TEWW yaagiza mikoa kukamilisha karakana za IPOSA

Habari Leo
Published: Mar 20, 2025 10:42:29 EAT   |  Educational

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupiti Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imeagiza mikoa inayotekeleza mradi wa…

The post TEWW yaagiza mikoa kukamilisha karakana za IPOSA appeared first on HabariLeo.

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupiti Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imeagiza mikoa inayotekeleza mradi wa IPOSA kuharakisha ujenzi wa karakana 30 za mafunzo pamoja na karakana 3 ambazo zitakuwa ni vituo vya mfano katika mikoa ya Manyara, Shinyanga na Tanga kabla ya Mei 2025.

Hayo yameelezwa katika mafunzo ya walimu na viongozi katika mradi wa mpango wa elimu changamani kwa madhumuni ya kuwapatia fursa za elimu mbadala vijana ambao wako nje ya shule.

Programu inayotekelezwa ni ya elimu ya Integrated Programe For Out -Of- School Adolescents (IPOSA) iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara.

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya watu wazima (TEWW) Profesa Philipo Sanga amesema kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi zoezi la usajili wa wanafunzi  kuanza masomo pia litakuwa limekamilika kwa mikoa 6 ya mpango wa IPOSA.

Mikoa hiyo ni Manyara,Tanga, Shinyanga,Simiyu,Singida na Pwani chini ya ushirikiano wa shirika la kimataifa la  Korea(KOICA) na ofisi ya Rais TAMISEMI.

“Tuko nyuma ya programu ya IPOSA sisi TEWW tumekwisha andaa mitaala na kuwajengea  uwezo walimu, viongozi na wasimamizi ili waweze kutekeleza.majukumu yao kupitia ujenzi wa karakana hizo hivyo ni muhimu zikamilike”Amesema Sanga.

Mpango wa IPOSA unalengwa na Taifa kuwa njia ya kufikisha elimu mbadala kwa vijana ambao walishindwa kupita katika njia ya mfumo rasmi wa elimu kusudi wasiachwe pasipo msaada au mwelekeo wa elimu.

” Kupitia programu hii mkoani Manyara jumla ya  viongozi  na wasimamizi 60 wamejengewa uelewa wa programu ya IPOSA itakayowasaidia kutekeleza majukumu ya usimamizi na uongozi”Amesema Sanga.

Kwa mujibu wa Sanga asilimia 18.2 ya idadi ya watu wazima hawana stadi za kusoma kuandika na kuhesabu(KKK) hivyo Programu ya IPOSA itashughulikia  pamoja na na kutoa mafunzo ya ujasiriamali,amali au ufundi na stadi za maisha ambapo vijana 42,183 wamenufaika hadi sasa.

The post TEWW yaagiza mikoa kukamilisha karakana za IPOSA appeared first on HabariLeo.