Sheria yaja elimu ya lazima miaka 10
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema serikali itawasilisha mabadiliko ya Sheria ya Elimu Na…
The post Sheria yaja elimu ya lazima miaka 10 appeared first on HabariLeo.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema serikali itawasilisha mabadiliko ya Sheria ya Elimu Na 25 ya 1978 ili kutungwa nyingine ambayo itatamka ni lazima mwanafunzi akae shuleni kwa miaka kumi.
Profesa Mkenda alisema hayo juzi mjini Morogoro akifungua warsha ya tathmini ya utekelezaji wa kazi mbalimbali za mradi wa Kulimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP-AEP) ambao unatekelezwa na Taasisi ya Elimu ya Watu wazima (TEWW).
Mkenda alisema kuanzishwa kwa SEQUIP na uboreshaji miundombinu ya elimu inasaidia wizara kutekeleza kikamilifu mitaala mipya.
Profesa Mkenda alisema mitaala mipya itakapotekelezwa kwa asilimia 100, shule ya msingi itaendeshwa kwa miaka sita na kwa elimu ya lazima itakuwa miaka 10.
“Hivi sasa elimu ya lazima ni miaka saba, hivyo itatoka miaka saba kwenda miaka 10, elimu ya msingi sasa itakuwa miaka sita na sekondari ya kati itakuwa miaka minne,” alifafanua Profesa Mkenda.
Waziri Profesa Mkenda alibainisha kwamba watakapokuwa wanatekeleza mitaala mipya kwa asilimia 100 hali hiyo ndivyo itakavyokuwa.
Waziri Profesa Mkenda alisema kwa upande wa shule ya msingi, waliokuwa darasa la tatu mwaka jana (2024), sasa wako darasa la nne (2025) na mwaka 2026 wataingia darasa la tano na mwaka 2027 wataingia darasa la sita.
“Na kwa sababu mtaala mpya ya elimu ya msingi ni miaka sita tu, wanafunzi wakifika darasa la sita watakuwa wamemaliza elimu ya msingi na hao ndio lazima waendelee kidato cha kwanza hadi cha nne kwa amri na kwa sheria,” alisema.
Profesa Mkenda alisema serikali kupitia wizara yake italazimika kubadilisha Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 na kuliweka hilo kisheria mwanafunzi akae shuleni kwa miaka 10.
Akitoa ufafanuzi na kueleza waliokuwa darasa la pili mwaka jana ambao hawakusoma mtaala mpya na sasa wameingia darasa la tatu, alisema nao watasoma na mtaala mpya.
Profesa Mkenda alisema kwa sasa wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza, darasa la pili, darasa la tatu na darasa la nne wote watakuwa kwenye mtaala mpya na hatimaye watafika hadi darasa la sita.
Alisema waliopo darasa la tano wenyewe lazima wasome hadi darasa la saba na kwa maana hiyo, mwaka 2027 kutakuwa na madarasa mawili yatakayomaliza shule kwa wakati mmoja .
“Mwaka 2027 kutakuwa na darasa la saba wakati huo na darasa la sita… tutakuwa na makundi mawili na iliwahi kutokea huko zamani miaka ya sitini, itatokea tena chini ya Serikali ya Awamu ya Sita,” alisema Profesa Mkenda.
Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda aliwaondoa hofu wazazi na walezi kuwa vitabu vya kufundishia mitaala mipya na ya zamani vipo vya kutosha na uwiano ni kitabu kimoja kwa watoto watatu.
“Kwa sasa tumeomba hadi magari ya jeshi yanatusaidia kusambaza vitabu hivyo ili kuhakikisha vinafika maeneo yote wanafunzi waweze kusoma kwa uwiano huo,” alisema.
The post Sheria yaja elimu ya lazima miaka 10 appeared first on HabariLeo.