Wanafunzi Chuo Kikuu Ardhi kupikwa zaidi kukabili soko la ajira

Mtanzania
Published: Jan 16, 2025 18:32:39 EAT   |  Business

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Katika jitihada za kujenga nguvu kazi yenye ushindani na ubunifu wanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU) sasa wataongezewa ujuzi na maarifa ili kukabiliana na changamoto za soko la ajira. Hatua hiyo inafuatia baada ya chuo hicho kuingia makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Ushauri na Usimamizi ya Empower Limited yenye […]

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Katika jitihada za kujenga nguvu kazi yenye ushindani na ubunifu wanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU) sasa wataongezewa ujuzi na maarifa ili kukabiliana na changamoto za soko la ajira.

Hatua hiyo inafuatia baada ya chuo hicho kuingia makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Ushauri na Usimamizi ya Empower Limited yenye lengo la kuwawezesha wanafunzi kwa ujuzi wa vitendo.

Akizungumza leo Januari 16,2025 wakati wa kusaini makubaliano hayo Mkuu wa Empower Limited, Joshua Naiman, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kubadilisha nguvu kazi ya Tanzania.

“Kama kinara katika usanifu, mipango miji na uendelevu wa mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi kinaleta mtazamo wa kipekee kwenye mtandao wa Generation Empower. Dhamira ya ARU ya kutoa elimu jumuishi inalingana kikamilifu na lengo la Empower Limited la kukuza wahitimu wenye uwezo wa kushughulikia changamoto halisi za maisha,” amesema Naiman.

Amesema programu hiyo inajumuisha warsha kuhusu ujuzi wa ajira ulioandaliwa kulingana na mahitaji ya sekta, semina na mijadala ya vikundi na wataalam wa sekta mbalimbali, changamoto na uwezo wa kuzitatua, fursa za mitandao na wadau muhimu katika sekta binafsi na umma.

Amesema wanatarajia kwa miaka mitano ijayo (2024 – 2029) programu hiyo katika chuo hicho itafikia zaidi ya wanafunzi 2,000 ambapo watahakikisha kila mshiriki anapata mafunzo bora bila gharama yoyote.

Kulingana na mkuu huyo, mpaka sasa zaidi ya wanafunzi 7,000 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) wamenufaika kupitia programu hiyo.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Profesa Evaristo Liwa, amesema kupitia ushirikiano huo wanafunzi watapata fursa za ushauri, mafunzo maalumu na msaada wa kazi wa kipekee.

“Tumejikita kutoa elimu bora na kukuza maendeleo ya kina kwa wanafunzi, tunatambua elimu lazima izidi darasani na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa ya vitendo, maendeleo ya kibinafsi na uzoefu wa maisha halisi ambao utawaandaa kuwa viongozi na wabunifu,” amesema Profesa Liwa.

Amewataka wanafunzi wa chuo hicho kuchangamkia fursa hiyo na kutumia kikamilifu rasilimali na utaalamu ambao programu hiyo inaleta chuoni hapo.

Mmoja wa wanafunzi watakaonufaika na programu hiyo, Jemina Obedi, amesema wameipokea vema programu hiyo na wanatarajia itakwenda kuleta matokeo chanya.