Tunahuzunika pamoja!

ZANZIBAR: Tulifurahi pamoja. Tunazunika pamoja! Pengine ndivyo unavyoweza kuzungumzia matokeo ya mchezo wa marudiano fainali Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na RS Berkane ya Morocco uliofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar Mei 25, 2025. NOVEMBA 13, 1993 maelfu ya mashabiki wa Simba walijitokeza Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Dar es Salaam kushuhudia …
ZANZIBAR: Tulifurahi pamoja. Tunazunika pamoja! Pengine ndivyo unavyoweza kuzungumzia matokeo ya mchezo wa marudiano fainali Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na RS Berkane ya Morocco uliofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar Mei 25, 2025.
NOVEMBA 13, 1993 maelfu ya mashabiki wa Simba walijitokeza Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Dar es Salaam kushuhudia mchezo wa marudiano fainali ya Kombe la CAF kati ya Simba na Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Mashabiki hao walijawa na imani kubwa kwamba Simba ingeandika historia kuwa bingwa wa michuano hiyo na hasa kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza uliofanyika Ivory Coast, ambao timu hizo zilitoka 0-0.
Lakini mashabiki wa mpira na Watanzania kwa ujumla wakiongozwa na mgeni rasmi Rais wa Tanzania wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, walishuhudia Simba ikifungwa mabao 2-0, hivyo ndoto za ubingwa zikapotea.
Tukio hilo bado lipo nyoyoni mwa mashabiki wa mpira, lakini huku kukiwa na kauli mbiu ya: ‘Hii Tunabeba’, Simba jana ilishuka Uwanja wa New Amaan Complex kucheza mchezo wa marudiano fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Mchezo wa kwanza uliofanyika Morocco Simba ilifungwa mabao 2-0, hivyo ilikuwa ikihitajika ishinde mabao 3-0.
Wakicheza mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, ambaye ni mtoto wa hayati Mzee Mwinyi Rais aliyeshuhudia maumivu ya fainali mwaka 1993, vijana wa Msimbazi jana pia walishindwa kung’ara na kutoka sare ya bao 1-1.
Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17 mfungaji akiwa Joshua Mutale, kabla ya Berkane kusawazisha dakika ya 90+3 mfungaji akiwa Soumaila Sidibe.
Kutokana na matokeo hayo Berkane imeibuka bingwa kufuatia ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata katika mchezo wake wa kwanza wiki iliyopita nchini Morocco.