Watatu wa familia moja wafariki kwa ajali Chato

WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia kwenye ajali ya gari iliyotokea katika barabara ya Mganza-Chato eneo la…
The post Watatu wa familia moja wafariki kwa ajali Chato appeared first on HabariLeo.
WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia kwenye ajali ya gari iliyotokea katika barabara ya Mganza-Chato eneo la kijiji cha Nyakabale kata ya Mganza wilayani Chato mkoani Geita.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Safia Jongo ametoa taarifa kwa waandishi wa habari na kueleza ajali hiyo ilitokea Aprili 02 2025 majira ya saa mbili usiku.
Kamanda Jongo amesema waliofariki ni watembea kwa miguu watatu ambao ni mwanaume, mwanamke na mtoto aliyekuwa mgongoni lakini bado hawajatambuliwa na inadaiwa ni familia moja waliohamia hivi karibuni.
Amesema baada ya ajali, dereva aliyekuwa akiendesha gari iliyowagonga watu hao ambaye hakufahamika jina lake alikimbia na gari na kutokomea kusikojulikana.
Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa Kituo cha Afya cha kata ya Muganza wilayani Chato kwa ajili ya taratibu za uchunguzi na utambuzi.
“Jeshi la Polisi linamshikilia Abel Josephat (43), Msukuma, Mkazi wa Nyamirembe wilayani Chato kwa tuhuma ya kupiga picha miili ya watu waliofariki katika ajali hiyo na kuzisambaza kwenye mtandao wa kijamii (Instagram)”.
Kamanda amesema picha hizo zilisambazwa zikiwa na maudhui yasiyokubalika kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na chunguzi wa matukio hayo mawili unaendelea kufanyika kwa kuwashirikisha wataalamu.
“Jeshi la Polisi linamtaka dereva na mmiliki wa gari hilo kujisalimisha mara moja katika Kituo chochote cha Polisi kwa ajili ya hatua za kisheria.
“Aidha, tunawataka wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo watabaini uwepo gari iliyopata ajali katika maeneo yao”, amesisitiza Kamanda Jongo.
The post Watatu wa familia moja wafariki kwa ajali Chato appeared first on HabariLeo.