Tathmini ya mikataba kuepuka ulipaji kodi maradufu Tanzania

Habari Leo
Published: Jan 14, 2025 07:42:12 EAT   |  Travel

TANZANIA nchi iliyopo Afrika Mashariki inajivunia utajiri mkubwa wa maliasili ilizo nazo pamoja na mwelekeo wake thabiti wa…

The post Tathmini ya mikataba kuepuka ulipaji kodi maradufu Tanzania appeared first on HabariLeo.

TANZANIA nchi iliyopo Afrika Mashariki inajivunia utajiri mkubwa wa maliasili ilizo nazo pamoja na mwelekeo wake thabiti wa ukuaji wa uchumi unaoifanya kuwa kivutio na chaguo kuu la uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI).

Ikiwa na vyanzo mbalimbali vya kiuchumi vikihusisha kilimo, madini na uzalishaji viwandani, Tanzania inakusudia  kutumia uwekezaji huo si tu kama chanzo muhimu cha mtaji, bali pia kama njia ya kuhamisha teknolojia, kuunda ajira na vyanzo mbalimbali vya uchumi.

Hata hivyo, kadiri uwekezaji huo unavyozidi kuwa muhimu katika mkakati wa kiuchumi nchini, ni muhimu pia kuelewa taratibu zinazowezesha uwekezaji huo. Kwa kiasi kikubwa, mikataba ya kuepusha kodi maradufu inachochea na kuifanya Tanzania kuwa kivutio zaidi cha uwekezaji hasa katika sekta ya ujenzi.

Mikataba hii ni makubaliano kati ya nchi mbili au zaidi yanayolenga kuepuka kutozwa kodi mara mbili kwa mapato yanayopatikana katika nchi hizo.

Mhandisi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika Mkoa wa Manyara, Brenda Kiwelu anabainisha namna mikataba hiyo (DTAs) inavyopunguza suala la ulipaji kodi maradufu unaofanya mapato kutozwa kodi katika maeneo mbalimbali.

Si tu kwamba unafuu huu wa kifedha unaongeza mvuto wa uwekezaji Tanzania, bali pia una ushawishi mkubwa katika kuvutia kampuni za ujenzi za kigeni.

Kiwelu anasisitiza kuwa, dhamira ya kampuni ya Kichina inayoongoza ujenzi wa Barabara ya Mburu-Garababi mkoani Manyara ni mfano bora wa imani waliyo nayo wawekezaji wa  kimataifa katika mazingira ya kodi ya Tanzania ikichochewa na mikataba hiyo (DTAs).

Mikataba hiyo inarahisisha wajibu wa kikodi na inawiana na maboresho makubwa ya kodi yanayofanywa Tanzania kujenga na kukuza mfumo wa kodi ulio wazi, wa haki na wenye ufanisi. Mfumo huu saidizi wa kodi ni muhimu kwa
kampuni za kimataifa za ujenzi zinazofanya miradi mikubwa na hivyo, kuiweka Tanzania kuwa soko linalovutia jitihada za kimataifa za ujenzi.

Makala haya yanabainisha namna DTAs nchini inavyosaidia maboresho ya kodi na kuchochea ukuaji wa uchumi huku yakibainisha mikataba hiyo inavyowiana na malengo ya taifa ya kodi, kuvutia wawekezaji kutoka nje na kutoa taswira ya mwelekeo wa uchumi wa nchi.

Huku yakijikita kutazama mafanikio na changamoto, makala haya yanatoa maarifa mapya kuhusu nafasi ya DTAs katika kubadili hali ya taifa kifedha

Ufupisho wa DTAs ya Tanzania

Tanzania imejihusisha kikamilifu kuanzisha DTAs kukuza uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) na kurahisisha wajibu wa kikodi kwa wawekezaji wa kimataifa. Mikataba hii ina mchango mkubwa katika kuondoa
utozaji kodi maradufu katika mapato ambayo yangeweza kutozwa kodi katika nchi ya mwekezaji na Tanzania.

Hili ni suala muhimu katika kushawishi uamuzi wa uwekezaji na uhusiano wa kiuchumi. Mhasibu na Mshauri wa Kodi anayeishi Dar es Salaam, Kelvin Paschal anasema Tanzania imesaini DTAs na mataifa mbalimbali ili kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi duniani na kutoa mifumo wazi ya kodi.

Miongoni mwa nchi hizo ni India, Afrika Kusini, Italia, Canada, Uingereza na mataifa ya Skandinavia—Sweden, Norway, Denmark na Finland. Hii ni mifano michache tu ya mtandao mpana wa Tanzania wa DTAs unaolenga kuondoa utozaji kodi maradufu na kuzuia ukwepaji wa fedha katika kodi ya mapato na kodi ya mtaji.

Kufanya hivyo hupunguza mzigo wa kodi katika vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwamo faida ya biashara, gawio na mrabaha na hivyo, kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha wawekezaji kutoka nje. Zaidi ya hayo, Tanzania ina mikataba ya kikanda na nchi jirani zikiwamo Zambia, Kenya na Uganda, inayokuza utangamano wa kiuchumi na kushughulikia changamoto za uwekezaji na kodi katika Afrika Mashariki.

