Wanafunzi waguswa na msaada wa kisheria Bukombe

Habari Leo
Published: Feb 05, 2025 12:36:40 EAT   |  Educational

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Ushirombo iliyopo wilayani Bukombe mkoa wa Geita wameeleza kuguswa na Kampeni ya Msaada…

The post Wanafunzi waguswa na msaada wa kisheria Bukombe appeared first on HabariLeo.

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Ushirombo iliyopo wilayani Bukombe mkoa wa Geita wameeleza kuguswa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) kwani imewaongezea uelewa wa kujikinga dhidi ya ukatili.

Wanafunzi hao wametoa maoni yao mara baada ya timu ya MSLAC kutembelea shuleni hapo  na kupewa elimu juu ya aina za ukatili, hatua za kuchukua, maeneo ya kuripoti ukatili na njia za kujikinga dhidi ya ukatili.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari Ushirombo, Petronia Clement amesema kampeni hiyo imewasaidia kujitambua na kuelewa haki za msingi za watoto na watu wazima.

“Pia imesaidia kutuelimisha na masuala ya ukatili wa kijinsia, kwa mfano mwanafunzi amefanyiwa ukatili wa kijinsia, wametuelekeza sehemu ya kwenda kutoa taarifa, na kupata haki zetu.

“Tunamshukuru mama Samia kwa sababu ametufungua kwa sababu kuna ndugu zetu wengi ambao wamepata changamoto lakini ujio wao wametusaidia kwa kiasi kikubwa”, amesema.

Mwanafunzi wa kidato cha tano Esther Suleman amesema elimu ya sheria mashuleni imewafungua wanafunzi na kuwapa mwanga juu ya taasisi za kisheria na taratibu za kufuata kupata haki zao.

“Wanasheria hawa kwa kweli wametufungua vitu vingi sana, maana ukiangalia watoto wengi, walikuwa wanapoteza haki zao, wengine walikuwa wanapata magonjwa ya zinaa, kupitia ukatili wa kijinsia”, amesema.

Kwa upande wake Naomi Charles amekiri kampeni ya MSLAC imeondoa ombwe la sheria na kuwafanya wanafunzi kuwa mabalozi wa kupunguza vitendo vya ukatili katika jamii.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Ushirombo, Alex Joseph amesema shule yake ina wanafunzi 2,100 kati yao wavulana ni 960 na wasichana ni 1,140 ambapo msaada wa kisheria utawafanya wawe salama dhidi ya ukatili wa kingono.

Amesema elimu ya sheria kwa wanafunzi imewapunguzia mzigo walimu na wazazi juu ya changamoto za watoto kukutana na madhira ya ukatili wa kijinsia na hivo itasaidia kuwafanya wawe salama ndani na nje ya shule.

The post Wanafunzi waguswa na msaada wa kisheria Bukombe appeared first on HabariLeo.