Tanzania yatajwa kinara kiuchumi

Habari Leo
Published: May 17, 2025 08:04:21 EAT   |  Business

RAIS wa Finland, Alexender Stubb ameipongeza Tanzania kwa juhudi kubwa inazochukua kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kusema hatua hizo zinaifanya iwe nchi yenye mazingira bora ya kiuchumi kwa maendeleo ya muda mrefu. Sambamba na hilo, Rais Samia Suluhu Hassan amemuaga Stubb aliyewasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu. Akizungumza Dar es …

RAIS wa Finland, Alexender Stubb ameipongeza Tanzania kwa juhudi kubwa inazochukua kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kusema hatua hizo zinaifanya iwe nchi yenye mazingira bora ya kiuchumi kwa maendeleo ya muda mrefu.

Sambamba na hilo, Rais Samia Suluhu Hassan amemuaga Stubb aliyewasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu.

Akizungumza Dar es Salaam kwenye kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Finland, Stubb alisifu juhudi hizo akisema si tu zinavutia wawekezaji wa ndani na nje, bali pia zinaifanya Tanzania kuwa yenye mazingira bora ya kiuchumi kwa maendeleo ya muda mrefu.

“Na hii inaonesha dhamira ya dhati ya serikali,” alisema Rais Stubb.

Alisema hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha mazingira hayo, kunalifanya taifa hilo kujenga uchumi imara na shindani unaoendana na kasi ya mabadiliko ya dunia ya sasa.

Alisema Finland ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa karibu katika maeneo ya kipaumbele yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Alitaja sekta za kipaumbele kwenye hilo kuwa ni pamoja na elimu na mafunzo ya ufundi, nishati jadidifu, afya, kilimo endelevu na uhifadhi wa maeneo ambayo Finland ina uzoefu mkubwa na iko tayari kushiriki kwa dhati katika miradi ya maendeleo.

Alisema ushirikiano huo unalenga kuimarisha ustawi wa wananchi wa pande zote mbili kwa njia ya kubadilishana maarifa, teknolojia na kuwajengea uwezo rasilimali watu.

Rais Stubb alisema Finland inaitazama Tanzania kama lango muhimu kuelekea masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutokana na nafasi yake ya kijiografia na ushawishi wake wa kikanda.

Aidha, alisisitiza mazingira hayo yanaiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee kama kituo cha biashara na uwekezaji kwa kampuni za nchi hiyo zinazotaka kupanua shughuli zao Afrika.

Alitoa wito kwa sekta binafsi kutoka nchi zote mbili kuchangamkia fursa zilizopo kwa kuanzisha na kukuza ushirikiano wa kibiashara unaoleta tija kwa wote.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza katika kongamano hilo alimshukuru, Rais Stubb na ujumbe aliofuatana nao na kusisitiza kuwa ziara hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya Finland kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na Tanzania.

Alisema kampuni nyingi kutoka Finland zimeonesha nia ya kuwekeza na kushirikiana na Tanzania katika sekta muhimu kama vile mawasiliano na teknolojia ya habari, afya na uzalishaji wa dawa na teknolojia za kisasa za kilimo.

Alisema serikali imeboresha mazingira bora kwa ajili ya wawekezaji ikiwemo kurahisisha taratibu za usajili, kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha na kuboresha mifumo ya mipakani.

Hivyo alihamasisha wafanyabiashara wa Tanzania kutumia fursa za soko la Finland, hasa katika bidhaa za kilimo hai, mazao ya chakula na nguo, akibainisha kuwa soko la Finland linathamini ubora, uwazi na uendelevu.

Rais Stubb pia aliwatembelea Wanawake Wajasiriamali katika Soko la Machinga Complex na kuwapongeza kwa ujasiri wa uongozi wao katika kuendesha biashara.

Akiwa ameambatana na mkewe, Suzanne Innes-Stubb, pamoja na ujumbe wa ngazi ya juu wakiwemo wabunge kutoka Finland, Rais Stubb alikutana na wanawake wajasiriamali na viongozi wa serikali za mitaa ambao ni wanufaika wa Mradi wa Uongozi wa Wanawake na Haki za Kiuchumi (WLER).

Mradi unatekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake(UN-Women) kwa kushirikiana na Serikali
ya Tanzania kwa msaada kutoka Serikali ya Finland.

Kupitia mradi huo, zaidi ya wanawake 1,060 wamechaguliwa kushika nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024.

Mradi huo umewezesha wanawake kupata mikopo isiyo na riba kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa, huku wanawake zaidi ya 600 mkoani Mtwara wakisajili ardhi kwa majina yao kwa mara ya kwanza.

Mwakilishi wa UN Women nchini, Hodan Addou alisema Machinga Complex ni eneo muhimu lenye zaidi ya wanawake 3,000 wanaofanya biashara na limekuwa kitovu cha utekelezaji wa mradi wa WLER.

Akizungumza na wanawake hao, Rais Stubb aliwahakikishia kuwa Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza usawa wa kijinsia kupitia sera yake ya kigeni ya kifeministi na ushirikiano wa maendeleo.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisifu jitihada hizo akisema kuwa mradi wa WLER unaonesha dhamira ya kweli ya Serikali ya Tanzania katika kuwawezesha wanawake wa sekta isiyo rasmi na kutekeleza ajenda ya Jukwaa la Usawa wa Kizazi.

Wakati huo huo, Rais Stubb aliagwa jana Ikulu Dar es Salaam kwa gwaride maalumu lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, ikiwemo wakuu wa ulinzi na usalama.

Msafara wa Rais Stubb ulipowasili katika viwanja vya ikulu, ulipokewa na mwenyeji wake, Rais Samia na moja kwa moja walielekea kwenye eneo maalumu lililoandaliwa kwa ajili ya kuagwa.

Katika hafla hiyo, Wimbo wa Taifa la Tanzania uliimbwa pamoja na wa Finland kama ishara ya kushirikiana.

Baada ya tukio hilo, Rais Stubb alitumia muda huo kuagana na viongozi wa Tanzania waliofika katika hafla hiyo.

Katika ziara hiyo, Tanzania na Finland zimekubaliana kuimarisha uhusiano na biashara katika maeneo tisa yenye fursa.

Maeneo hayo ni sekta ya elimu, biashara, nishati, utalii, uhusiano wa kimataifa, uwekezaji, uhamilishaji wa teknolojia, madini na uchumi wa buluu.

Aidha, nchi hizo zimekubaliana kuendeleza kwa dhati uhusiano wao kwenye maeneo hayo na kuongeza maeneo mapya ambayo ni uchumi wa buluu na nishati.

Rais Stubb aliwasili nchini Mei 14, mwaka huu kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu akiambatana na mke wake.