Majaliwa: Tumewekeza makubwa elimu

Habari Leo
Published: Mar 22, 2025 07:47:19 EAT   |  Educational

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imeweka kipaumbele kikubwa cha uwekezaji katika sekta ya elimu nchini, kujenga jamii…

The post Majaliwa: Tumewekeza makubwa elimu appeared first on HabariLeo.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imeweka kipaumbele kikubwa cha uwekezaji katika sekta ya elimu nchini, kujenga jamii madhubuti yenye kujitambua, kujitegemea, kujiheshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu.

Ameyasema hayo alipomwakilisha, Rais Samia Suluhu Hassan katika harambee ya ujenzi wa maktaba ya kisasa, ukumbi wa mikutano na madarasa ya amali ya Shule ya Seminari ya Agape inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini.

Katika harambee hiyo iliyofanyika Dar es Salaam, zaidi ya Sh milioni 600 zilikusanywa, ikiwa ni ahadi na fedha taslimu.

Majaliwa alisema sekta ya elimu ni wakala wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni katika kuleta maendeleo ya nchi.

“Harambee hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba tunafanya uwekezaji mkubwa katika elimu ya watoto wetu. Maktaba na madarasa ya amali katika Sekondari ya Agape yataleta manufaa mengi yenye tija kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla,” alieleza Majaliwa.

Alisema ni muhimu kutambua kwamba bila ya uwekezaji mzuri katika elimu, hatuwezi kufika mbali.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia imejizatiti kuunga mkono juhudi za taasisi zinazochangia katika ujenzi wa Taifa letu,” alisema Majaliwa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Alisema ili kuwa na vijana wenye maarifa na ujuzi wa kukabiliana na changamoto za kijamii, kitaifa na kimataifa inahitaji kuwa na sekta ya elimu iliyo bora, imara na inayokidhi mahitaji ya jamii.

Waziri Mkuu pia, alisema ili kuongeza fursa za elimu kwa Watanzania wote, serikali imeongeza idadi ya shule za msingi kutoka 16,656 mwaka 2020 hadi 19,783 mwaka 2024 na shule za sekondari kutoka 5,001 mwaka 2020 hadi 5,926 mwaka 2024.

Naye Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alilipongeza KKKT kwa kushirikiana na serikali katika kuendeleza sekta ya elimu nchini.

Awali, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk Fredrick Shoo alitumia fursa hiyo kuipongeza serikali kwa kazi nzuri ya maboresho ya sekta ya elimu nchini.

Akizungumzia kuhusu harambee hiyo, alisema inalenga kukusanya Sh bilioni 1.1 za ujenzi wa maktaba ya kisasa, madarasa ya amali pamoja na ukumbi anuai katika Seminari ya Agape ili kuunga mkono maboresho yaliyofanyika katika sera ya elimu.

The post Majaliwa: Tumewekeza makubwa elimu appeared first on HabariLeo.