TIC yabainisha inavyotoa elimu ya uwekezaji

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinatoa elimu ya uwekezaji kwa watu mbalimbali wakiwamo mabalozi wanaokwenda kuwakilisha Tanzania nje ya nchi. Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani TIC, Felix John amesema hayo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kongamano kuhusu nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kufanikisha Dira …
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinatoa elimu ya uwekezaji kwa watu mbalimbali wakiwamo mabalozi wanaokwenda kuwakilisha Tanzania nje ya nchi.
Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani TIC, Felix John amesema hayo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kongamano kuhusu nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
“Mathalan mabalozi, kila teuzi zinapofanyika TIC imekuwa ikipewa nafasi ya takribani siku mbili kuwajengea uwezo ili wakaiwakilishe vema nchi yetu kuvutia wawekezaji kutoka nje na kusaidia Watanzania namna ya kutekeleza miradi ya ubia kwa ushirikiano na wawekezaji kutoka nje ya nchi,” alisema John.
Alisema ili kutoa huduma bora kwa wawekezaji ndani na nje ya nchi serikali kupitia TIC, imeanzisha kitengo cha huduma ya uwekezaji mahala pamoja ambayo kwa sasa ina takribani taasisi 15 zilizo kwenye mnyororo wa thamani ya sekta ya uchumi.
“Kupitia huko wawekezaji wanapata huduma bora na kwa urahisi na tumeleta ufanisi wa hali ya juu na kupunguza urasimu,” alisema John.
Alisema ili kutekeleza kwa ufanisi miradi ya uwekezaji serikali imetoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi lengo ni kupunguza gharama za mtaji wa utekelezaji mradi husika.
“Mfano kama kilimo ushuru wa forodha unapata msamaha wa kodi hadi asilimia 100, visivyo vya kikodi ni pamoja na ruhusa ya kuleta watalaamu wasiozidi 10 kwa ajili ya kutekeleza mradi, kunufaika na huduma za kituo cha uwekezaji mahali pamoja bila gharama yoyote,” alifafanua.
Alisema mafanikio ya kituo hicho ni makubwa kuhusu uwekezaji kwani mwaka 2022 miradi ya ubia kati ya Watanzania na wageni iliyosajiliwa ilikuwa 80.
“Na mwaka 2023 tulisajili miradi 526 kati ya hiyo miradi ya ubia wa Watanzania na wageni ni 130 na mwaka 2024 miradi 901 iliyosajiliwa ya ubia ni 176,” alisema John.
Mhadhiri katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Profesa Abel Kinyondo alisema utawala bora ni muhimu ili kuongeza tija ya PPP.
“Ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ni muhimu lakini hauleti ufanisi na maendeleo pamoja na fedha moja kwa moja kama ambavyo nadharia zinatueleza, lakini zinaweza kufanya hivyo kama kuna utawala bora,” alisema Profesa Kinyondo.
Imeandikwa na Zena Chande na Lidya Inda