na rahisi ya kuwasiliana, lakini kuna madhara ya kutumia njia hizi za mkato. Kwa mujibu wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Penn State, Amerika mazoea ya kutumia jumbe fupi kwa mawasiliano miaka ile ya mwanzoni ya kuweka msingi wa masomo mwanafunzi akiwa shuleni, kunaweza kupunguza ujuzi wa lugha na sarufi. Katika utafiti uliochapishwa kwenye jarida la New Media & Society, watafiti waliwapa wanafunzi wa shule za sekondari mtihani wa tathmini ya sarufi kulingana na dhana walizofundishwa wakati wa mwaka wa masomo. Walikusanya taarifa kuhusu tabia za wanafunzi katika kutuma ujumbe mfupi, ikiwa ni pamoja na mara wanazotuma na kupokea jumbe. Pia, waliwauliza wanafunzi waandike idadi ya mafupisho (yaani, njia fupi za kuandika ujumbe) walizotumia katika jumbe zao tatu za mwisho. Watafiti waligundua kuwa matumizi ya njia fupi za kuandika ujumbe yanaweza kuwa na athari kubwa kwa mawasiliano rasmi. Katika utafiti huu, matumizi ya jumbe fupi kwa wingi yalihusiana na utendaji duni wa wanafunzi katika mtihani wa sarufi. Katika ulimwengu wetu wa teknolojia ya kisasa, kutuma ujumbe na njia nyingine za mawasiliano ya haraka kutaendelea kuwepo. Hilo si jambo baya kabisa. Kutuma ujumbe huwapa watoto wetu njia rahisi na ya haraka ya kujieleza. “Lengo letu kama wazazi si kujaribu kuondoa matumizi ya arafa kabisa! Badala yake, kuna mambo tunayoweza kufanya ili kusaidia kukuza ujuzi wa lugha na uandishi kwa watoto wetu wanapokua,” asema Dkt Debbie Glasser, mmoja wa watafiti hao. Wataalamu wanashauri wazazi kuchukua muda kuwasiliana na watoto kwa sentensi kamili.“Unapowatumia watoto wako ujumbe, chukua muda wa ziada kuwasiliana kwa sentensi kamili mara kwa mara. Kuna utafiti unaopendekeza kuwa watoto huwa na hamu ya kuiga marafiki na familia zao. Hii ni fursa nzuri kuwa mfano mzuri katika matumizi ya sarufi sahihi,” aeleza Dkt Debbie.
Na Nora Damian, Mtanzania Digital Walimu wakuu 60 na wapishi katika shule za msingi Halmashauri ya Manispaa Temeke wamejengewa uwezo kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuboresha afya zao na wanafunzi pamoja na kulinda mazingira. Mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika Shule ya Msingi Likwati yameandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Mpango wa Chakula […]
Na Malima Lubasha, Serengeti Kampuni ya Grumeti Reserves inayoshughulika na uhifadhi wa wanyamapori katika mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, imekabidhi msaada wa madawati 50 kwa Shule ya Msingi Mbirikiri yenye thamani ya sh 3.5 milioni ili kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini wakati wa masomo. Ofisa Rasilimali […]
Na Malima Lubasha, Serengeti Vijana 112 wa kundi rika (Saiga) katika Kijiji cha Mbirikiri Kata ya Sedeco Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, kwa kushirikiana na wazee na wanawake wamekubaliana wejenge nyumba mbili za walimu kwa nguvu zao zitakazogharimu sh 12 milioni kutokana na changamoto ya uhaba wa nyumba unaoikabili shule ya msingi Mbirikiri […]
Na Malima Lubasha, Serengeti Kampuni ya Beyond Wild Impact, inayofanya shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, imesaini makubaliano na uongozi wa Kamati ya Shule ya Msingi Mbirikiri kutoa dola 50,000 sawa na Sh 127 milioni kuboresha miundombinu ya shule hiyo iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na kushindwa kuikamilisha. Makubaliano ya utekelezaji wa mradi […]
Na Nora Damian, Mtanzania Digital Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA) inatarajia kujenga vyuo vipya sita ambavyo vitajikita zaidi kutoa elimu katika Uchumi wa Buluu. Kwa sasa mamlaka hiyo ina vyuo vitano ambapo vitatu vipo Unguja na viwili Pemba. Akizungumza Machi 20,2025 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA), Dk. Bakari […]
