Sillah, Saadun wailiza KenGold, Taoussi achekelea

Mwanaspoti
Published: Apr 03, 2025 16:06:58 EAT   |  Sports

Harakati za kujinasua mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara zimeendelea kuwa ngumu kwa KenGold baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Azam FC. Katika mchezo wa leo Aprili 3, 2025 uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, licha ya hali ya hewa kutokuwa nzuri sana kutokana na mvua iliyonyesha, lakini wenyeji walikubali kipondo hicho. Gibril Sillah ndiye alianza kuwainua mashabiki wa Azam kwa bao la kutangulia dakika ya 27 kabla ya Nassor Saadun kupachika la pili dakika ya 37 mabao ambayo yalidumu hadi mapumziko. Kipindi cha pili licha ya timu zote kufanya mabadiliko ya wachezaji, lakini hakukuwa na mabadiliko ya matokeo na kufanya dakika 90 kumalizika kwa Azam kushinda 2-0. Matokeo hayo yanaifanya Azam kubaki nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 51 huku KenGold ikienelea kuwa ya mwisho kwa pointi 16 baada ya timu zote kucheza mechi 24 zikibakiwa na sita kufunga msimu. KenGold inafikisha mechi nne mfululizo bila ushindi ikiwa ni sare tatu dhidi ya Mashujaa 2-2, JKT Tanzania 1-1 sawa na KMC, huku mara ya mwisho kupata alama tatu ilikuwa Februari 18, 2025 ilipoizaba Kagera Sugar 1-0. Kwa upande wa Azam inaendeleza ushindi baada ya mechi iliyopita kutakata kwa mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons, huku mechi mbili nyuma ikiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Namungo na Simba 2-2. Kocha Mkuu wa Azam, Rachid Taoussi amesema matokeo hayo ni kutokana na uimara na ubora wa kikosi chake haswa wachezaji kuwa na morali ya ushindi. Ameongeza kuwa licha ya ushindi huo lakini bado kazi ni ngumu katika mechi sita zilizobaki kuhakikisha wanashinda zote na kusubiri hatma yao katika vita ya ubingwa. "Vijana wanapambana, morali ya ushindi wanayo, lakini hii ni kutokana na ubora na uimara wa timu, niwapongeze lakini tunaenda kujipanga na mechi zinazofuata," amesema kocha huyo. Kocha Mkuu wa KenGold, Omary Kapilima amesema licha ya kupoteza mechi hiyo lakini suala la kushuka daraja haiwezekani kwani wanaenda kujipanga upya kumaliza vyema michezo iliyobaki. "Tumepata nafasi kadhaa tumeshindwa kuzitumia, wapinzani wakapata bahati ya mabao mawili, hatujakata tamaa na mechi sita zijazo tutafanya vizuri, hatushuki daraja," amesema Kapilima.