‘Uchumi Tanzania unainuka kwa kasi kupitia Muungano’

Habari Leo
Published: May 13, 2025 07:49:09 EAT   |  News

“NAOMBA niwe mkweli, Zanzibar tuna madaktari 134 na kati yao, madaktari bingwa ni wanne tu. Hali hii inalazimu wagonjwa wetu kusafiri kwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH-Upanga) na Mloganzila kwa ajili ya matibabu.” “Serikali inalipa zaidi ya Shilingi bilioni 400 kugharamia huduma hizo na haya yote yanatokana na …

“NAOMBA niwe mkweli, Zanzibar tuna madaktari 134 na kati yao, madaktari bingwa ni wanne tu. Hali hii inalazimu wagonjwa wetu kusafiri kwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH-Upanga) na Mloganzila kwa ajili ya matibabu.”

“Serikali inalipa zaidi ya Shilingi bilioni 400 kugharamia huduma hizo na haya yote yanatokana na ushirikiano mzuri wa serikali hizi mbili.”

Anasema Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam kuhusu Wiki ya Afya Zanzibar yaliyofanyika Mei 4 hadi 10 mwaka huu Pemba na Unguja.

Mazrui anasema hayo ni matunda ya Muungano unaosimamiwa vema na viongozi wa pande zote mbili yaani Rais Samia Suluhu Hassan (Rais wa Jamhuri ya Muungano na Dk Hussein Mwinyi (Rais wa Zanzibar) kwa kuweka mbele maslahi ya wanachi.

Anasema kupitia sekta ya afya, kila mwezi takribani wagonjwa 200 kutoka Zanzibar husafiri kwenda Tanzania Bara kupata huduma za kibingwa. Anasema serikali na wananchi hutumia zaidi ya Sh milioni 400 kila mwezi kugharamia matibabu hayo hapa nchini na kuepusha usumbufu wa kutafuta matibabu nje ya nchi.

Mazrui anasema Muungano umesaidia pia kukuza utalii tiba kwani zaidi ya watalii 200 hufika Zanzibar kila mwezi kwa huduma za kujifukiza (kupigwa nyungu). Utalii unaingiza fedha nyingi na kukuza pato la taifa sambamba na kuongeza ajira kwa vijana. Kwa mujibu wa waziri huyo, juhudi zinazofanywa na serikali kuinua sekta ya utalii kwa Tanzania Bara zimekuwa na athari kubwa chanya kwa Zanzibar.

Anasema hii ni kwa kuwa watalii wanaotembelea Bara wamekuwa pia wakitembelea visiwani Zanzibar na kusababisha ongezeko la idadi ya watalii visiwani.

“Pato letu na wenzetu wa Bara hutokana na utalii. Watalii wanaokuja Serengeti au Ngorongoro huvutiwa, hufika Zanzibar na hatimaye huchochea uwekezaji na uboreshaji wa miundombinu ya afya, mazingira ya kazi na ustawi wa wafanyakazi ikiwa ni pamoja na sehemu za mapumziko,” anasema Mazrui.

Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2023, sekta ya kilimo ilichangia zaidi ya asilimia 25 ya Pato la Taifa na kutoa zaidi ya asilimia 65 ya ajira nchini na hivyo, kupunguza utegemezi kwa vijana. Taarifa hiyo inasema Muungano umeimarisha sera za kilimo kupitia miradi kama ‘Building a Better Tomorrow’ (BBT) inayowalenga vijana na wanawake.

Miradi hiyo imepanua maeneo ya uzalishaji, kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara katika masoko, usambazaji wa pembejeo na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Aidha, Sera ya Uratibu wa  masuala ya Muungano ya Mwaka 2006 kwa kushirikisha Sera ya Kilimo ya Zanzibar (ZASP) pamoja na Mpango wa Sekta ya Kilimo (ASDP Zanzibar), vimesaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara kama karafuu, viungo, nazi na mwani visiwani humo.

“Zanzibar haina ardhi kubwa kama Bara, lakini imefanikiwa katika kilimo cha viungo, mboga na matunda.  Programu kama ZEEF (Zanzibar Economic Empowerment Fund) zimewasaidia wakulima wadogo,” inaeleza sera hiyo. Aidha, inafafanua zaidi kuwa viwanda vidogo vya usindikaji wa samaki, sabuni, mafuta ya nazi na kazi za ufundi sasa vimeongezeka visiwani humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar Investment Promotion Authority (ZIPA), Saleh Saad Mohamed anasema kupitia ushirikiano wa Muungano, Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa ushirikiano baina ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na ZIPA.

“Mwaka 2023, Tanzania ilipokea uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje wa Dola bilioni 3.5. Miradi mingi ilihusisha miundombinu, utalii, viwanda na teknolojia, na Zanzibar ilinufaika kwa kupokea sehemu ya uwekezaji huo,” anasema Mohamed.

Anasema dira ya maendeleo ya Dk Mwinyi inalenga maendeleo jumuishi na ustawi wa kiuchumi kupitia uchumi wa bluu, kilimo, nishati mbadala na utalii kukuza zaidi uchumi wa Zanzibar. “Tanzania Bara imewekeza kwenye miundombinu ya kisasa kama reli ya kisasa (SGR), barabara, madaraja, bandari na mradi mkubwa wa
umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).”

“Mradi huu utaboresha upatikanaji wa nishati na kuchochea uzalishaji viwandani kwa pande zote za Muungano,” anaongeza Mohamed. Kwa upande wake, Profesa Omary Mbura wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema sekta ya utalii ni moja ya faida kubwa za Muungano kwa sababu watalii wengi huja nchini wakivutiwa na vivutio vya kipekee na kutumia fedha za kigeni.

“Hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Nje ilitumia mabalozi kutangaza vivutio vyetu. Vivutio vya Bara kama Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro na Ruaha na vile vya Zanzibar ambavyo ni fukwe na historia ya Mji Mkongwe na vyote vimepata soko kupitia Muungano,” anasema Profesa Mbura.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) na mtaalamu wa uchumi,
Dk Isaac Safari anasema ushirikiano wa kiuchumi kati ya pande mbili umeimarisha biashara kupitia bandari kama Malindi.

“Zanzibar hufaidika na soko la Bara kwa kuuza bidhaa kama samaki, viungo, nazi na mazao ya baharini.” “Mfumo huu huruhusu biashara ya ndani bila ushuru wa forodha, kutokana na sera bora za Muungano,” anasema Dk Safari.