Wanafunzi nje ya mfumo rasmi waongezeka Geita

Habari Leo
Published: May 12, 2025 14:20:06 EAT   |  Educational

GEITA: IDADI ya wanafunzi wanaosoma Elimu ya Sekondari Nje ya Mfumo Rasmi (ASEP) katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita imeongezeka kutoka wanafunzi 105 mwaka 2021 hadi kufikia 176 Aprili mwaka 2025. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la wanafunzi 71 wa Elimu ya Sekondari Nje ya Mfumo Rasmi ndani ya kipindi cha miaka minne sawa …

GEITA: IDADI ya wanafunzi wanaosoma Elimu ya Sekondari Nje ya Mfumo Rasmi (ASEP) katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita imeongezeka kutoka wanafunzi 105 mwaka 2021 hadi kufikia 176 Aprili mwaka 2025.

Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la wanafunzi 71 wa Elimu ya Sekondari Nje ya Mfumo Rasmi ndani ya kipindi cha miaka minne sawa na ongezeko la asilimia 67.

Ofisa  Elimu Sekondari Manispaa ya Geita, Rashid Juma alieleza hayo katika hafla ya kutathmini maendeleo ya elimu sekondari tangu Novemba 2021 hadi kufikia Aprili, 2025.

Amesema mbali na wanafunzi waliopo nje ya mfumo rasmi, wanafunzi wa sekondari kwa shule za serikali wameongezeka kutoka 17,145 mwaka 2021 hadi kufikia wanafunzi 22,362 kwa takwimu za Aprili 2025.

Amesema wanafunzi wanaosajiliwa kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kutoka asilimia 74.7 ya wanafunzi waliochaguliwa mwaka 2021 na kufikia asilimia 92 ya wanafunzi waliochaguliwa mwaka 2025.

Amebainisha wanafunzi 4,137 mwaka 2021 walisajiliwa kati ya wanafunzi 5,535 waliochaguliwa huku wanafunzi 6,296 walisajiliwa mwaka 2025 kati ya wanafunzi 6,806 waliochaguliwa mwaka 2025.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Yefred Muyenzi amesema katika kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wametenga kiasi cha sh milioni 175 kutengeneza madawati takribani 4,000.

Muyenzi amekiri baadhi ya shule ndani ya manispaa ya Geita zina idadi kubwa ya wanafunzi zaidi ya miundombinu iliyopo akitaja baadhi ya shule za maeneo ya mjini zina takribani wanafunzi 3,000.

“Tuna kazi kubwa ya kuongeza vyumba vya madarasa, kuongeza matundu ya vyoo, kujenga nyumba za walimu na miundombinu mingine ili mafanikio yaliyokwisha kupatikana kwenye ufaulu yaendelee”, amesema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyakato-Geita, Mwalimu Severian Robnson amesema hatua ya manispaa kutoazawadi kwa shule zilizofanya vizuri inatoa motisha kwa wanafunzi na walimu kunua taaluma.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Merry Queen of Peace, Jenifer Nicolous ameiomba jamii na serikali kuchukua hatua za ziada kudhibiti wimbi la watoto kuacha shule na kujiingiza kwenye biashara mitaani.