Upekee wa vivutio lukuki Hifadhi ya Lukwika Lumesule

LINDI; Lukwika Lumesule ni moja ya hifadhi za kipekee Tanzania lakini zisizotembelewa na watalii wengi. Naweza kusema ni hifadhi zisizo na umaarufu mkubwa kulinganisha na vivutio vya kipekee vilivyomo ndani yake. Hifadhi hiyo iliyojificha Kusini mwa Tanzania (Kusini Magharibi na Magharibi mwa Wilaya ya Masasi) katika Mkoa wa Lindi, kijiografia inapakana na Hifadhi ya Niassa …
LINDI; Lukwika Lumesule ni moja ya hifadhi za kipekee Tanzania lakini zisizotembelewa na watalii wengi. Naweza kusema ni hifadhi zisizo na umaarufu mkubwa kulinganisha na vivutio vya kipekee vilivyomo ndani yake.
Hifadhi hiyo iliyojificha Kusini mwa Tanzania (Kusini Magharibi na Magharibi mwa Wilaya ya Masasi) katika Mkoa wa Lindi, kijiografia inapakana na Hifadhi ya Niassa nchini Msumbiji zikiwa zimetenganishwa na Mto Ruvuma.
Kwa jiografia hiyo, wanyama wengi wamekuwa wakivuka kwenda Msumbiji na kurudi.
Kwa mujibu wa Tovuti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ndiyo inasimamia hifadhi hiyo, miongoni mwa wanyamapori wanaohama kupitia Ushoroba wa Wanyamapori wa Selous-Niassa ni tembo, nyati, pundamilia na nyumbu.
Tovuti hiyo inaeleza kuwa Hifadhi ya Lukwika Lumesule iliteuliwa kuwa Pori la Akiba Novemba 20, 1995 kupitia Tangazo la Serikali Na 7 la 1996 na ina ukubwa wa kilometa za mraba 444.2.
Mtandao wa exploretanzaniatours.com unataja vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika hifadhi hiyo ambavyo watalii wanaweza kutembelea na kufurahia uzuri wake.
Wanyamapori
Lukwika Lumesule ni hifadhi yenye aina mbalimbali za wanyama wakubwa na wadogo.
Watalii wanapotembelea wanaweza kuona wanyama maarufu kama chui, simba, tembo, kiboko, mamba, swala, kudu na nyati.
Pia, kuna pundamilia na nyumbu sambamba na chatu, kobe, aina mbalimbali za nyoka na mijusi.
Ndege
Kutokana na uwepo wa vijito na mito katika hifadhi hiyo, ndege wa aina mbalimbali wamekuwa wakivutiwa na kuweka makazi katika maeneo ya mito hiyo.
Inaelezwa kuwa, kuna zaidi ya aina 300 za ndege katika hifadhi hiyo wakiwemo korongo weupe, kware, njiwa, bata bukini, bundi na tai.
Mimea
Mandhari nzuri ya Lukwika Lumesule inachangiwa na uoto mzuri wa asili na aina mbalimbali za mimea iliyoota juu ya ardhi yenye rutuba kukiwa na aina tofauti za udongo kwenye maeneo ya hifadhi hiyo zinazoruhusu ukuaji wa misitu ya aina mbalimbali za miombo na nyasi zenye mchanganyiko wa miti.
Mito
Hifadhi hii ina mchanganyiko wa mito midogo na mikubwa inayotiririka ndani ya hifadhi ukiwemo Mto Lumesule unaotiririka kutoka Magharibi kwenda Kusini na Mto Lukwamba unaogawa hifadhi hiyo katika sehemu mbili.
Mito hii ni muhimu kwa bayoanuai katika hifadhi hiyo kwa kuwa ni vyanzo vya maji kwa wanyamapori lakini pia inasaidia jamii zinazozunguka hifadhi kwa kusambaza maji kwa wakazi wa vijiji vya Mburusa, Chimika, Mpwahia, Lukwika na Masuguru.
Chanzo kinasema mbali na utalii wa wanyama wakubwa katika makazi yao ya asili, kuna utalii wa kihistoria, mito ya kuvutia, miamba na maporomoko ya maji.
Safari za kutembea
Shughuli nyingine ya utalii inayoweza kufanyika katika hifadhi hiyo ni kutembea hifadhini na kujionea mandhari nzuri na kujionea wanyamapori kwa ukaribu shughuli inayofanywa chini ya uangalizi wa mwongoza watalii mwenye silaha.
Kuangalia ndege
Kwa wapenda ndege, Lukwika Lumesule ni mahali sahihi kabisa kwa utalii wa kutazama ndege.
Kama ilivyobainishwa awali, hifadhi hiyo ina zaidi ya aina 300 za ndege, hivyo wanaweza kutembelea huko na kusikia milio ya kuvutia ya ndege hao.
