Wamiliki vyuo binafsi wataja mbinu kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Wamiliki wa shule na vyuo binafsi wametoa mapendekezo kwa Serikali yatakayosaidia kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini. Mapendekezo hayo yametolewa Machi 19,2025 na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (TAPIE), Dk. Mahmoud Mringo, kwenye kongamano la miaka 30 ya Mamlaka ya Mafunzo ya […]
Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wamiliki wa shule na vyuo binafsi wametoa mapendekezo kwa Serikali yatakayosaidia kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Mapendekezo hayo yametolewa Machi 19,2025 na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (TAPIE), Dk. Mahmoud Mringo, kwenye kongamano la miaka 30 ya Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) linalofanyika jijini Dar es Salaam.
Dk. Mringo ambaye aliwasilisha mada kuhusu Utoaji wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika taasisi binafsi; Falsafa, mafanikio, changamoto na matarajio amesema gharama kubwa za uendeshaji zimesababisha huduma ya elimu katika sekta binafsi kugharimu fedha nyingi.
“Gharama ya mtaji wa kuanzisha vyuo ni kubwa, ili uweze kujenga chuo kizuri cha Veta unatakiwa uwe na bilioni moja na ili uweze kuirudisha fedha hiyo itakuchukua miaka 30.
“Kama fedha hizo umezichukua benki ina maana utalipa bilioni 10 ndani ya miaka 30, kwahiyo mwanafunzi anapoingia analipa gharama halisi za kusoma Veta pamoja na zile bilioni tisa zilizoongezeka.
“Badala ya kulipa laki sita ili asome Veta itabidi alipe milioni moja na laki mbili ili laki sita zingine zilipie gharama ya mtaji, kwahiyo kama tungepata benki ambayo inaweza kukopesha kwa gharama ndogo tungeweza kutoa elimu kwa nusu ya bei iliyoko sokoni sasa hivi,” amesema Dk. Mringo.
Dk. Mringo ameshauri pia suala la kodi mbalimbali zinazotozwa na Serikali liangaliwe upya na wanafunzi wanaosoma Veta nao wapatiwe mikopo ya elimu kama inavyofanyika kwa elimu ya juu na vyuo vya kati.
Mwenyekiti hiyo pia amependekeza mitaala ianze kumtambua mtu katika ujasiriamali wake kisha afundishwe anachokitaka.
“Mitaala haimfundishi mtu kuwa mjasiriamali au mtu anayejibeba, inaendelea kung’ang’ania mtu afundishwe akawe mwajiriwa. Nchi hii hatutaweza kuajiri watu wote kwa kutegemea mfumo mmoja wa Serikali, ujasiriamali unatakiwa iwe dhana mama na shirikishi,” amesema.
Amependekeza pia kuwe na bima ya elimu ili watu waweze kupata elimu bora.
Naye Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo wa Veta, Dk. Abdallah Ngodu, amesema wanaendelea kujenga uelewa kwa jamii ili ione umuhimu wa mafunzo ya ufundi stadi bila kujali viwango vyao vya elimu kwani ni fursa kubwa ya kupata maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet), Dk. Mwajuma Lingwanda, amesema elimu ya ufundi ni muhimu kwani inaangalia zaidi msingi wa ubora wa elimu unaotolewa na matokeo wanayopata wahitimu.
Aidha amesema kipimo cha wale wanaohitimu ni kuangalia maarifa na ujuzi walioupata, uhitaji wao katika soko la ajira jambo linalotoa taswira ya umuhimu wa mafunzo ya elimu ya ufundi nchini.