Tanzania kutumia teknolojia ya kisasa utafiti, uchimbaji mafufa, gesi

Habari Leo
Published: May 27, 2025 19:11:55 EAT   |  General

DAR ES SALAAM: TANZANIA imesema imegeukia matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye utafiti, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi kwa kushirikiana na wadau na wawekezaji wa sekta hiyo ndani na nje ili wananchi wanufaike na taifa pia. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),Charles Sangweni alisema hayo jana Dar …

DAR ES SALAAM: TANZANIA imesema imegeukia matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye utafiti, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi kwa kushirikiana na wadau na wawekezaji wa sekta hiyo ndani na nje ili wananchi wanufaike na taifa pia.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),Charles Sangweni alisema hayo jana Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Jumuiya ya Wafanyakazi Wahandisi wa Sekta ya Petroli Duniani (SPE).

Aidha, alitoa mwito kwa wataalamu wa sekta ya mafuta na gesi duniani kuungana na Afrika kujadili mustakabali wa teknolojia na mabadiliko ya nishati kwa maendeleo endelevu barani humo.

Sangweni alisema mkutano huo mkubwa wa siku mbili umelenga kukuza ubora wa teknolojia kwa ajili ya nishati endelevu Afrika na alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka msisitizo kwenye mabadiliko ya nishati, akisema kuwa suala hilo limekuwa mjadala mkubwa barani Afrika.

“Je, tunawezaje kutoka hapa tulipo hadi kufikia hali ya kutokuwa na hewa ukaa ,yaani tufike asilimia sifuri?,alihoji Sangweni.

Alisema katika kufikia huku, hatua mbalimbali zimechukuliwa na serikali ikiwemo kugeukia teknolojia ya kisasa katika kufanya tafiti, utafutaji na uchimbaji wa bidhaa za petroli kwa ushirikiano na wadau wan je ili kuleta tija nchini.

“Tunataka teknolojia ya kisasa itumike zaidi kuleta mapinduzi kwenye sekta hii bidhaa za petroli zipatikane na zitumike kuwanufaisha Watanzania na taifa,katika hilo hatutawaacha waandisi vijana wa sekta hii,”alisema Sangweni.

Alisema ingawa mabadiliko hayo ya nishati si ya kwanza duniani, kasi yake ni kubwa kuliko yaliyopita, hivyo nchi za Afrika zina jukumu la kuchagua kwenda sambamba au hatua kwa hatua katika safari hiyo ya mapinduzi ya teknolojia katika sekta hiyo.

Hivyo mkutano huo umelenga kujadili mada muhimu kama vile mpito wa kimataifa wa nishati, ushirikishwaji wa jamii za ndani, utofauti na ujumuishwaji, matumizi ya akili unde (AI), sayansi ya data, uhandisi na uchambuzi wa taarifa.

Alisema mada hizo zitasaidia kushughulikia changamoto za sekta ya Petroli Afrika katika ukuaji wa teknolojia na mabadiliko ya nishati huku zikitekeleza dira na malengo ya jumuiya ya SPE ya kusambaza maarifa kwa wanachama wake na jamii kwa ujumla.

“Tanzania imekuwa kinara katika utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya nishati kama vile matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusambaza umeme vijijini,lakini pia sasa tumeanza kutumia gesi asili kama nishati kwenye magari na tunataka tuende mbele zaidi hata kuisafirisha gesi kwa mfumo wa kimilimika kuuza nje,”alisema Sangweni.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya SPE-Afrika Dk Riverson Oppong alisema Tanzania imebainisha vitalu 23 vyenye fursa ya uwekezaji katika uchimbaji wa mafuta na gesi na kuwa hilo ni moja na vitu watakavyojadili kuona jinsi gani wanaweza kushiriki.

“Mkutano huu ni mkubwa na masuala ya Petroli na tutadajili kuku ana kuimarika kwa teknolojia na jinsi tunavyoweza kuitumia kwenye sekta hii ya mafuta na gesi kwa kuwahusisha vijana ili kuleta tija,”alisema Dk Oppong.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyakazi wa Petroli Tanzania (SPE-Tanzania)Alex Stephano alisema mkutano huo umekuwa fursa kwa Tanzania kwani umewakutanisha wahandisi kutoka mataifa mbalimbali Afrika na duniani kuzungumzia fursa zilizopo nchini .

Sptephano alisema yapo maeneo ambayo tafiti za mafuta na gesi yanaendelea na baadhi yamekamilika na gesi inazalishwa na hizo ni fursa zilizovutia washiriki wa mkutano huo kuona jinsi gani wanaweza kushiriki katika mnyororo huo.