Ndege wanaoweza kuonekana katika hifadhi hiyo ni pamoja na bundi, kware, njiwa, bata bukini, tai na wengine wengi.
Utalii wa kambi
Mandhari ya Lukwika Lumesule ni maeneo ya kuvutia, hutoa fursa kwa watalii kufanya utalii wa kambi kwa kuweka kambi kwenye maeneo maalumu yaliyowekwa kwa utalii wa aina hiyo na kuwezesha watalii kufurahia na kutuliza akili kutokana na mazingira tulivu yanayopatikana katika hifadhi hiyo.
Ndani ya hifadhi hiyo kuna kambi maarufu ya utalii iliyojengwa kwa ajili ya wageni wanaotembelea hifadhi.
Kambi hiyo iko pembezoni mwa Mto Ruvuma ikiwa na huduma muhimu kama choo, jiko na sehemu ya kula chakula.
Eneo hilo ni tulivu na wageni hupata fursa ya kuona wanyama na ndege wa aina mbalimbali.
Utalii wa fukwe
Utalii wa ufukweni ni shughuli nyingine ya kufurahisha katika utalii wa Lukwika Lumesule.
Shughuli hii inawapa wageni fursa ya kutembelea fukwe za mchanga na miamba kando ya Mto Ruvuma na kuwapa uzoefu wa kipekee wa utalii wa fukwe.
Katika utalii huo, wageni wanaweza kupumzika kando ya mto, wakifurahia mazingira tulivu huku wakishiriki katika shughuli mbalimbali kama uvuvi na matembezi.
Mapango ya Habiba
Ofisa Utalii wa Tawa, Sosteness Kweka anasema mapango hayo yamo ndani ya hifadhi hiyo na yamebeba historia ya kipekee ya mwanamke aliyeitwa, Habiba aliyewahi kujificha kwenye mapango hayo akimkimbia mume wake.
“Kuna historia iliyokuwa imeandikwa kuhusiana na mapango ya Lukwika Lumesule.
Historia ile ilikuwa inaeleza juu ya wanandoa wawili ambo ni Habiba na mumewe waliokuwa wanaishi katika Kijiji cha Mpombe karibu na Hifadhi ya Lukwika Lumesule,” anasema Kweka.
Anasema historia inaeleza, Habiba alishikwa ugoni (alifumaniwa) na mumewe.
Kitendo hicho kilimfanya, Habiba kuogopa kudhuriwa na mumewe. Akaamua kukimbilia katika Hifadhi ya Lukwika Lumesule iliyopo jirani na kujificha katika mapango yaliyopo ndani ya hifadhi na yaliyokuwa yanasifika kuwa na wanyama wakali.
Anasema, Habiba alikaa katika mapango hayo kwa siku saba huku wanakijiji wakimtafuta baada ya mumewe kutoa taarifa ya kupotea kwake.
“Wanakijiji walianza kumtafuta, Habiba na kufanikiwa kumkuta katika mapango hayo, ujasiri ambao aliuonesha, Habiba wa kukaa ndani ya mapango hayo kwa muda wa siku saba, mumewe baada ya kumkuta hapo alimsamehe kwa ujasiri aliounesha na kuamua kurudi nyumbani kuendelea na maisha ya ndoa,” anasema Kweka.
Anaongeza: “Tangu hapo mapango hayo yaliitwa, Habiba na wageni wengi wanatembelea hapo kuomba amani ya ndoa na msamaha kama ambavyo, Habiba alipata amani ya ndoa yake na mumewe.”
Anaendelea kusema kuwa mapango hayo yana historia nyingne kwani yalitumiwa kama maficho ya askari wakati wa mapigano ya Frelimo nchini Msumbiji.
Daraja la Umoja
“Hiki ni kivutio kingine cha utalii ambacho hupatikana kilometa 10 kutoka Hifadhi ya Lukwika Lumesule,” anasema Kweka.
Anasema Daraja la Umoja ni daraja lililojegwa kwa ushirikiano wa Tanzania na Msumbiji na limekuwa kivutio kikubwa kwa kuunganisha nchi hizo mbili sambamba na ujenzi wake wenye muundo wa pembe za ndovu zinazowakilisha makundi makubwa ya tembo yaliyokuwa yanavuka kutoka Msumbiji kuja Tanzania.
Daraja hili lina urefu wa takribani meta 720 na upana meta 13
Fursa
Akizungumzia fursa za uwekezaji zilizopo Lukwika Lumesule, Kweka anasema hifadhi hiyo kwa sasa ina mwekezaji ambaye dhamira yake ni kuanzisha shughuli za uwindaji wa kitalii.
Anasema, katika kipindi hiki ambacho mwekezaji huyo anaendelea na hatua za uwekezaji, shughuli za utalii wa picha zinaweza kuendelea kufanyika kwa utaratibu maalumu baina ya mwekezaji na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).