Na Nora Damian, Mtanzania Digital Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema amefurahishwa na kazi inayofanywa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) ya kutoa mafunzo ya ufundi stadi na kuwezesha Watanzania wengi kupata ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa. Pinda ameyasema hayo leo Machi 20,2025 katika maadhimisho ya miaka 30 ya Veta ambapo […]
Na Nora Damian, Mtanzania Digital Wamiliki wa shule na vyuo binafsi wametoa mapendekezo kwa Serikali yatakayosaidia kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini. Mapendekezo hayo yametolewa Machi 19,2025 na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (TAPIE), Dk. Mahmoud Mringo, kwenye kongamano la miaka 30 ya Mamlaka ya Mafunzo ya […]
Na Nora Damian, Mtanzania Digital Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo manane kwa wizara, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), taasisi za umma na binafsi kuweka mwelekeo wa kitaifa wa namna ya kuboresha mafunzo ya ufundi stadi hapa nchini. Amesema mafunzo ya ufundi stadi ni nguzo muhimu katika kutengeneza fursa za ajira […]
MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema yuko tayari kumuunga mkono Rais William Ruto endapo ataweka sera bora za kuimarisha sekta ya elimu. Bw Owino ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Ruto alisema anashangaa namna mwanasiasa huyo alivyobadilika tangu aingie mamlakani licha ya kutangaza alivyolelewa maisha ya uchochole. Akiongea kwenye hafla ya elimu huko Malindi, mbunge huyo alisema yuko tayari kushirikiana na Rais endapo ataweka elimu iwe bure. Alimpa changamoto Rais kuweka elimu ya bure kwanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kuwapunguzia Wakenya gharama ya maisha ikiwemo ulipaji karo. “Ulipochaguliwa nilijua kuwa utawatumika Wakenya vizuri sababu ya kule ulikotoka. Ulilelewa kwa biashara ya kuku na mayai, mbona umebadilika? Unataka nikuunge mkono hata uchukue kamba uniweke kwa shingo haina shida, sitafanya hivyo. “Lakini ukileta elimu ya bure nitakuunga mkono,” alisema Bw Owino. Bw Owino alisema mfumo wa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu una ubaguzi akimsihi kuirekebisha ili kuwe na usawa. Mbunge huyo alisema Rais hangelipiga hatua kubwa kimaisha ingalikuwa hakupelekwa shule huku akimsihi kusikia vilio vya Wakenya. “Ulikutana na marehemu Rais Daniel Moi ulipokuwa chuo kikuu sababu ya elimu. Sasa umeleta mfumo mpya wa kufadhili elimu ya vyuo vikuu ambao una changamoto tele, unatekeleza mfumo wa CBC ambayo ina changamoto tele, hakuna maabara na kuna uhaba wa walimu,” akaongeza. Kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022, Rais aliapa kwamba ataondoa mfumo huo na kupiga msasa mfumo wa 8-4-4 lakini alipoingia mamlakani aliunda jopokazi la elimu ambalo lilichukua maoni kwa Wakenya. Zaidi ya asilimia 90 ya Wakenya walikumbatia mfumo wa CBC. “Ukifanya elimu iwe ya bure kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu nitakuunga mkono,” akasisitiza. Bw Owino alijinaki kuwa mwenyewe amewekeza kwenye sekta ya elimu kwa kujenga shule, kutoa basari kwa wanafunzi ili Wakenya wapate elimu bora. Alisema wazazi wanapitia changamoto kulipa karo ya shule kwa watoto wao wanaosoma shule kutwa
