Na Malima Lubasha, Serengeti

Vijana 112 wa kundi rika (Saiga) katika Kijiji cha Mbirikiri Kata ya Sedeco Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, kwa kushirikiana na wazee na wanawake wamekubaliana wejenge nyumba mbili za walimu kwa nguvu zao zitakazogharimu sh 12 milioni kutokana na changamoto ya uhaba wa nyumba unaoikabili shule ya msingi Mbirikiri

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, ,Hamisi Mega amesema hayo wakati alipozungumza na Mtanzania Digital ofisini kwake kuhusu upungufu wa miundombinu mbalimbali inayokabili shule hiyo hasa nyumba za walimu.

Amesema kuwa kutokana na changamoto hiyo aliitisha mkutano wa wananchi na wazazi wa kijiji hicho kwa kushirikisha uongozi wa kijiji kujadili changamoto zinazokabili shule hasa nyumba za walimu ambapo katika maazimio yaliyopitishwa na mkutano huo ilikubaliwa vijana waliotoka jandoni hivi karibuni ndiyo wapewe jukumu la kujenga na kukamilisha ujenzi ndani ya miezi mitatu.

Viongozi wa Kijiji na Shule ya Mbirikiri wakiwa katika mkutano na wananchi kujadili

ujenzi wa nyumba mbili za walimu.

“ Tunapendekeza vijana hao wa Saiga ndio wawe wasimamizi wa kukusanya fedha za michango, kusomba mchanga, kokoto, matofali, mawe na gharama za fundi kwani kwa mujibu wa mila na desturi za kabila letu saiga ni wasimamizi wazuri katika kudhibitiana ,” amesema Mega.

Mega amesema katika kufanikisha ujenzi huo ilikubaliwa kuwa kundi la wazee na akina mama kila mmoja atachanga sh 6,000, kundi la akina baba na vijana litatoa sh 11,000 ambapo viashiria na ukusanyaji wa fedha watasimamia vijana hao.

Wananchi wa Kijiji cha Mbirikiri Kata ya Sedeco Tarafa ya Rogoro Wilaya ya Serengeti wakiwa katika mkutano kujadili maendeleo ya shule na changamoto ya miundombinu ya nyumba inayoikabili shule

Amesema kilichowasukuma vijana hao wa Saiga kupendekezwa na mkutano huo ni taarifa aliyowasilishwa na mwalimu mkuu kuhusu upungufu wa nyumba za walimu unaokabili shule yao ndipo wananchi wa kakubaliana kuhamasishana kujenga nyumba hizo hadi kukamilika kwani uhaba uliopo ni nyumba nane na hizo mbili zitapokamilika upungufu utakuwa nyumba sita.

Mwalimu Mega amesema makundi rika yote maarufu Saiga yanahusika na ujenzi huo tayari kwa sasa wamekamilisha kuchimba na kujenga misingi miwili na viashiria vipo kama vile tofali na fedha zipo ujenzi unaendelea kwani walimu sita ndiyo wenye nyumba huku wengine wakiishi kwa kuchangia.

Aidha Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Yohana Senteu amesema uongozi wa kijiji kwa kushirikiana na mwalimu mkuu wa shule watasimamia kwa weledi mkubwa miradi yote ya sekta ya elimu na mingine inayoletwa katika kijiji kuitekeleza nakuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli zote za maendeleo .

Naye mwenyekiti kijiji hicho William Mwita amesema kuwa taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto ya kukosa umeme kwani nguzo zimeishia uwanja wa michezo wa shule hivyo hakuna sababu shule kushindwa kutopata nishati ya umeme hata hivyo ofisi ya kijiji na shule inafuatilia jambo hilo.