Biteko atia neno mjadala wa VETA

Habari Leo
Published: Mar 22, 2025 07:25:30 EAT   |  Educational

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko amesema mjadala unaoendelea kuhusu Mamlaka ya Elimu na…

The post Biteko atia neno mjadala wa VETA appeared first on HabariLeo.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko amesema mjadala unaoendelea kuhusu Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) unaonesha umuhimu wa mafunzo yanayotolewa na kwamba wamefanikiwa kuifanya izungumzwe na itasonga mbele.

Amesema tafiti zinaonesha ukiwekeza Dola moja ya Marekani kwenye ufundi stadi kile utakachokipata ni sawa na Dola nne, maana yake wanapaswa kuwekeza zaidi eneo hilo.

Akifunga maadhimisho ya Miaka 30 ya VETA yaliyofanyika Dar es Salaam, Dk Biteko alisema zipo nyanja tatu muhimu za kufundisha ambazo ni utambuzi, uelekeo na ustadi eneo ambalo ni muhimu kumfanya mtu ajitegemee.

“Kwa mfano, kuna changamoto watoto wanaofundishwa leo baada ya kumaliza kidato cha nne au cha sita ana kitu gani kinachomwezesha aishi kwa elimu hiyo na kukabiliana na changamoto, kiukweli ustadi ni eneo la kuwekewa mkazo watoto wetu waweze kujitegemea sasa na baadaye,’’ alisema Dk Biteko.

Aliongeza: “Ni kawaida mtoto aliyemaliza chuo hawezi kujipikia wala kujifulia mwenyewe anataka kuhudumiwa, unataka kuzalisha maofisa wa kuhudumiwa au kuhudumia. Jambo hili ni hatari kwa taifa na VETA wanaweza kukabili tatizo hilo”.

Alisisitiza utafiti uliofanywa na World Forum ulieleza jamii yoyote inayofanya kazi ya kufundisha lakini haihusianishi stadi katika mafunzo yake, taifa hilo litakuwa linapoteza kati ya asilimia moja hadi sita ya Pato la Taifa kwa mwaka kama hasara kutokana na ukosefu wa ajira na kukosa ujuzi wa kukabili matatizo.

“Nataka kuwaambia hakuna taifa lolote duniani ambalo limeendelea bila kuwa na watu wenye stadi fulani za kutatua matatizo yao, ndiyo maana tunawekeza kwenye ufundi,” alieleza Dk Biteko.

Dk Biteko alisema wasipowekeza kwenye ufundi itawalazimu kutumia gharama kubwa kuchukua watu wenye ujuzi kutoka nje ya nchi.

Alisisitiza maendeleo ya teknolojia yamekuwa tishio katika sekta za uzalishaji ambao umeshuka kwa asilimia 20 huku sekta ya huduma ikipanda kwa asilimia 27.

Pia, alisema asilimia 14 ya kazi ziko hatarini kutoweka kutokana na kuwepo teknolojia mpya zinazopunguza matumizi ya watu kazini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore alisema watasimamia ubora wa mafunzo yanayotolewa na vyuo vya ufundi stadi kuwa na vijana wenye ubora na ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.

Kuhusu ubunifu, Kasore alisema wanatamani serikali iongeze bajeti kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili wabunifu wapate fedha za kuendeleza bunifu zao na kuziuza sokoni.

Alisitiza watarasimisha ujuzi kutoka kwa Watanzania 80,000 kati ya 100,000 ili kutambua kazi zao na kuzipeleka katika soko la ajira.

The post Biteko atia neno mjadala wa VETA appeared first on HabariLeo.