Wabunge wahimiza uandaaji wa sera jumuishi za akili mnemba

DODOMA: WABUNGE wanawake wametoa wito kwa serikali kuharakisha mchakato wa uandaaji na utekelezaji wa sera jumuishi na zenye kuzingatia usawa wa kijinsia kuhusu matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) katika sekta mbalimbali muhimu za taifa, huku wakisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanawake katika uundaji wa sera na sheria za teknolojia hiyo bunifu. Wito huo umetolewa …
DODOMA: WABUNGE wanawake wametoa wito kwa serikali kuharakisha mchakato wa uandaaji na utekelezaji wa sera jumuishi na zenye kuzingatia usawa wa kijinsia kuhusu matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) katika sekta mbalimbali muhimu za taifa, huku wakisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanawake katika uundaji wa sera na sheria za teknolojia hiyo bunifu.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma mwishoni mwa wiki wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake viongozi kuhusu teknolojia ya AI, ikiwa ni sehemu ya mpango wa FemAI Leaders for Africa unaolenga kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika usimamizi na matumizi ya teknolojia hiyo kwa maendeleo ya jamii.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Shirika la OMUKA Hub kwa ushirikiano na Taasisi ya Women Political Leaders (WPL) na kufadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) kupitia Kituo cha Mabadiliko ya Kidijitali Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Fatma Toufiq alisema AI inazidi kuwa muhimu katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, kilimo na mazingira, lakini bado hakuna sera wala sheria zinazoliongoza jambo hilo nchini.
“Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linajivunia kuwa sehemu ya juhudi hizi za kuelewa na kutumia teknolojia ya AI kwa manufaa ya Watanzania. Tunapaswa kuwa na mfumo wa kisheria utakaolinda makundi yaliyo hatarini, hususan wanawake ambao mara nyingi huathirika zaidi na changamoto za kidijitali,” alisema Toufiq.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) na Mwanzilishi wa OMUKA Hub, Neema Lugangira alisema AI ni nyenzo yenye uwezo mkubwa wa kusaidia wabunge na viongozi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, lakini hilo haliwezi kufikiwa iwapo hakutakuwepo sera ya taifa inayosimamia teknolojia hiyo.
“Akili Mnemba inaweza kutusaidia kukusanya na kuchambua taarifa kwa haraka, lakini bila sera ya taifa, hatutafaidika ipasavyo na fursa hii ya teknolojia,” alisema.
Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu alisema dunia inabadilika kwa kasi kupitia teknolojia ya AI na Tanzania haiwezi kubaki nyuma huku mataifa mengine yakipiga hatua.
“Tukichelewa kujiandaa na AI, tutabaki nyuma kama kisiwa katika maendeleo ya kidijitali. Tunapaswa kuwa tayari kwa mabadiliko haya kwa kujifunza na kujiimarisha,” alisema.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dkt Jabhera Matogoro alisema ili Tanzania inufaike na teknolojia hiyo, ni lazima kuwa na sera ya kitaifa ya AI inayozingatia mazingira ya ndani.
“Sera hiyo inapaswa kueleza misingi ya maadili, kuainisha vipaumbele vya kitaifa na kutambua miradi ya kimkakati. Hii ni pamoja na kujifunza kutoka kwa nchi kama Mauritius, Afrika Kusini, Ghana, Rwanda, Kenya, Senegal na Nigeria ambazo zimeanza kutumia au kuandaa sera zao,” alisema Matogoro.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Mabadiliko ya Kidijitali cha GIZ Tanzania, Julia Schappert alisema ushiriki wao katika semina hiyo una lengo la kuhakikisha teknolojia ya AI inatumika kwa manufaa ya jamii za Kiafrika na kuimarisha nafasi ya Afrika katika uongozi wa ubunifu wa kiteknolojia duniani.
Kupitia tamko la pamoja, wabunge wanawake waliitaka serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, sekta binafsi, vyombo vya habari, na taasisi za elimu kuanzisha jukwaa la Female AI Leaders Lab litakalowezesha kuelimisha umma kuhusu matumizi ya AI.
Walisema jukwaa hilo litawezesha uanzishaji wa kampeni za elimu kwa umma, mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu matumizi ya AI kwa maadili, pamoja na kuandaa kozi fupi kwa wabunge na viongozi wa mitaa chini ya kaulimbiu “AI kwa Utawala na Sera.”
Wabunge hao pia walipendekeza kuanzishwa kwa jukwaa la kitaifa la kuwawezesha wanawake viongozi kueneza sera ya Taifa ya AI 2025 hadi ngazi ya majimbo na vijiji kwa kushirikisha mabalozi wa AI Jamii.
Aidha, walisisitiza umuhimu wa kuwa na sera, sheria na kanuni madhubuti zitakazolinda faragha na usalama wa watumiaji wa teknolojia hiyo ili kuhakikisha haki za watu wote, hususan wanawake, zinazingatiwa na kulindwa.