KUKOSA kushiriki mapenzi kwa kipindi kirefu kunasababisha matatizo ya kiafya ikiwemo saratani na magonjwa ya moyo, Watafiti wamebaini. Watafiti hao, wanasema kuwa kushiriki tendo la ndoa lenye ubora wa juu, kuna manufaa yake kiafya. Kukosa kufanya hivyo, wanaeleza, kuna athari hasi kiafya ambayo huandamana na shinikizo la damu na maumivu mgongoni. Wanaume wapo pabaya zaidi kwa sababu kukosa kushiriki mahaba pia kunahusishwa na uwezekano wa kupata saratani ya tezi dume. “Watu hukosa kushiriki ngono kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo shughuli nyingi, kutokuwa na mpenzi au kuamua tu kuchukua mapumziko baada ya uhusiano wa awali kuvunjika pamoja na imani ya kidini,” wanasema watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Anglia Ruskin, Cambridge, Uingereza. Kukosa kushiriki ngono kwa kipindi kirefu pia kuna athari zake hasa ki hisia katika uhusiano. “Kusononeka, msongo wa mawazo na wasiwasi kunaweza kutokea kutokana na kukosa kushiriki mapenzi mara kwa mara au ukame wa kipindi kirefu. Ngono pia huimarisha kinga mwilini,” wanaongeza watafiti hao. Wapenzi ambao hawashiriki ngono mara kwa mara huwa hawana mnato imara au dhabiti kati yao. Kushiriki ngono kunasaidia katika kuzalisha homoni zinazofahamika kama oxytocin na endorphins ambazo zinasaidia kuzuia au kudhibiti msongo wa mawazo na matatizo mengine ya kiakili. Homoni ya oxytocin pia huimarisha mnato wa kiakili na kumbukizi kwa kuwa pia inasaidia katika kuhakikisha mtu anapata usingizi mzuri. Ngono pia huimarisha mazungumzo kati ya wapenzi ambao hujawa na furaha pamoja kuweka hisia zao kuwa pamoja na dhabiti. Wataalamu hao hata hivyo wanashauri si lazima wapenzi washiriki ngono kila siku kwa kuwa hata mara moja pekee kwa wiki huwa imetosha. Baada ya kupita umri wa miaka 20, wapenzi wanastahili kufanya mapenzi angalau zaidi ya mara mbili kwa mwezi ili kuzuia matatizo yanayotokea mtu asiposhiriki ngono.
SERIKALI imefanunua kwamba haitakuwa lazima wanafunzi wa Gredi 10, 11, na 12 kusoma masomo hisabati na sayansi. Badala yake wanafunzi hao wana uhuru wa kuchagua masomo wanayotaka kulingana na uwezo na matamanio yao. Wizara ya Elimu imetangaza kuwa kutakuwa na uhuru wa wanafunzi kuchagua masomo wanayotaka kufanya wanapofika shule za sekondari pevu baada ya kukamilisha sekondari msingi. Kwanzia mwaka ujao wanafunzi wa Gredi ya 9 watajiunga na sekondari pevu kulingana na masomo watakayochagua ikiwemo Sayansi, Spoti, (Sayansi jamii, Sanaa na spoti, na Sayansi ya Tekinolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM). “Haitakuwa lazima kwa wanafunzi wa Gredi 10, kuchagua somo la Sayansi wala Hisabati. Watoto wana uhuru wa kuchagua maosmo wanayotaka, tusiwalimbikizie masomo,” alifafanua Katibu wa Elimu Dkt Belio Kipsang. Hata hivyo alisisitiza kuw ani sharti shule zote nchini kuchagua masomo ya sayansi na hesbati ili kuongeza idadi ya wataalam wa tajriba hiyo. Hii ni afueni kwa wanafunzi hao ambao wazazi wao walianza kuuliza maswali kwanini wanalazimika kuchukua masomo hayo ilhali wanapenda masomo mengine kama spoti. Lakini kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Katibu huyo wa Elimu alisema mfumo wa CBC inalenga kumpa mwanafunzi nafasi bora ya kufana kwenye masomo ambayo anapenda tofauti na mtaala wa 8-4-4 ambao masomo ya Hisabati na Sayansi ni lazima. Serikali iliandaa mdahalo wa elimu kutathmini safari hiyo iliyoanza miaka tisa iliyopita. Wanafunzi wa kwanza wa CBC wamefika Gredi ya Tisa. Katibu huyo alisema Jopokazi la Rais la kuthathmini Elimu nchini, lilipendekeza kuwa asilimia 60 ya shule zote za sekondari ya juu zinafaa kuwa na masomo ya sayansi na hesabati. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mombasa Prof Laila Abubakar, ambaye alikuwa kwenye jopokazi, hilo alisema ni sharti shule zote ziwe na masomo ya sayansi na hesabu. “Lakini si lazima wanafunzi wachukue au wachague masomo hayo. Mwanafunzi anaweza kuchagua sporti na afane maishani,” alieleza Prof Abubakar kwenye mdahalo wa elimu. Mwenyekiti wa muungano wa wazazi nchini Bw Silas Obuhatsa, aliwasihi wazazi kuhudhuria mdahalo huo unaoendelea kote nchini ili kutoa maoni yao kuhusu mtaala.
