SUZA ni matunda ya SMZ kutekeleza Ilani ya CCM

Habari Leo
Published: Feb 19, 2025 08:18:44 EAT   |  Educational

“NASHUKURU sana kupata heshima hii ya juu kwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu katika fani ya elimu ambayo ni…

The post SUZA ni matunda ya SMZ kutekeleza Ilani ya CCM appeared first on HabariLeo.

“NASHUKURU sana kupata heshima hii ya juu kwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu katika fani ya elimu ambayo ni sehemu ya SUZA (Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar) kutambua mchango wangu mkubwa wa kuanzishwa kwake.”

Anasema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora) Dk Haroun Ali Suleiman na kuongeza: “…Kwangu mimi nilikuwa nikitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM (Chama Cha Mapinduzi) ya Mwaka 1995-2000 iliyokuwa ikitutaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuanzisha chuo kikuu chetu.”

Kimsingi, ni sifa na fahari kwa kiongozi wa wizara au taasisi kumaliza muda wake au kuondoka akiacha alama inayotokana na utendaji uliotukuka ambayo haitosahaulika.

Alama hiyo hubaki kuwa kigezo cha utendaji na uwajibikaji katika kuleta ufanisi sehemu ya kazi na kuwawezesha wananchi wengi kunufaika.

Ndivyo ilivyokuwa hata kwa Dk Haroun Ali Suleiman ambaye kutokana na utumishi wake uliotukuka, chuo kikuu hicho cha taifa (Suza) kimemtunuku Shahada ya Uzamivu (PhD) ya heshima kutokana na uwajibikaji wake na kuwa chachu ya kuanzishwa kwa chuo kikuu hicho hicho cha kwanza cha Serikali, Zanzibar mwaka 1999.

Dk Suleiman anakumbukwa kwa kazi kubwa aliyoifanya baada ya kukabidhiwa jukumu la kuhakikisha Suza
kinaanzishwa na kusimama imara. Alilitekeleza jukumu hilo kwa uaminifu. Suza kilimtunuku Shahada ya Uzamivu kutambua mchango wake katika kuanzishwa kwake wakati huo akiwa Waziri wa Elimu.

Anasema: anashukuru kupata heshima hiyo ya kutunukiwa Shahada ya Uzamivu ya heshima katika fani ya elimu ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Suza kutambua mchango wake katika kuanzishwa kwake. “…Kwangu mimi nilikuwa nikitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM (Chama Cha Mapinduzi) ya Mwaka 1995-2000 iliyokuwa ikitutaka
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuanzisha chuo kikuu chetu.”

Kwa mujibu wa Dk Suleiman, kabla ya mwaka 1995 Zanzibar haikuwa na chuo kikuu cha serikali hivyo, wanafunzi wenye sifa za kusoma elimu ya chuo kikuu walilazimika kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Anasema mchakato wa kuanzishwa kwa chuo kikuu hicho ulianza baada ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk Salmin Amour Juma kuunda timu ya wataalamu wakiongozwa Professa Saleh Idrissa (ambaye baadaye alikuwa Makamu Mkuu wa Suza) kuanza mchakato wa kuanzishwa chuo hicho.

Anasema binafsi alishiriki kikamilifu kuanzishwa kwa mchakato huo wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu. Anasema mwaka 1999 aliyekuwa Waziri wa Elimu, Omar Ramadhan Mapuri aliwasilisha katika Baraza la
Wawakilishi muswada wa kuanzishwa Suza kwa mujibu wa sheria.

Muswada huo ulipata baraka za wawakilishi na kupitishwa na wajumbe Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kauli moja huku wale wa Chama cha Wananchi (CUF) wakipinga kwa kile walichosema Zanzibar haikuwa tayari kuwa na chuo kikuu chake.

“Muswada wa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) ulipitishwa na wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi ingawa wenzetu wapinzani waliupinga kwa madai kwamba Zanzibar haijawa tayari kuwa na chuo kikuu chake,” anasema.

Suleiman anasema mchakato wa kuanzishwa Suza ulisonga mbele baada ya Rais wa Zanzibar wakati huo, Amani Abeid Karume kumteua kuwa Waziri wa Elimu mwaka 2000. Anasema alipata nafasi ya kumkabili Rais Karume na kumuuliza kwanini Ilani ya CCM inayotaka Zanzibar kuwa na chuo chake haitekelezwi wakati mchakato wake ulishakamilika na unasubiri utekelezaji.