Zikiwa zinawakilisha sehemu ya mtandao mkubwa wa DTA wa Tanzania, nchi hizi pia zinatumika kama rejea muhimu kuelewa namna mikataba hii inavyowezesha biashara na uwekezaji wa mipakani. Kwa mujibu wa mtaalamu maarufu wa masuala ya kodi, Barita Taseni, manufaa ya mikataba ya kuepusha kodi maradufu yana sura nyingi na muhimu katika kukuza na kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.

Kimsingi anasema, mikataba hiyo (DTAs) hufanya kazi ya kuzuia utozwaji kodi maradufu kwa kuhakikisha mapato yanatozwa kodi katika nchi moja tu au kwa viwango vilivyopunguzwa katika nchi chanzi na madeni ya kodi yaliyo katika nchi ya mwekezaji.

Taseni anasema, “Kwa kiasi kikubwa mfumo huu hupunguza madeni ya kodi kwa wawekezaji wa kigeni na kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji wa kimataifa.” Anasisitiza kuwa, mikataba hiyo ni zaidi ya unafuu wa kodi kwa kuwa pia huchangia ushirikiano mpana wa kiuchumi kwa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi
husika katika mkataba huo.

“DTAs pia zina nafasi muhimu kuboresha utekelezaji wa taratibu, kanuni na sheria za kodi kwa kuwezesha usimamizi bora katika utekelezaji wa sheria za kodi, kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa kati ya mamlaka za kodi na kuhakikisha uwazi na ufanisi zaidi.”

Kwa mtazamo wake, mtandao wa DTA unaozidi kupanuka nchini Tanzania ni sehemu ya jitihada za kimkakati za
kuunganisha kwa karibu zaidi uchumi wa dunia. “Kwa kuweka mazingira ya kodi yaliyo wazi na rafiki kwa wawekezaji, Tanzania inalenga kuvutia uwekezaji wa kimataifa na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia kanuni za haki za kodi na zinazofaa,” anasema Taseni.

Mifano ya DTA

Mikataba ya kuepusha kodi maradufi baina ya Tanzania na India ni mfano bora wa namna mikataba hiyo inavyoweza kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kuchochea uwekezaji. Kimsingi, mikataba hiyo ya 1979 na iliyoboreshwa mwaka 2013, imekuwa nguzo imara ya ushirikiano wa kiuchumi baina ya mataifa hayo mawili.

Wataalamu mbalimbali wanasisitiza umuhimu wa mikataba wakitilia mkazo matumizi na athari zake kwa uchumi wa Tanzania. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya uhandisi na mshauri wa zamani wa masuala kodi, Emmanuel Edwin anafafanua kuhusu upeo na madhumuni ya DTAs.

Anasema makubaliano hayo yalianzishwa kuondoa tishio la utozaji kodi maradufu kwa mapato yanayopatikana kutokana na kuvuka mipaka, yakijumuisha vyanzo mbalimbali vya mapato yakiwamo yatokanayo na faida za biashara, gawio, riba, mrabaha na ongezeko la mtaji.

Edwin anasema: “Mikataba hii inapunguza mzigo wa kifedha na kiutawala kwa wawekezaji huku ikiwezesha urahisi katika uendeshaji wa kifedha na kuhimiza ushirikiano wa kina wa kiuchumi baina ya Tanzania na India.” Ikiwa miongoni mwa washirika wakuu wa uwekezaji wa Tanzania, India inajihusisha kwa kiasi kikubwa katika sekta
muhimu kama viwanda, madini na huduma.

Kwa mujibu wa Edwin, mikataba hiyo hurahisisha majukumu ya kodi na kutoa utabiri unaohitajika katika taratibu za kodi hali inayofanya Tanzania kuwa kivutio cha kwa mashirika ya India.

“Kabla ya DTAs, gawio lililolipwa na kampuni ya Kitanzania kwa wanahisa wa India lingeweza kutozwa kodi katika nchi zote mbili,” anasema Edwin.

Anaongeza: “Sasa, gawio hili ama linatozwa kodi nchini India pekee au kwa viwango vilivyopunguzwa nchini Tanzania, ikiwa na mikopo ya kodi inayopatikana nchini India kwa kodi inayolipwa hapa nchini, hivyo kuondosha kabisa utozaji kodi maradufu.”

Mtaalamu wa masuala ya kodi, Taseni anaunga mkono maoni haya akisisitiza kuwa, vifungu hivyo vinapunguza
madeni ya kodi kwa wawekezaji wa kigeni na hivyo kuweka mazingira thabiti zaidi na ya kuvutia ya uwekezaji.

Naye Paschal, mshauri wa masuala ya kodi anazungumzia athari kubwa zaidi za DTAs kuhakikisha wawekezaji wa
kigeni wanatendewa haki kupitia viwango vya kodi vilivyopunguzwa kwa riba na mirabaha na ushughulikia bora wa ongezeko la mitaji ambazo kwa ujumla hutozwa kodi katika nchi anayoishi muuzaji pekee.