HUENDA wazazi wenye watoto katika vyuo vikuu vya umma humu nchini wakalazimika kugharamika zaidi baada ya serikali kuungama kuwa inapitia changamoto kufadhili masomo hayo. Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi Jumapili alisema serikali inapitia changamoto katika kufadhili masomo katika vyuo vikuu vya umma kutokana na uhaba wa fedha, hazina kuu ya kifedha ikiwa imefilisika. Bw Mbadi alitoa kauli hiyo baada ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Kaunti ya Mombasa kumuuliza kwa nini sekta ya elimu ya juu inapitia changamoto za kifedha. “Kama nchi, imekuwa vigumu kufadhili elimu katika vyuo vikuu. Vyuo vikuu vinahitaji Sh107 bilioni kila mwaka lakini tunaweza kutenga Sh79 bilioni pekee kwa hivyo hapo kuna changamoto. Lakini changamoto kubwa zaidi ni kwamba tunaelimisha watoto ambao wanaweza kugharamia elimu hiyo badala ya kulenga wale ambao hawajiwezi,” akasema waziri huyo. Alitoa mifano ya watoto ambao wanasomea shule za kibinafsi kuanzia chekechea, msingi hadi shule za upili wakitozwa karo ya Sh600,000 kila mihula na wanapofika vyuo vikuu wanataka kufadhiliwa masomo na serikali. Aidha waziri huyo alisema hakuna usawa kati ya mwanafunzi ambaye amesomea shule za kibinafsi kufadhiliwa masomo yake katika chuo kikuu na yule ambaye amesomea shule ya umma maisha yake yote. “Mtoto wa maskini kama mwalimu wa shule ya msingi ni tofauti sana na mtoto wa Waziri Mbadi. Mtoto wa mwalimu anafaa kufadhiliwa masomo yake chuoni huku mtoto wa Bw Mbadi kugharamikia elimu ya mtoto wake, huo ndio usawa,” alifafanua. Alisema ipo haja ya serikali kuwekeza kwenye elimu ya watoto ambao wanatoka familia zilizolemewa na uchochole ili kuleta usawa katika sekta ya elimu. “Kama si elimu ya bure katika vyuo vikuu hii leo nisingelikuwa hapa, nilifaidika na ufadhili huo sababu wazazi wangu walikuwa wachochole. Hata ndugu zangu wakubwa hawangeliweza kunilipia karo ya chuo kikuu sababu walikuwa hawajiwezi kifedha,” alieleza. Hata hivyo, alisema serikali inaweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi ambao hawawezi kufadhili masomo ya vyuo vikuu wanafadhiliwa. Haya yanajiri huku sekta hiyo ya elimu ya juu ikikumbwa na changamoto za kifedha. Wanafunzi wa vyuo vikuu huko Mombasa walikutana katika ukumbi wa Swahilipot hub kujadili changamoto za elimu ya ngazi ya juu. Walieleza wasiwasi wao baada ya mfumo mpya wa kufadhili elimu katika taasisi ya ngazi ya juu iliyoanzishwa na Rais William Ruto mnamo 2023 ilisimamishwa na mahakama ambayo ilisema si kikatiba. Hata hivyo serikali ilikataa rufaa. Aidha Rais Ruto amekuwa akitetea mfumo huo akisema aliuvumbua ili kusaidia vyuo vikuu kupata fedha kutokana na malimbikizi ya madeni ya zaidi ya Sh60 bilioni.