Anasema anakumbuka namna alivyokutana na maswali magumu kutoka kwa Rais Karume. Kwamba, Rais Karume
alimhoji kama jambo hilo linawezekana na kutaka kujua kama wana majengo kwa ajili ya chuo na kama walimu walikuwepo.

“Maswali yote aliyoniuliza Rais Karume niliyajibu na kumwambia majengo ya kuanzia yapo hapo Chuo cha Taasisi ya Elimu ya Kigeni na walimu wapo wa kutosha,” anasema. Anasema hapo alianza kuona mwanga wa kuanzishwa kwa chuo kikuu cha kwanza cha taifa, Zanzibar.

Hata hivyo anasema haikuwa rahisi kwa sababu ilimlazimu kusafiri mara kwa mara kwenda Bara kwa ajili ya maandalizi ya chuo ikiwa ni pamoja na kushughulikia suala la ithibati ambalo hutolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Anasema ilifika wakati akihisi ‘kugonga mwamba’katika suala la upatikanaji wa ithibati, lakini baadaye alifanikiwa
kwa msaada wa viongozi wa nchi wa pande zote yaani Zanzibar na Tanzania Bara. “Nakumbuka suala hili
walilazimika kuingilia kati marais wote wawili yaani Rais Jakaya Kikwete na Rais Karume (Amani) mwenyewe,” anasema.

Aidha, anasema heshima kubwa aliyopewa na Suza ni zawadi kwa Wazanzibari wote katika kuona chuo hicho kinasimama na Wazanzibari wanakuwa na chuo chao kinachoshughulikia maendeleo ya elimu ya kwao wenyewe.
Dk Suleiman anasema anajivunia kufanya kazi na marais wanne wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika nafasi mbalimbali.

“Nashukuru Mungu nimefanya kazi na marais wanne wa Zanzibar wakiwemo wastaafu kwa kushika wizara tofauti kuanzia elimu hadi utawala bora katiba na sheria,” anasema. Waziri Dk Suleiman licha ya utumishi wake serikalini
kwa zaidi ya miaka 49, pia ni kada wa Chama Cha Mapinduzi anayewatumikia wananchi wa Jimbo la Makunduchi kwa muda wa vipindi vitano tangu mwaka 2000.

Anasema siri ya kushika nafasi ya uwakilishi wa Makunduchi kwa kipindi chote hicho ni ushirikiano na wananchi na wanachama katika kutafuta maendeleo bila ubaguzi. Dk Suleiman anasema siku zote unapokuwa mwakilishi au mbunge, hauna budi kufahamu na kuzingatia kuwa, wewe ni mwajiriwa wa wananchi kwani ndio waliokupigia kura na kukuweka katika nafasi hiyo.

Anasema yeye anapoitwa na wananchi wa jimbo lake kwa shughuli yoyote au kumhitaji, huwa hasiti kufanya hivyo kwa sababu anafahamu waliomwita ndio waajiriwa wake. “Ukiitwa na wapiga kura wako katika jimbo la uchaguzi kama ni waziri basi unatakiwa uweke pembeni mambo yako yote kwa sababu hao ndio waajiri wako,” anasema.

Aidha, anasema anajivuna na kuona fahari kwamba ufaulu unazidi kuongezeka kwa wanafunzi wa kike katika chuo
hicho jambo ambalo ni faraja kubwa kwa wanawake katika siku za baadaye kushika hatamu ya kuongoza nchi katika
ngazi mbalimbali.

Anasema sekta ya elimu kwa ujumla imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dk Hussein Mwinyi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule za ghorofa pamoja na vyuo vya amali vitakavyosaidia
kuwaingiza wahitimu wake katika soko la ajira.

“Hayo ni mafanikio makubwa ambayo yamesaidia kuongeza wahitimu kuingia katika vyuo vikuu, mageuzi yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika kipindi cha miaka minne tu ya uongozi wake,” anasema.

The post SUZA ni matunda ya SMZ kutekeleza Ilani ya CCM appeared first on HabariLeo.