Tanzania mwenyeji tuzo za kimataifa za utalii, nchi 30 kushiriki

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za Kimataifa za Utaili zijulikanazo kama World Travel Awards katika hafla ya kutangaza washindi wa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi. Hafla hiyo ya kutangaza washindi wa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi ‘Africa & Indian Ocean Gala Ceremony’ itafanyika […]
Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za Kimataifa za Utaili zijulikanazo kama World Travel Awards katika hafla ya kutangaza washindi wa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi.
Hafla hiyo ya kutangaza washindi wa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi ‘Africa & Indian Ocean Gala Ceremony’ itafanyika Juni 28, 2025 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Aprili 14,2025 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephrahim Mafuru, amesema tuzo hizo zimekuwa chachu ya ubunifu, ushindani na kuboresha viwango vya huduma duniani kote.
Amesema mchakato wa kupiga kura kwa kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi ulifunguliwa rasmi Machi 11,2025 na utafikia tamati Mei 4,2025.
Amesema Tanzania imetajwa katika vipengele zaidi ya 15 nchi inayoongoza kwa Utalii Afrika (Africa’s leading Destination), Bodi bora ya Utalii Afrika (Africa’s leading Tourist Board) – Bodi ya Utalii Tanzania, Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika (Africa’s leading Tourist Attraction) Ngorongoro, Mlima unaoongoza Afrika Mlima Kilimanjaro.
Vipengele vingine ni Hifadhi Bora ya Taifa Barani Afrika (Africa’s leading National Park) Serengeti, Hifadhi za Kitulo, Nyerere, Udzungwa, Mahale, Arusha Tarangire na nyingine zimetajwa katika vipengele vingine kulingana na ubora wake.
Pia vimo vipengele vya Uwanja Bora wa Ndege Barani Afrika – Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Bandari Bora Barani Afrika – Bandari ya Dar es Salaam, Fukwe Bora Afrika Zanzibar.
Zimo pia kampuni za watoa huduma za usafiri, malazi na waongoza watalii nchini nazo zimetajwa katika makundi ya tuzo hizio.
“Tukio hili ni fursa ya kuutangaza Tanzania kama kivutio bora cha utalii duniani, wageni kutoka zaidi ya nchi 30 wanatarajiwa kushiriki, wakiwemo wawekezaji, wanahabari wa kimataifa, viongozi wa sekta ya utalii na wadau mbalimbali.
“Kupitia jukwaa hili tutapata nafasi ya kuonesha vivutio vyetu vya kipekee ikiwemo milima, hifadhi za wanyamapori na misitu, fukwe, vyakula, tamaduni zetu na nyingine,” amesema Mafuru.
Ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya utalii, mabalozi, watalii, wasanii, vyombo vya habari na wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura kwa vivutio vya Tanzania.
Tanzania imekuwa ikitambulika kwa ngazi za Kikanda na Dunia katika tuzo hizo ambapo mwaka 2024 ilipata tuzo katika makundi ya World’s Leading Safari Destination Africa’s Leading Destination -Tanzania, Africa’s Leading Tourist Board – Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Africa’s Leading Tourist Attraction – Hifadhi ya Taifa Mlima Kilimanjaro na Africa’s Leading National Park – Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Pia wadau wa utalii walipewa tuzo hizo kwa ngazi ya Kikanda na Dunia.
Aidha, Bodi ya Utalii Tanzania kama Taasisi yenye jukumu la kutangaza Utalii nchini ndio tutaratibu hafla hii.
Mkurugenzi huyo wa TTB amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kuitangaza sekta ya utalii kupitia juhudi mbalimbali anazozifanya.
“Heshima hii ya kuwa mwenyeji wa World Travel Awards ni matokeo ya jitihada zake na maono ya kuiletea Tanzania maendeleo kupitia utalii. Nawasihi Watanzania kushiriki kikamilifu kupigia kura vivutio vyetu ili kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais wetu na kuweza kuwapokea wageni wanaokuja tukiwa kifua mbele kwa kushinda tuzo hizi,” amesema Mafuru.
Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 1993 na Kampuni ya World Luxury Media Group zikiwa na lengo la kutambua, kuthamini na kusherehekea mchango wa wadau katika Sekta ya Utalii na Ukarimu Duniani.
Wadau wanaotambuliwa kupitia tuzo hizi ni pamoja na mashirika ya ndege (Airlines), watoa huduma za malazi (Accomodation facilities), vivutio vya utalii (Tourist attractions), Wakala wa biashara za utalli (tour operators), Mamlaka za Usimamizi na Utangazaji Utalli na wadau wengine muhimu katika sekta hii.
Ili kuweza kupigia kura vivutio vya Tanzania ingia katika tovuti ya https://www.worldtravelawards.com/vote.