Thamani vitega uchumi NSSF juu asilimia 92

THAMANI ya vitega uchumi vya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeongezeka kwa asilimia 92 kwa…
The post Thamani vitega uchumi NSSF juu asilimia 92 appeared first on HabariLeo.
THAMANI ya vitega uchumi vya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeongezeka kwa asilimia 92 kwa miaka minne, imefahamika.
Imeongezeka kutoka Sh trilioni 4.28 kwa mwaka ulioishia 2021 mpaka Sh trilioni 8.21 kwa mwaka ulioishia Februari 2025 sawa na ongezeko la asilimia 92.
Aidha, katika kipindi hicho pia thamani ya mfuko imeongezeka kwa asilimia 92 kutoka Sh trilioni 4.83 Februari 2021 hadi Sh trilioni 9.29 kwa Februari 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana ni kutokana na maboresho yaliyofanywa na serikali kuwa na mchango chanya na wenye manufaa katika ukuaji wa mfuko huo.
Mshomba amesema hayo Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari kueleza mafanikio ya taasisi hiyo kwa miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa wanachama, mapato yatokanayo na michango na kukua kwa thamani ya vitegauchumi vya mfuko, mwenendo mzuri wa ukuaji wa mfuko unaashiria uhimilivu na uendelevu imara wa mfuko,” alisema Mshomba.
Alisema kwa kipindi hicho ustahimilivu wa mfuko umefikia asilimia 90.7 na kwamba matokeo ya tathmini ya uhai na uendelevu wa mfuko katika kipindi kinachoishia Juni 2023, yameonesha kuwa kiwango cha sasa cha uchangiaji cha asilimia 20 kitatosha kugharamia ulipaji wa mafao, gharama za uendeshaji na gharama zingine kwa kipindi kirefu.
“Aidha, tathmini inaonesha hali ya ustahimilivu ya mfuko ni asilimia 90.7 kwa kipindi kilichoishia Juni 2023 ukilinganisha na asilimia 87.7 iliyokuwepo katika tathmini ya kipindi kilichoishia Juni 2020, hii inaashiria kwamba mfuko upo katika hali nzuri,” alisema Mshomba.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne mfuko umeongeza uwezo wake wa kukusanya michango ikikusanya Sh trilioni 6.99 kutoka kwa wanachama, na michango inayokusanywa kwa mwaka ikiongezeka kutoka Sh trilioni 1.13 katika mwaka ulioishia Februari 2021, hadi kufikia Sh trilioni 2.15 katika kipindi kilichoishia Februari 2025, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 90.
Kuhusu mafao, Mshomba alisema kwa miaka minne mfuko ulilipa mafao ya Sh trilioni 3.10, na malipo ya mafao kwa mwaka yaliongezeka kwa asilimia 69 kutoka Sh bilioni 537.08 mwaka 2021 mpaka Sh bilioni 909.16 Februari 2025.
Alisema katika kipindi cha miaka minne, wanachama wapya 1,052,176 wameandikishwa baada ya serikali
kutekeleza mikakati mbalimbali kuimarisha uchumi na kufungua fursa za uwekezaji na biashara.
Aidha, alisema kutokana na mabadiliko ya kanuni ya ulipaji mafao ya kustaafu (kikokotoo) yaliyofanyika na kuanza kutekelezwa Julai 2022, wastaafu wa NSSF walianza kupokea mkupuo wa awali wa asilimia 33 ukilinganishwa na asilimia 25 waliyokuwa wakilipwa kabla ya mabadiliko hayo.
“Aidha, kutokana na utendaji uliotukuka wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwajali wastaafu, mfuko umeendelea kuboresha tena ulipaji wa mafao kwa wanachama wote waliokuwa wanalipwa mkupuo wa awali wa asilimia 33 na kuanzia Julai 2022, waliongezewa kiwango cha mkupuo kufikia asilimia 35… uamuzi huu wa serikali wa kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kwa wanachama wa NSSF pia umezingatia uendelevu wa mfuko wetu,” alisema Mshomba.
Alisema wapo kwenye hatua za mwisho kuboresha kiwango cha kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu kutoka Sh 100,000 hadi Sh 150,000 huku viwango vingine vya pensheni vikitarajiwa kuongezeka kwa kati ya asilimia mbili na asilimia 20.
The post Thamani vitega uchumi NSSF juu asilimia 92 appeared first on HabariLeo.