Wananchi wakumbushwa kuhusu matumizi sahihi ya alama za taifa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam Wito umeitolewa kwa wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya alama za taifa, ikiwemo Ngao ama Nembo ya Taifa, Bendera ya Taifa, na Wimbo wa Taifa, huku wakihimizwa kuendelea kujifunza kuhusu matumizi sahihi ya alama hizo pamoja na matumizi ya Gazeti la Serikali. Hayo yamesemwa mapema Machi 20, 2025 na Mpiga […]
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wito umeitolewa kwa wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya alama za taifa, ikiwemo Ngao ama Nembo ya Taifa, Bendera ya Taifa, na Wimbo wa Taifa, huku wakihimizwa kuendelea kujifunza kuhusu matumizi sahihi ya alama hizo pamoja na matumizi ya Gazeti la Serikali.
Hayo yamesemwa mapema Machi 20, 2025 na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, George Lugome kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, alipokuwa akizungumza na chombo kimoja cha habari jijini Dar es Salaam.
Lugome alisema kuwa hivi karibuni kumekuwa na upotoshwaji wa alama za taifa na akakumbusha kuwa alama hizi zipo kwa mujibu wa sheria. Alisisitiza kuwa “Yeyote atakayezichezea alama hizi atapata adhabu kwa mujibu wa sheria. Adhabu yake inaweza kuwa kifungo cha miaka miwili jela, faini, ama vyote viwili kwa pamoja. Sheria hii ya mwaka 1964 iko kwenye mchakato wa kubadilishwa,” alisema.
Akizungumzia kuhusu Nembo ya Taifa, Lugome alisema kuwa nembo hiyo ni kwa matumizi ya shughuli za Serikali pekee, na sheria inasema wazi kuhusu hili. Aliongeza kuwa matumizi ya alama za taifa kwa namna isiyo sahihi yanaharibu haiba ya taifa, na Idara ya Mpiga Chapa ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa alama hizi zinatumika kwa usahihi.
Aidha, alifafanua kuwa uchapishaji holela wa alama hizi na uchoraji wa nembo kwa kubuni, unachangia upotoshwaji na kuharibu uhalisia wake.
Kwa upande wa Bendera ya Taifa, Lugome alizungumzia rangi nne za bendera ya taifa zinazotumika na kutoa ufafanuzi wa umuhimu wake.
Akielezea kuhusu Wimbo wa Taifa, Bw. Lugome alisema kuwa wimbo huu unapaswa kuimbwa kwa beti zote mbili na kufuata ala zilizowekwa, huku wananchi wakiwa wamesimama kwa heshima, ili kuonyesha utamaduni na uzalendo kwa taifa hili.
Kuhusu Gazeti la Serikali, alisema kuwa ni jarida linaloratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, na kuhaririwa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Gazeti hili linachapishwa mara moja kwa wiki na linajikita kutoa taarifa muhimu za Serikali, hasa kuhusu utendaji wa Serikali na taarifa binafsi.
Amesisitiza kuwa gazeti hili lipo kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma, kanuni C27-30.