Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo manane kwa wizara, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), taasisi za umma na binafsi kuweka mwelekeo wa kitaifa wa namna ya kuboresha mafunzo ya ufundi stadi hapa nchini.

Amesema mafunzo ya ufundi stadi ni nguzo muhimu katika kutengeneza fursa za ajira ndiyo maana Serikali imeendelea kuwekeza katika eneo hilo kwa kuongeza bajeti ya Veta kutoka Sh bilioni 54 mwaka 2021 hadi kufikia Sh bilioni 85 mwaka 2024/2025.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Machi 18,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 30 ya Veta ambapo alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema mafunzo yazingatie mahitaji ya soko la ajira kwa kufanya tafiti za mara kwa mara kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na mashirika ya kimataifa.

“Ni muhimu kwa Veta kuendelea kujiimarisha ili kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia, hakikisheni mnatoa mafunzo ya ufundi stadi yanayoendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kuhakikisha yanajumuisha ujuzi, teknolojia ya kisasa na kuchochea uzalishaji wenye tija,” amesema Majaliwa.

Aidha amaeiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais – Tamisemi pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha vyuo vya ufundi 65 vinavyoendelea kujengwa na Serikali vinakamilika haraka ili kuongeza fursa za mafunzo kwa vijana.

Vilevile ameitaka Veta kutangaza fursa za mafunzo zilizopo ili vijana waweze kuzitumia kwa kuwa wengi hasa walioko vijini hawana taarifa za fursa zilizopo za mafunzo ya Veta.

Maagizo mengine ni kwa taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi stadi kuhakikisha zinashirikiana na viwanda, waajiri na mashirika mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kutoa fursa za mafunzo kwa vijana kulingana na mahitaji ya soko la ajira.

Pia amewataka wazazi kutumia fursa za mafunzo ya ufundi stadi zilizoko nchini kupitia vyuo vilivyojengwa kwenye mikoa na wilaya kwa kuwapeleka vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kujishughulisha na kujipatia kipato.

Waziri Mkuu ametoa rai kwa mashirika ya kimataifa na washirika wa maendeleo kuendelea kuchangia vifaa na fedha na ushauri wa kitaalamu na kuanzisha programu mbalimbali za kubadilishana taarifa ili kuibua teknolojia, mbinu mpya na kuboresha ubora wa mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya ufundi stadi hapa nchini.

“Nitoe wito kwa Watanzania wote na taasisi za umma kuwaunga mkono wazalishaji wetu na wajasiriamali walioko nchini, kwa kununua bidhaa zao na kuzitumia ili kuwawezesha kuendekeza uzalishaji wa bidhaa hizo na kushiriki katika ujenzi wa uchumi na kukuza mapato yao binafsi na taifa kwa ujumla,” amesema Majaliwa.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema ujenzi wa vyuo vya Veta unaendelea katika wilaya 64 na Mkoa wa Songwe na kwamba watahakikisha vinakamilika haraka ili vianze kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Veta, CPA Anthony Kasore, amesema wameanza kushirikiana na wazalishaji na wenye viwanda ili kuwawezesha wanafunzi wapya kupata ujuzi zaidi kutoka kwa mafundi bobezi.

“Katika kuzidi kuimarisha mfumo wa utoaji elimu ya ufundio stadi nchini Veta inaimarisha mahusiano yake na wazalishaji na wenye viwanda ili kuongeza ujuzi kwa wanafunzi,” amesema CPA Kasore.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, amesema yeye ni miongoni mwa wanufaika wa Veta ambaye alipata ujuzi wa kutengeneza viatu kazi anayoendelea kuifanya mpaka sasa na kuipongeza Serikali kwa kujenga vyuo hivyo kwa kuwa vinapunguza wimbi la ukosefu wa ajira nchini.