Washauri taasisi za fedha kuwa nguzo Dira 2050

Habari Leo
Published: Dec 19, 2024 13:10:50 EAT   |  Business

WADAU wa sekta ya fedha na Umoja wa Mabenki nchini Tanzania (TBA) wameitaka Dira ya Taifa ya Maendeleo…

The post Washauri taasisi za fedha kuwa nguzo Dira 2050 appeared first on HabariLeo.

WADAU wa sekta ya fedha na Umoja wa Mabenki nchini Tanzania (TBA) wameitaka Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ijumuishe taasisi za kifedha kuwa moja ya nguzo kutokana na umuhimu mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi.

Hayo yalielezwa hapo Desemba 18,2024 Dar es salaam katika mkutano uliofanyika kati ya Timu Kuu ya Uandishi wa Dira ya Taifa kutoa nafasi kwa Taasisi za Kifedha Kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akiwasilisha maoni na mapendekezo kwa niaba ya taasisi za kifedha Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Tuse Joune alisema kama wamepewa nafasi ya kuelezea wanajotamani kiwa katika dira ya maendeleo alisema walitamani sekta ya fedha iwekwe kama moja ya nguzo kwa sababu ya umuhimu wao katika maendeleo ya kiuchumi.

Akifafanua sababu ya kutamani sekta yao kuwa moja nguzo alisema ukiangalia katika kipindi cha ukuaji wa uchumi wa uingereza mwanzoni mwa karne ya 20 taasisi za fedha walizokuwa nazo zilikuwa zikisaidia serikali, zilisaidia uzalishaji, utaratibu wa kubadilishana usambazaji na kufanya biashara ya kimataifa.

Joune aliongeza kuwa hata ukiangalia katika maendeleo ya baadhi ya nchi kama vile katika China, Singapole, Brazil na Indonesia kwa ufupi nchi nchi nyingi ambazo zimekuwa kiuchumi kwa kasi wamekuwa wakizingatia kuhakikisha sekta ya fedha inasaidia katika shughuli zote za uzalishaji na uendeshaji.

“Kwahiyo wangeipa uangalizi maalumu sekta ya benki kwani hakuna ambaye anabisha kuwa sekta ya benki ndiyo kichocheo cha ukuaji wa uchumi na hilo ndilo nia yetu kubwa ya kuona katika dira hii ya 2050 na kama tungeambiwa kuweka kwenye aya moja hiki ndicho tungekieleza,” alisema Joune.

Aidha, Joune alisema kuwa dira wanapendekeza kuwa dira iweke mkazo wa umuhimu wa taasisis za kifedha za maendeleo kama TIB, TADB, na TMRC kupata msaada wa serikali ili ziweze kupata ufadhili wa muda mrefu kwa miradi mikubwa, kwani kwa sasa imekuwa changamoto.

Pia alisema wanapendekeza dira imeweka msingi madhubuti na mifano halisi katika sekta ya kifedha, mawasiliano ya simu, afya, na usafirishaji na kusisitiza wanapaswa kuwekeza vya kutosha na ya kimkakati katika eneo hilo ili kupata manufaa halisi.

Joune alisema wanapendekeza dira iweke misingi madhubiti ya matumizi ya teknolojia na sayansi kwani teknolojia inatoa suluhisho la changamoto za uzalishaji, kuongeza thamani, na usambazaji wa bidhaa, huku ikiimarisha uwezo wa ukuaji wa sekta za kiuchumi na kijamii nchini.

Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia katika sekta ya kifedha si muhimu tu kwa kuboresha huduma za kifedha bali pia kwa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya kifedha na sekta nyingine zenye kipaumbele katika Dira ya 2050.

Kwa upande mwingine Joune ametaja maeneo kadhaa yanayohitaji kuimarishwa katika Rasimu ya Dira ya Maendeleo 2050, ikiwamo eneo la ufadhili wa ubunifu.

Aidha, Joune alisema rasimu iweke msisitizo juu ya umuhimu wa masuala ya Mazingira, Jamii, na Utawala (ESG) kama sehemu muhimu ya Dira 2050, kwani masuala hayo ni muhimu si tu kwa sekta ya kifedha bali pia kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Pia walisema wanaomba kujua kuhusu Mpango Mrefu wa Utekelezaji ‘Long Term Perspective Plan’ kwamba ni kitu gani, kinahuzu nini, imeandaliwa na nani, inachukua muda gani kuandaa na ushirikishwaji wa sekta binafsi upo vipi.

Makamu Mwenyekiti wa Timu Kuu ya Uandishi wa Dira, Joseph Semboja alisema kuwa lengo kuu la kuita kikao hicho ni kusikia maoni ya nini kundi husika wanachohitaji kiongezeke kwa ajili ya kuboresha rasimu mpya itakayotoka baada ya uhakiki.

Alisema dira ni kama njozi ya kitu wanachotamani kitokee, hivyo ndo maana haiwezi kuongelea utekelezaji wake kiundani sana kwa sababu mambo hayo ni ya kimkakati zaidi na ndiyo sababu kutakuwa na huo mpango mrefu wa utekelezaji ili kuelezea mikakti huyo kiundani zaidi.

Pia walipendekeza kuwa dira iweke mikakati kuhakikisha idara za kifedha zinasimama na zinapewa kipaumbele kwenye masuala ya ushuru kwani baadhi zinakufa na wanakuja watu kutoka nje kusaidia kuzinyanyua na kuoewa masharti magumu wanayoshindwa kuyatimiza.

Waliongeza kuwa wenye Dira liwekwe hadharani neno Rushwa, iwe kwenye misingi mikubwa, ile misingi ya kuibeba Dira 2050 kutengeneza jamii ambayo haina rushwa.

Katika hatua nyingine, walisema kuna haja ya kufanyia mageuzi suala la rasilimali watu kabla hata ya dira kukamilika, huku akishauri Serikali kujenga nguvu kazi kwa watoto kuanzia mashuleni ili kupata wataalamu wazawa na kutotegemea watu kutoka nje.

Aidha, waliwataka Watanzania wakiwemo viongozi kupuka dhana ya kuwa Watanzania hawawezi kufanya vitu kwa kuhakikisha watoto wanaandaliwa vizuri na kuondoa dhana ya utegemezi kwa mataifa mengine.

The post Washauri taasisi za fedha kuwa nguzo Dira 2050 appeared first on HabariLeo.