TTB, Turkish Airlines kutangaza utalii

Habari Leo
Published: Jan 08, 2025 09:36:37 EAT   |  Travel

BODI ya Utalii Tanzania(TTB) imeingia makubaliano ya miaka mitatu na Shirika la Ndege la Uturuki ‘Turkish Airlines ‘…

The post TTB, Turkish Airlines kutangaza utalii appeared first on HabariLeo.

BODI ya Utalii Tanzania(TTB) imeingia makubaliano ya miaka mitatu na Shirika la Ndege la Uturuki ‘Turkish Airlines ‘ kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kwenye ndege na tovuti zao zote duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Ephraim Mafuru amesema wamechagua Shirika hilo kwa kuwa huduma yao ni pana wana zaidi ya ndege 490 na wanaenda miji zaidi ya 411 kati ya hiyo, 61 ni miji ya Afrika.

Amesema maeneo waliyokubaliana ni kutoa matangazo ya vivutio vya utalii katika ndege zao zote, tovuti zao na ofisi zao. Pia, kutakuwa na punguzo la nauli kwa watu watakaosafiri kwa ajili ya kutalii.

“Matarajio yetu ni kuongeza idadi ya watalii kuja kutembelea vivutio mbalimbali nchini lakini pia, waongezeke wawekezaji waje kwa wingi kuwekeza kwenye sekta za utalii nchini,”amesema.

Amesema mikakati yao ni kuendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali ya ndege na huo ni mwanzo wataingia na makampuni mengine lengo ni kujitangaza na kuvuta watalii na wawekezaji pande zote za dunia.

Mafuru amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, viongozi mbalimbali kwa kuwafungilia njia na kuwasimamia kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Turkish airlines Kadiri Karaman amesema kwa miaka 15 ya shirika la ndege la Uturuki nchini Tanzania wanathamini juhudi za Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan, katika kuweka mazingira salama ya biashara.

Pia, amesema wanaitambua TTB kama mshirika mkuu katika kuitangaza Tanzania kama kivutio kikuu akisema ushirikiano huo utasaidia kuimarisha lengo la pamoja la kuifungua Tanzania kwenye masoko ya utalii ya kimataifa, kukuza ukuaji na manufaa kwa pande zote.

“Katika Shirika la Ndege la Uturuki, kauli mbiu yetu ni “Panua Ulimwengu Wako.”Tunajivunia kushikilia Rekodi ya Dunia ya Guinness kwa kusafiri kwa ndege hadi nchi nyingi zaidi, hatua ambayo inasisitiza uwezo wetu wa kuunganisha watalii kutoka kila kona ya dunia hadi Tanzania,”amesema.

Ameongeza kuwa kuanzia Juni, wataongeza masafa ya ndege Kilimanjaro: kutoka safari nne hadi 14 kwa wiki, Zanzibar kutoka safari tisa hadi 14 kwa wiki.

“Tunawahimiza wadau kutumia Istanbul kama kitovu cha kuunganisha kupitia programu kama vile Touristanbul na *Stopover mjini Istanbul,*zinazoboresha uzoefu wa wasafiri wanapoelekea Tanzania, tuendelee kuimarisha ushirikiano wetu na kufungua fursa kamili ya sekta ya utalii ya Tanzania,”amesema.

Mwisho

The post TTB, Turkish Airlines kutangaza utalii appeared first on HabariLeo.