Pinda akoshwa usimamizi Veta, ahimiza vijana kuchangamkia fursa

Mtanzania
Published: Mar 20, 2025 18:23:47 EAT   |  Educational

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema amefurahishwa na kazi inayofanywa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) ya kutoa mafunzo ya ufundi stadi na kuwezesha Watanzania wengi kupata ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa. Pinda ameyasema hayo leo Machi 20,2025 katika maadhimisho ya miaka 30 ya Veta ambapo […]

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema amefurahishwa na kazi inayofanywa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) ya kutoa mafunzo ya ufundi stadi na kuwezesha Watanzania wengi kupata ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa.

Pinda ameyasema hayo leo Machi 20,2025 katika maadhimisho ya miaka 30 ya Veta ambapo pia alitembelea mabanda mbalimbali kwenye viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Amesema ufundi stadi ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na ya maendeleo ya taifa hivyo hakuna mtu yeyote anayeweza kukwepa na kuipongeza Veta kwa kazi kubwa waliyoifanya tangu kuanzishwa kwake.

“Tumeona mambo mengi mazuri, yanaonyesha dhahiri kwamba tulikokuwa siko tulipo, tumepiga hatua kubwa, ufundi stadi pamoja na ubunifu katika maisha ya mwanadamu hawezi kuyakwepa, ni sehemu ya maisha ya mtu, ni sehemu ya maendeleo ya taifa.

“Veta mnastahili kupewa pongezi kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya mpaka sasa, ndani ya mafunzo yanayotolewa utakuta kilimo kipo, ufugaji upo, uvuvi upo. Ukitazama kwenye huduma za jamii afya, elimu yenyewe na vitu vingine mafundi stadi wametoka kwenye vyuo vyetu,” amesema Pinda.

Pinda pia amepongeza ushirikiano uliopo baina ya Veta na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambao utawezesha wahitimu Veta kupata fursa kupitia uwekezaji mbalimbali unaofanywa nchini.

“Nitoe wito kwa vijana watumie fursa hii kwenda kupata maarifa ya ufundi stadi kwenye vyuo vya Veta na vingine vya watu binafsi, na bahati nzuri kuanzia Mkurugenzi Mkuu wa Veta na watendaji wengine ni vijana kwahiyo napata matumaini kwamba fikra zao zinaweza kuwasaidia vijana kutoka walipo na kwenda mbele zaidi,” amesema Pinda.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Veta, CPA Anthony Kasore, amesema Pinda ni kati ya viongozi walioshiriki kuhakikisha mamlaka hiyo inafanikiwa kutoa ujuzi kwa Watanzania ndiyo maana walimualika aje kuona walipotoka na wanakotaka kwenda.

“Tunashukuru sana kwa Waziri Mkuu mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda kuja na kujionea mambo ambayo tunafanya, alisimamia matokeo na maboresho ambayo yameweza kutokea Veta na mengine ambayo sasa hivi tunayaona yamefanyika.

“Katika kuadhimisha miaka 30 tuliona kwa sababu yeye ni mmoja wa watu walioshiriki na kuhakikisha kwamba Veta inatoa ujuzi kwa Watanzania tuliona ni vema nayeye aweze kujionea wapi tulipotoka na tunakotaka kwenda…amekuwa akitushauri katika maeneo mbalimbali ya ujuzi, tunamshukuru sana,” amesema CPA Kasore.