KANDO na kufanya kazi ya ukarani kwa muda mfupi katika miaka miwili kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Fort Hare Afrika Kusini 1948, baada ya kutoka Shule ya Upili ya Alliance 1945, John Njoroge Mungai alikuwa dereva wa basi, akiwasafirisha abiria kati ya Limuru na Nairobi. Mungai ambaye baadaye alikuwa Waziri wa Ulinzi alikumbuka: “Nilipata leseni yangu ya kuendesha Magari ya Uchukuzi wa Umma (PSV) mwaka wa 1946, ambayo nakala yake bado ninaihifadhi. Nilikuwa nikiendesha basi la Chevrolet lenye viti 60 kati ya Limuru na Nairobi kupitia Kikuyu. Kabla ya hapo, nilifanya kazi kwa muda mfupi katika Shirika la British Overseas Airways.” Mungai alizaliwa katika kijiji cha Gichungo kando ya mpaka wa Nairobi na Kiambu mnamo Januari 7, 1926, na wazazi Wakristo, George Njoroge Singeni ole Mbachucha na Leah Gathoni wa Kungu wa Magana. Babake alitoka Narok na mamake alitoka Gatundu. Nyumba ya familia yake ilikuwa ikitumiwa kwa siasa na hata kabla Mungai kuzaliwa, siasa za wakadamizaji na waliokadamizwa zilikuwa katika eneo lao. Nyumba hiyo ilihifadhi wale wote waliotetea haki na maadili ya Kiafrika, kama vile Waiyaki wa Hinga, na 'mtumishi wa wakandamizaji wa kikoloni' kama Chifu Mkuu Kinyanjui wa Gathirimu. "Kuwa kati ya pande mbili zilizopingana ilivutia. Siasa zinazohusu ardhi, elimu na dini zilikuwa utaratibu wa kila siku,” anasema. Anakumbuka kuambiwa jinsi John William Arthur, msimamizi wa ukoloni wa Kanisa la Scotland huko Kikuyu, alijaribu kuwalazimisha wenyeji kuacha mila na tamaduni zao na kufuata za kigeni. "Kwa kweli, kulikuwa na upinzani kutoka kwa wale ambao hawakuona mgongano kati ya Ukristo, elimu, maisha ya kisasa na mila na tamaduni zao," Mungai anasema. Ingawa huenda desturi fulani hazikufaa, mtazamo wa Arthur ulizua mzozo na mgawanyiko wa watu na wafuasi wa kanisa. ”Kundi lililogawanyika, lililoongozwa na Gatungu Gathuna, lilijitenga na dini na kuanzisha shule za kujitegemea zinazojulikana kama Gikuyu Karing'a.Mungai anakumbuka: “Mfumo huu wa elimu baadaye ulizaa wapiganiaji wa uhuru. Wale waliojitenga na Kanisa la Scotland wakawa wapiganiaji wa ardhi iliyotwaliwa na wakoloni na vita vya uhuru,” alikumbuka Mungai. Sababu moja ambayo huenda ilichangia chaguo la Mungai la kazi baadaye maishani inaweza kuwa ukweli kwamba alizaliwa hospitalini wakati ambapo, kwa Waafrika, kujifungulia nyumbani kulikuwa kawaida na ilikuwa vigumu kwenda hospitalini kujifungua. Alieleza : “Mama yangu alikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kwenda shule na kujifunza kusoma na kuandika. Yeye na baba yangu walikuwa washiriki wa Kanisa la Mwenge, Kikuyu, ambako kumbukumbu za kuzaliwa kwangu zilihifadhiwa. Rekodi hizo bado ziko Kanisani na zinaonyesha kuwa mkunga wangu alikuwa Dkt John William Arthur.” Wazazi wake walikuwa Wakristo waaminifu na Mungai alibatizwa mwaka uleule aliozaliwa na katika Kanisa la Torch.