“Kimsingi, faida za kiuchumi za DTAs zinadhihirika katika uwekezaji iliohimiza,” sema Emmanuel. Anasisitiza namna kampuni kama Bharti Airtel zilivyopanua shughuli kwa kiasi kikubwa katika sekta ya mawasiliano nchini Tanzania zikisaidiwa na punguzo la mzigo wa kodi kwa faida na mirabaha kwa matumizi ya teknolojia.

Kadhalika, taasisi kama Benki ya Baroda zimefanya kazi kubwa kusaidia miradi na biashara za ndani ikisaidiwa na huduma bora na rafiki za kodi katika mapato yakiwamo mapato ya riba.

Hii ni mfano tu inayoonesha athari chanya za DTAs katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji. Uwekezaji wa India nchini Tanzania umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 20 kwa mwaka tangu yalipofanyika marekebisho ya mwaka 2013 na kuchangia ongezeko la asilimia 15 la mapato ya kodi kutoka katika kampuni za India.

Katika kampuni hizo, ajira zimeongezeka kwa asilimia 25 na kutengeneza nafasi zaidi ya 15,000. Kwa mujibu wa Paschal, takwimu hizi zinaonesha namna DTAs zinavyoweza kupunguza vikwazo katika biashara ya kimataifa na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Bado kuna changamoto

Ugumu uliopo katika usimamizi na gharama kubwa zilizopo katika utekelezaji wa sheria za kodi, hukwamisha ufikiaji kamili wa manufaa ya mikataba hiyo (DTAs). Aidha, tofauti katika manufaa ya kiuchumi miongoni mwa
washirika wa mkataba huo imesababisha kuwapo mwito mpya wa mazungumzo kuhakikisha pande zote zinapata matokeo sawa.

“Bila shaka wakati mikataba hiyo (DTAs) inaongeza uwekezaji, maboresho yanayoendelea ni muhimu ili kuongeza manufaa ya mikataba hiyo,” anasema Taseni.

Katika tafakari yake kuhusu jambo hili, Edwin yeye anasema, “Bado kuna kazi ya kufanya kuhakikisha DTAs zinaendelea kuleta manufaa kwa pande zote na kuendana na vipaumbele vinavyoendelea vya uchumi vya Tanzania.”

Athari za DTAs katika maboresho ya kodi

DTAs zina nafasi kubwa katika juhudi za Tanzania kufanya mfumo wa kodi kuwa wa kisasa na unaovutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Kwa kuzuia kutozaji kodi maradufu, mikataba hiyo (DTAs) inawapunguzia wawekezaji mzigo wa kodi na kuifanya
Tanzania kuwa kivutio zaidi kwa biashara za kimataifa. Kimsingi, mikataba hii ni zaidi ya kurahisisha kodi kwani
hujenga uaminifu na ushirikiano miongoni mwa mataifa kwa kuwezesha ushirikishanaji taarifa na kuimarisha mifumo ya utekelezaji wa sheria za kodi.

Aidha, DTAs huchangia ujenzi wa mazingira ya kodi yanayotabirika ambayo ni muhimu kwa mipango ya muda mrefu ya uwekezaji na utulivu wa kiuchumi. Ingawa faida za mikataba hiyo ziko wazi, bado utekelezaji wake una changamoto fulani.

Kuoanisha majukumu ya mkataba na vipaumbele vya kodi ya ndani vinavyoendelea vya Tanzania bado ni kazi nyeti.
Ili kufikia uwiano sahihi kati ya kuvutia uwekezaji wa kigeni na kulinda malengo ya taifa ya mapato, kunahitajika mazungumzo thabiti na ya kimkakati.

Zaidi ya hayo, kadiri hali ya uchumi wa dunia inavyobadilika, suala la kuhakikisha mikataba hiyo inakuwa na manufaa sawa kwa wadau wote linazidi kuwa muhimu. Licha ya changamoto, mikataba hiyo inaendelea kuwa nguzo
imara ya mkakati wa Tanzania kuunganisha uchumi wa dunia na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.

Hitimisho

Makala haya yamejikita kubainisha nafasi muhimu ya mikataba/ makubaliano kuhusu utozaji kodi maradufu (DTAs)
katika ujenzi wa mazingira bora zaidi ya kodi nchini Tanzania ili kuvutia wawekezaji kutoka nje ya Tanzania.

Hata hivyo licha ya kuwa na manufaa mengi, mikataba hii ina changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kufungua kikamilifu uwezo na manufaa yake.

Makala yajayo yatajikita katika masuala muhimu ya usimamizi na utekelezaji wa sheria za kodi yanayoweza kuzuia
ufanisi wa mikataba hiyo na pia, makala yatajadili maboresho ya kibunifu yanayoweza kufanya mikataba kuwa bora zaidi.

Endelea kufuatilia kwa undani ujue fursa na vikwazo katika ulimwengu wa mikataba ya kuzuia utozaji kodi maradufu!

The post Tathmini ya mikataba kuepuka ulipaji kodi maradufu Tanzania appeared first on HabariLeo.