Wanawake wasifu fursa za korosho Mtwara

Habari Leo
Published: Nov 02, 2024 10:55:19 EAT   |  Business

BAADHI ya wajasiliamali wanawake wanaojishughulisha na biashara mbalimbali eneo la ghala ya kuhifadhia korosho ghafi (OLAM) Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wamesema, kitendo cha korosho kuzaa kwa wingi msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025 ni fursa kubwa kwa wanawake hao na wananchi kutoka ndani na nje ya mkoa huo kwa ujumla. Wakizungumza katika manispaa hiyo, …

The post Wanawake wasifu fursa za korosho Mtwara first appeared on HabariLeo.

BAADHI ya wajasiliamali wanawake wanaojishughulisha na biashara mbalimbali eneo la ghala ya kuhifadhia korosho ghafi (OLAM) Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wamesema, kitendo cha korosho kuzaa kwa wingi msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025 ni fursa kubwa kwa wanawake hao na wananchi kutoka ndani na nje ya mkoa huo kwa ujumla.

Wakizungumza katika manispaa hiyo, wafanyabiashara hao wanaofanya kazi yao hiyo kwenye eneo hilo la Olam, wamesema neema hiyo ya korosho kuzaa kwa wingi kwenye msimu huo imekuwa tofauti na misimu mingine iliyopita hali inayochangia mzunguko wa biashara kuwa mkubwa kwasababu kila siku wana uhakika wa kipato kupitia biashara zao.

Mfanyabiashara anayejishughulisha na uuzaji wa maji baridi katika eneo hilo na mkazi wa Mtaa wa Kisutu katika manispaa hiyo, Binae Manzi amesema kupitia korosho wanawake wanapata fursa ya kufanyabiashara ndodo ndogo na kujiingizia kipato na kwa msimu huo mazingira ya biashara yamekuwa mazuri ikilinganishwa na misimu iliyopita.

‘’Msimu wa mwaka huu umekuwa tofauti sana na misimu iliyopita kwasababu korosho zimezaa sana huko mashambani kwahiyo watu kutoka maeneo mbalimbali wamekuja mtwara katika msimu kwahiyo mji umechangamka na mzunguko wa biashara unakwenda sana tu, sasa hivi wanawake wengi tuko hapa Olam tunachangamkia fursa ya biashara ’’amesema Binae.

Mkazi wa Mtaa wa Mtepwezi katika manispa hiyo, Asia Juma ambaye ni mfanyabiashara wa matunda katika eneo hilo, amesema  licha ya korosho kuzaa kwa wingi katika msimu huo lakini ameipongeza serikali kwa kuruhusu korosho zote zinazolishwa mikoa ya kusini kusafirishwa kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) mkoani mtwara hali inayochangia tija katika uchumi wao na familia zao.

‘’Tunamshukuru sana Rais Samia kuruhusu korosho kupitia huku kwasababu biashara zimechangamka hazilali kila siku tunauza tunamaliza na tunapata faida hasaa, mfano mimi binafsi kwa siku napata kati ya Sh 30,000 kupitia biashara yangu hii kwahiyo tunaishukuru sana serikali yetu,’’amesema Asia.

Aidha wamepongeza kitendo cha serikali kuweka bei mzuri ya korosho katika msimu huo kwani kimechangia uwepo wa fursa kubwa ya kiuchumi mkoani humo kwasababu mzunguko wa biashara umekuwa mzuri ikilinganishwa na bei ya korosho ilivyokuwa katika msimu iliyopita hivyo wameendelea kuiomba serikali kuwa bei hiyo isiishie kwa msimu huo  wa mwaka 2024/2025 tu bali iwe endelee hadi misimu ijayo ya korosho.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred ameishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwa jitihada  zao ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku ya pembejeo kwa asilimia 100 na kumepelekea ongezeko la uzalishaji huo mkubwa lakini pia uboreshaji wa masoko ya bidhaa za kilimo, matumizi ya kuuza korosho kwa kutumia mfumo wa kidijitali (TMX) kwani imesaidia kuongeza ufanishi na ushindani katika biashara ya korosho.

Aidha katika msimu huo wa kilimo mwaka 2024/2025 bei ya korosho ghafi katika mnada wa kwanza uliyoanza rasmi Oktoba 11, 2024 bei ya juu ilikuwa Sh 4,120 na bei ya chini Sh 4,035 chini ya Chama kikuu cha Ushirika kinachosimamia wilaya ya Tandahimba na Newala (TANECU Ltd) mkoani Mtwara uliyofanyika katika Halmashauri ya mji Newala.

The post Wanawake wasifu fursa za korosho Mtwara first appeared on HabariLeo.