Tanzania, Msumbiji kimkakati biashara, uwekezaji

SERIKALI za Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji. Rais Samia Suluhu Hassan alisema hayo Ikulu, Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na kuzungumza na mgeni wake Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu. Alisema wamekubaliana kuwawezesha …
SERIKALI za Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji.
Rais Samia Suluhu Hassan alisema hayo Ikulu, Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na kuzungumza na mgeni wake Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Alisema wamekubaliana kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati ili wafanye biashara kwa urahisi.
Rais Samia alisema wamekubaliana kuharakisha uanzishwaji wa vituo vya pamoja vya mpakani ili kuondoa shida wanazopata wananchi wa pande zote mbili katika kufanyabiashara za kuvuka mipaka.
“Tukianzisha kituo kimoja cha biashara ambapo watu watapita vizuri pale Mtambaswala tutarahisisha zaidi biashara zetu,” alisema.
Rais Samia alisema wamekubaliana kuanzisha Tume ya Pamoja ya Kiuchumi itakayokuwa na jukumu la kufuatilia kwa karibu zaidi ambayo pande zote mbili zimekubaliana ili kukuza uchumi.
Alisema uhusiano wa kiuchumi unakuzwa na kuimarika kwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji na hivyo wamezungumzia masuala ya ujenzi wa barabara za mipakani zinazounganisha nchi zote mbili.
Rais Samia alisema amefanya mapitio ya mkataba wa ushirikiano wa usafiri wa anga na kuimarisha usafiri wa majini kupitia Ziwa Nyasa na Mto Ruvuma.
Alisema mawaziri wa masuala ya uchumi na uchukuzi walikutana Mei 6, mwaka huu Dar es Salaam kuangalia namna ya kuimarisha uhusiano wa mataifa hayo mawili katika eneo hilo.
Rais Samia alisema Tanzania ina mpango wa kujenga reli ya kisasa (SGR) itakayounganisha Bandari ya Mtwara na Mbamba Bay hadi katika maeneo yenye machimbo ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga mkoani Ruvuma.
Alisema kwa kufanya hivyo Tanzania itakuwa imeufungua ushoroba wa Kusini na kuiunganisha na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.
“Nchi zetu mbili zimebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa gesi hivyo tukazungumzia na kukubaliana kubadilishana za pamoja,” alisema Rais Samia.
Pia, alisema Tanzania na Msumbiji zina eneo kubwa la Bahari ya Hindi na fursa za utajiri unaotokana na uchumi wa buluu ukiwemo uvuvi, utalii, madini na usafirishaji.
Rais Samia alisema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya rasilimali za baharini, kubadilishana uzoefu na kufanya kazi kwa karibu kwenye masuala ya Bahari Kuu, utalii na usafirishaji.
Alisema kwa kuwa uchumi wa nchi hizo unategemea kilimo, wamekubaliana kushirikiana katika kilimo hasa kubadilishana uzoefu na kufanya tafiti za pamoja hususani kwenye zao la korosho.
Alikaribisha watafiti kutoka Msumbiji katika Taasisi ya Utafiti ya Naliendele mkoani Mtwara kuja kujifunza namna Tanzania inavyotumia taasisi hiyo kuimarisha kilimo hasa cha korosho.
Rais Samia alitaja maeneo mengine ya kuimarisha uhusiano ambayo waliyozungumzia ni pamoja na madini, mawasiliano, elimu na afya.
“Kwenye masuala ya kimataifa tumekubaliana kuendelea kushirikiana katika majukwaa ya kikanda kupitia Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) ambako sote ni wanachama,” alisema.
Rais Samia alisema wamejadiliana kuhusu masuala ya amani usalama na utangamano wa Bara la Afrika na kukubaliana pia kufanya kazi kwa pamoja katika kukabiliana uhalifu wa kimataifa ukiwemo ugaidi na ujangili.
Alimshukuru Rais Chapo kwa ahadi yake ya kumuunga mkono mgombea wa Tanzania kwenye kinyang’anyiro cha Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi.