Wawekezaji wasifu mazingira ya biashara Tanzania

DAR ES SALAAM – WAWEKEZAJI wa kigeni wameisifu Tanzania kwa kurahisisha mazingira ya uwekezaji hatua inayowawezesha kuanzisha na kusajili kampuni zao kwa haraka na kuanza shughuli rasmi bila vikwazo. Akizungumza katika uzinduzi wa Tawi la Kampuni ya Teknlojia ya Spidd Africa nchini, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni hiyo, Catherine Kisaka, alisema Tanzania imeonesha …
DAR ES SALAAM – WAWEKEZAJI wa kigeni wameisifu Tanzania kwa kurahisisha mazingira ya uwekezaji hatua inayowawezesha kuanzisha na kusajili kampuni zao kwa haraka na kuanza shughuli rasmi bila vikwazo.
Akizungumza katika uzinduzi wa Tawi la Kampuni ya Teknlojia ya Spidd Africa nchini, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni hiyo, Catherine Kisaka, alisema Tanzania imeonesha nia ya dhati ya kuvutia wawekezaji kupitia sheria rafiki na mifumo rahisi ya usajili.
“Hatujapata ugumu wowote. Sheria za uwekezaji zimerahisishwa na utaratibu uko wazi. Ukiwasilisha nyaraka zako kwa ukamilifu, unapewa nafasi mara moja. Kama Spidd, hatukutana na changamoto yoyote kuingia kwenye soko la Tanzania,” alisema Kisaka.
SOMA ZAIDI: Vyuo vikuu vyashauriwa kuzingatia ubunifu, teknolojia
Kampuni hiyo yenye makao yake makuu nchini Uganda, inalenga kukuza biashara na kubadilisha namna biashara zinavyoendeshwa kutumia suluhisho bunifu za kidijitali.
Kasanga amesema kuingia kwa kampuni hiyo nchini ni hatua muhimu kusaidia biashara barani Afrika kuongeza ufanisi, kuimarisha ulinzi wa kimtandao, na kustawi kidijitali kuanzia kwa wajasiriamali wadogo hadi kwa mashirika makubwa.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Spidd Uganda, Angela Semwogerere, alisema kuwa kampuni hiyo imejikita pia katika kutoa elimu na mafunzo kwa taasisi mbalimbali ili kukabiliana na changamoto za usalama wa kimtandao.
“Katika kipindi hiki ambacho kuna changamoto kubwa ya udukuzi na udanganyifu wa kifedha, tunasaidia taasisi hasa za kifedha kujikinga na mashambulizi ya kimtandao. Tunatoa mafunzo ya namna ya kugundua, kuzuia na kukabiliana na vitisho hivyo,” amesema.
SOMA ZAIDI: Watafiti wafundwa matumizi ya teknolojia
Semwogerere aliongeza kuwa Tanzania imekuwa kitovu muhimu cha maendeleo ya teknolojia na uchumi katika Afrika Mashariki, hali iliyochochea uamuzi wa kampuni hiyo kuwekeza nchini.
“Tunaiona Tanzania kama kitovu cha teknolojia Afrika Mashariki. Maendeleo ya kidijitali yanaenda kwa kasi sana, na hiyo ni fursa kubwa kwetu kushirikiana na taasisi mbalimbali kutoa suluhisho za kidijitali kwa biashara za Kiafrika,” alieleza.