Na Imani Nathanieli, Mtanzania Digital Kampuni ya Mawasiliano ya Halotel imedhibitisha dhamira yake katika uwajibikaji Sekata kwenye jamii baada ya kuwapatia usafiri wa baiskeli wanafunzi wa shule ya Sekondari Visiga iliyoko mkoani Pwani ikiwa ni moja ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Lengo la kufanya hivyo ni kutatua changamoto wanazokumbana nazo wanafunzi katika elimu, […]
MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika ya kurusha mkuki kwa watu walio na ulemavu wa macho (F12/13) Sheila Wanyonyi amefichua kwamba alikuwa na ndoto ya kuwa mhandisi akiwa mtu mzima, lakini haikuwezekana. Licha ya kuzaliwa na ulemavu wa kukosa kuona nyakati kuna giza ama mwangaza mdogo, Wanyonyi amejaa matumaini kuwa anaweza kufikia na hata kufuta rekodi ya dunia iwapo atapata usaidizi muhimu. Wanyonyi alizaliwa katika eneobunge la Bumula, Kaunti ya Bungoma, mwaka 1998 na kusoma katika shule za vipofu za St Francis School for the Blind (Kapenguria, Pokot Magharibi) na Thika High School for the Blind (Kiambu). [caption id="attachment_168923" align="alignnone" width="2000"] Wanyonyi akaza mazoezi kuelekea Olimpiki za Walemavu mwaka jana. PICHA | SILA KIPLAGAT[/caption] Alifuzu na digrii katika Masuala ya Jinsia na Maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta (Nairobi) mwaka 2023. Nilipokuwa mdogo, ndoto yangu ilikuwa kuwa mhandisi. Hata hivyo, nilipogundua watu walio na ulemavu hawawezi kufanya masomo ya sayansi (fizikia na kemia) bali “Adoptive Biology” nilihisi kuchanganyikiwa Wanyonyi hakujua afanye nini baada ya kufahamu hilo. “Nilijaribu kubadilisha kozi yangu nilipojiunga na kidato cha kwanza 2015 katika shule ya Thika School for the Blind. Nikiwa huko tulialikwa kwa mazungumzo kama wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuulizwa taaluma ambayo tungependa kufanya," anatanguliza katika mahojiano. "Hata hivyo, niliposimama na kusema nataka kuwa mhandisi nilififia moyo kuambiwa mtu asiyeona hawezi kufanya kozi hiyo. Hapo ndipo nilijua sisi wenye tatizo hilo hatuwezi kufanya kozi za kemia na fizikia bali Adoptive Biology, ambayo kwangu nilihisi haiwezi kunisaidia sana,” alieleza. Vizingiti kote kote Wanyonyi alipiga moyo konde na kudhani kwa sababu anapenda hisabati angegeukia uhasibu. “Nilivunjwa moyo tena kwamba siwezi fanya kozi hiyo. Kozi pekee nilishauriwa nichague ilikuwa elimu ama sheria. Lakini sikutaka taaluma hizo, wala sikujiona nikisimama mbele ya wanafunzi kufundisha,” asema. Hali ilikuwa ngumu kwake kwa sababu pia alifanya kozi ya mhudumu wa kike katika ndege, ambayo vile vile hakufanikiwa kupata kazi. “Niliamua sasa kuchukua kozi yoyote itakayokubalika. Ulemavu wangu ulifanya niwe hapo tu bila ya chaguo lililonipendeza. Niliendelea na mosomo lakini bila motisha,” anaeleza. [caption id="attachment_168924" align="alignnone" width="2560"] Bingwa huyo wa Afrika avuta gurudumu la kilo sita kama sehemu ya mazoezi yake uwanjani Kasarani, Nairobi, wakati wa mahojiano Februari 25, 2025. PICHA | GEOFFREY ANENE[/caption] Wanyonyi alidhani kuwa anaweza kupata kazi kutokana na kozi za sayansi ya nyumbani ama hisabati, lakini “nikapata kuwa somo ambalo lingenisaidia ni sayansi za jamii ukizingatia changamoto zilizopo.” “Tuliambiwa kuwa mtu asiyeona anaweza kufanya tu ualimu ama sheria. Nilipokamilisha masomo ya shule ya upili niliitwa Chuo Kikuu cha Pan African na pia kile cha Kikatoliki (CUEA). Vyuo hivi vilitaka nifanye saikolojia ya kutoa ushauri nasaha. Hata hivyo, havikuwa na vifaa vya walemavu ndipo nikaamua kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) ambako sasa ninasomea kozi ya masuala ya jinsia. Ilibidi nipende kozi hiyo kwani ndiyo niliangukia," akasema Wanyonyi aliyefuzu na digrii ya Masuala ya Jinsia na Maendeleo kutoka