Elimu haki za binadamu kuingizwa kwenye mtaala

Habari Leo
Published: Mar 21, 2025 11:01:05 EAT   |  Educational

DODOMA: SERIKALI ya Tanzania inakusudia kuingiza elimu ya haki za binadamu katika mtaala wa shule na vyuo ili…

The post Elimu haki za binadamu kuingizwa kwenye mtaala appeared first on HabariLeo.

DODOMA: SERIKALI ya Tanzania inakusudia kuingiza elimu ya haki za binadamu katika mtaala wa shule na vyuo ili kupunguza matukio ya ukiukwaji wa haki hizo nchini.

Hatua hii inalenga kustawisha utu, heshima, ulinzi na ukuaji wa haki za binadamu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, ameeleza hayo jijini Dodoma katika mafunzo ya Wanachama Wapya wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), ambapo amesema kuwa uamuzi huo umetokana na ombi la THRDC kwa Wizara ili kuhakikisha elimu ya haki za binadamu inafundishwa mashuleni na vyuoni kwa kina.

“Wizara itatekeleza ombi hili kwa kuliingiza katika sera ya elimu na sheria ya elimu ili kuwe na somo rasmi la haki za binadamu nchini,” amesema Maswi.

Aidha, amebainisha kuwa wizara inaangalia uwezekano wa kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa walio na kesi katika Mahakama ya Rufani ili kuhakikisha haki zao zinazingatiwa. Ambapo amesisitiza luwa wizara iko tayari kupokea mapendekezo ya maboresho ya sheria ili yaendane na uhalisia wa utendaji kazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amewataka wanachama wapya wa THRDC kuwa wavumilivu na kutoogopa changamoto zinazotokana na kazi hiyo ya utetezi wa haki.

“Katika kazi ya kutetea haki, kuna changamoto nyingi, ikiwemo kutengwa au kutafsiriwa vibaya hata na watu wa karibu. Lakini msivunjike moyo, endeleeni kusimamia ukweli na haki,” amesema wakili Mwabukusi.

Naye Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesisitiza kuwa uwepo wa watetezi wa haki za binadamu umechangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haki nchini. Ameongeza kuwa wanachama wa mtandao huo wamekuwa wakifanya kazi kubwa kusaidia serikali, hususan Rais Samia Suluhu Hassan, katika utoaji wa misaada ya kisheria.

Mafunzo hayo, yaliyofanyika jijini Dodoma kwa siku mbili yalilenga kuwawezesha wanachama wapya wa THRDC kupata maarifa kuhusu tathmini ya hatari, usimamizi wa taasisi, na uzingatiaji wa sheria katika utendaji wao wa kazi.

The post Elimu haki za binadamu kuingizwa kwenye mtaala appeared first on HabariLeo.