Shule yafungwa ghafla muhula wa masomo ukianza
WAKATI jana wanafunzi kote nchini wakianza muhula mpya wa masomo, hali ni tofauti kwa Shule ya Sekondari ya…
The post Shule yafungwa ghafla muhula wa masomo ukianza appeared first on HabariLeo.
WAKATI jana wanafunzi kote nchini wakianza muhula mpya wa masomo, hali ni tofauti kwa Shule ya Sekondari ya G.G Shulua iliyopo Kibamba wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam iliyofungwa ghafla siku mbili kabla ya shule kufunguliwa.
Shule hiyo yenye usajili namba S 4079, ilikuwa na wanafunzi takribani 60. Hata hivyo, imelazimika kuwahamishia shule za sekondari Fabcast iliyopo Kibaha na Emi.
Mmoja wa wazazi waliozungumza na HabariLEO jana, Kanali mstaafu Geofrey Mmbaga alisema Jumamosi saa 1:00 usiku alipigiwa simu na Mkuu wa shule hiyo, Mathew Shambula na kumueleza kuwa asimpeleke mtoto wake shuleni hapo kwa sababu imefungwa.
Alisema mwalimu alimshauri ampeleke mtoto wake (Natalia) shule nyingine au katika shule ambazo wamezichagua.
“Nilistaajabu kupewa taarifa hizi usiku tena kwa mdomo bila barua, wamefunga shule bila kutupa taarifa kwa sababu gani?” alihoji Kanali mstaafu Mmbaga.
Alieleza kuwa baada ya kuhoji kwa kina kwa mkuu huyo wa shule, aliambiwa kuwa uamuzi huo umetolewa katika kikao kilichoketi Ijumaa ambacho wajumbe wa bodi waliamua kufutwa kwenye usajili shule hiyo.
Alisisitiza kuwa uongozi huo haukuwatendea haki kwani waliamini watoto wao wataendelea na masomo, badala yake wanahangaika kutafuta shule nyingine wakati ambao hawakutarajia.
Akielezea sababu za kufungwa kwa shule hiyo, Mwalimu Shambula alikiri kutoa notisi ya muda mfupi kwa wazazi kutowapeleka shuleni hapo kutokana na uamuzi wa bodi ya wakurugenzi wa shule hiyo uliotolewa Januari 10, mwaka huu.
Mwalimu Shambula alisema ufungaji wa shule hiyo umefuata taratibu na sheria ya elimu kwa kuhakikisha wanagharamia uhamishaji wa wanafunzi wote.
“Sababu za kufunga shule hii ni mgogoro wa umiliki kati ya familia, mapato machache ambayo yanachangia kushindwa kujiendesha ikiwemo kulipa kodi, kulipa mishahara na gharama nyingine,” alifafanua Shambula.
Alifafanua kuwa shule ilikuwa na wanafunzi chini ya 60 wa kidato cha kwanza hadi cha nne pamoja na walimu saba na kwamba wakurugenzi walikuwa wanatumia fedha zao kwenye uendeshaji wa shule hiyo.
“Kuhusu mgogoro ni kati ya ndugu wawili (mjomba na mpwa wake) ambapo mjomba alitoa ardhi na kumpa mpwa wake kwenda kusajili shule na kuingiza jina lake kwenye usajili,” alidai mkuu huyo wa shule.
Aliongeza kuwa, “Huyo mpwa wake alifahamu kuwa hakuwa mmiliki wa shule lakini alijipenyeza kutokana na kuaminiwa na mjomba wake hivyo shule ikawa na wamiliki wawili.”
Mwalimu Shambula alidai waliandika barua kuhusu kubadilisha umiliki lakini ilishindikana kutokana na mpwa huyo kukataa kuukana umiliki wa shule hiyo.
“Maamuzi ya bodi yaliyoamriwa si kubadilisha umiliki, bali pia kufuta usajili wa shule hii ambayo ilianza mwaka 2009. Tumeifahamisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhusu suala la kufunga shule,” alieleza.
Kadhalika, alieleza kuwa wanafunzi hao wamehamishwa katika shule ambazo gharama zake zinaendana na za shule hiyo, pia walizingatia ukaribu ili kutoathiri wazazi na wanafunzi hao.
Alikiri kwamba baadhi ya wazazi walilipa ada ya muhula huo na kwamba wanaporipoti shuleni hao huwapeleka shule walizowapangia pamoja na ada zao au wakichagua kuwapeleka shule tofauti watawarudishia ada.
“Wazazi wanaowaleta watoto kuripoti tunawaelekeza kuhusu shule ambazo tumezichagua kupeleka watoto wao, ikiwa hawataridhika basi wataamua waende wapi na kama amelipa ada na anataka kumpeleka shule nyingine, wanarudishiwa pesa yao,” alisisitiza.
The post Shule yafungwa ghafla muhula wa masomo ukianza appeared first on HabariLeo.