Ulega atoa maagizo ujenzi barabara Kigamboni
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amefanya ziara katika wilaya ya Kigamboni kujionea maendeleo ya miradi ya ujenzi wa…
The post Ulega atoa maagizo ujenzi barabara Kigamboni appeared first on HabariLeo.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amefanya ziara katika wilaya ya Kigamboni kujionea maendeleo ya miradi ya ujenzi wa barabara na kutoa maelekezo kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni ya Nyakemore Engineering Group kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati na ubora wa hali ya juu.
Akiwa katika eneo la Kigamboni Mnadani, Waziri Ulega ameeleza kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo ni lazima marekebisho yake yakamilike haraka.
Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha barabara haifungwi kabisa wakati wa ujenzi ili kuepusha athari kwa shughuli za kijamii, na kwa wananchi wanaokwenda kufuata huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya, masoko, ofisi za umma.
“Ni lazima barabara iwe inapitika hata wakati wa ujenzi ili wananchi waendelee kupata huduma muhimu. Tunataka kazi hii ikamilike ifikapo Januari 30, 2025, na nitakuja kukagua na kuifungua rasmi. Mkandarasi anapaswa kufanya kazi usiku na mchana, kuongeza wataalamu, vibarua, na vifaa ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na na changamoto ya msongamano inatatuliwa haraka,” alisema Ulega.
Aidha, Waziri Ulega ameagiza kuwekwa utaratibu wa kudhibiti kasi ya malori yanayopita katika barabara ya Kigamboni, ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Pia amesisitiza umuhimu wa kujenga vituo vya mabasi kandokando ya barabara hiyo ili kuimarisha usafiri kwa wananchi.
Waziri Ulega amemtaka mkandarasi kutumia njia za ubunifu ili kuondoa msongamano wa magari katika eneo la Kigamboni Mnadani na maeneo mengine na kuhakikisha shughuli za ujenzi haziathiri ratiba za kila siku za wakazi wa eneo hilo.
The post Ulega atoa maagizo ujenzi barabara Kigamboni appeared first on HabariLeo.