Chuo Kikuu Huria kuanzisha Shahada ya Utamaduni

Habari Leo
Published: Mar 22, 2025 09:07:30 EAT   |  Educational

MKURUGENZI wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Boniface Kadili amekipongeza Chuo kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kuanzisha…

The post Chuo Kikuu Huria kuanzisha Shahada ya Utamaduni appeared first on HabariLeo.

MKURUGENZI wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Boniface Kadili amekipongeza Chuo kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kuanzisha Shahada ya Umahiri katika usimamizi wa rasilimali za utamaduni.

Kadili amezungumza hayo wakati akifungua kikao cha kupitia rasimu ya mtaala wa shahada hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi za Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba jijini Dodoma juzi.

Alisema anakishukuru OUT kwa kuendelea kutambua umuhimu wa kuenzi, kudumisha, kurithisha na kutunza amali za urithi wa utamaduni ambapo kupitia programu hii pia, itaondoa ombwe linalowakwamisha maofisa utamaduni kujiendeleza kitaaluma wakiwa katika maeneo yao ya kazi.

“Serikali kupitia wizara hiyo inatambua mchango wa taasisi za elimu ya juu, kutokana na mabadiliko ya sera, miundo na sheria hivyo natoa wito kwa maofisa utamaduni nchini, kutumia fursa hizi kujiendeleza kitaaluma ili kuongeza ufanisi na weledi katika majukumu yao,” alisema Kadili.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Jamii, Historia na Philosophia, Dk Jacob Lisakafu alisema shahada hiyo inalenga kuboresha maadili pia, kusaidia watahiniwa kujiajiri kupitia utalii wa utamaduni kwani itajumuisha kozi zinazohusu ujasiriamali na maadili ya viongozi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau wengine kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Uhasibu Arusha na maofisa utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

The post Chuo Kikuu Huria kuanzisha Shahada ya Utamaduni appeared first on HabariLeo.