KU mwaka 2023. Akiwa Kenyatta, Wanyonyi alipata kufahamu kuhusu mchezo wa kurusha mkuki. Alifundishwa mchezo huo na Dkt Samwel Litaba ambaye ni kocha wa riadha katika chuo hicho. Alinifundisha jinsi ya kukamata mkuki. Hapo ndipo safari yangu ya kurusha mkuki ilianzia Rekodi zatamba Kabla kuingilia urushaji mkuki Wanyonyi alidhania ni mchezo hatari. Hata hivyo, tangu akite humo mchezo huo umemfanya apande ndege kuenda Ghana, Nigeria, Tunisia, Japan, Ufaransa na Milki za Kiarabu (UAE) kushiriki mashindano. Katika ziara yake majuzi, Wanyonyi alishiriki mashindano ya Dubai 2025 World Para Athletics Grand Prix kule UAE. Alirusha mkuki umbali wa mita 30.40, 35.03m, 27.55m, 25.99m, 29.44m na 24.67m katika mitupo yake sita ya kitengo cha F12. Matokeo hayo yalimwezesha kutwaa taji kwa rekodi mpya ya bara Afrika ya 35.03m. Mchina Yuping Zhao anashikilia rekodi ya dunia kitengo hicho baada ya kurusha mkuki 47.06m alipojishindia dhahabu kwenye Olimpiki za Paris 2024. Lengo langu sasa ni kufikia rekodi ya dunia ikiwezekana kabla Michezo ya Olimpiki ya Walemavu mwaka 2028 Wanyonyi pia analenga kueneza injili ya Olimpiki mashinani. “Walemavu wengi hawana habari kuhusu Olimpiki ya Walemavu. Nataka niwafikie ili tuweze kuimarisha idadi ya wachezaji na pia ushindani,” alihoji Wanyonyi. [caption id="attachment_168925" align="alignnone" width="1280"] Wanyonyi akipasha misuli joto katika uwanja wa Kasarani, Nairobi, mnamo Februari 19, 2025. PICHA | GEOFFREY ANENE[/caption] Alifurahi sana kupata rekodi ya Afrika mjini Dubai mwezi Februari. “Sikuamini macho yangu kwa sababu nilikuwa napata mirusho ya mita 30, 31, 32, 28, lakini nikaandikisha 35," asema. Anaamini anaweza kuimarisha rekodi hiyo yake na hata kuweka mpya ya dunia akipata usaidizi mzuri wa vifaa, kifedha na maandalizi Ilipothibitishwa kuwa rekodi ya Afrika ilinipa motisha tele. Ilinifanya nihisi kwamba naweza kufikia rekodi ya dunia Shujaa wake katika urushaji mkuki ni Andreas Thorkildsen, 42, wa Norway anayejivunia kushinda mataji ya Olimpiki mwaka 2004 na 2008, dunia (2009) na bara Ulaya (2006 na 2010). “Kinachonipendeza kumhusu ni ustadi wake na moyo wa kujituma. Nilisoma kumhusu akiwa bingwa, kufifia na hatimaye kurejea tena kwa kishindo. Sifa hizo ni za kipekee na zinanitia moyo kila siku kama mwanamichezo. Mbinu zake za kurusha mkuki pia bado zinatumiwa na makocha,” akaeleza. Goalball Mbali na kurusha mkuki, Wanyonyi pia ameshiriki mpira wa mikono almaarufu goalball. Hivi majuzi pia alijitosa katika uendeshaji baiskeli. Wanyonyi amejifunza mengi kupitia michezo. “Nimepata nidhamu. Ukiwa mwanamichezo lazima pia ufahamu mambo ya lishe usije ukapigwa marufuku kwa kutumia bidhaa ambazo zina kemikali za kusisimua misuli. Si haki kutumia njia haramu kushinda wenzako. Michezo pia imenifundisha kuepuka maovu pamoja na kuweka malengo na kutia bidii hadi niyatimize,” asema.
Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Mkoani Iringa kimeadhimisha miaka 30 ya VETA na miaka 50 ya ufundi stadi huku ikijivunia muitikio wa wananchi kujiunga na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na chuo hicho. Maadhimisho hayo ya siku mbili yamehitimishwa katika Chuo cha elimu ya mafunzo ya ufundi stadi Mkoani Iringa ambapo pia yalihudhuriwa […] The post Veta Iringa yajivunia miaka 30 ya mafanikio first appeared on Millard Ayo.
Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital Afisa Mkuu Mtaala Mwandamizi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Joyce Kahambe, amewasihi wazazi waendelee kuwahimiza watoto wapende elimu na kuhakikisha wanatumia ujuzi wanaojifunza shuleni katika shughuli za maisha yao ya kila siku, kama vile kilimo, ufugaji, muziki, na nyinginezo, hata kama wanapendelea kufuata taaluma zao rasmi. Dkt. Kahambe […]