Serikali yawezesha wabanguaji korosho kujiimarisha kiuchumi

Habari Leo
Published: May 13, 2025 08:53:28 EAT   |  News

SERIKALI inaendelea kuwainua wabanguaji wadogo wa zao la korosho nchini katika mazingira mbalimbali. Mazingira hayo ni pamoja na suala la masoko, uwekezaji wa viwanda na mengine ili kuongeza thamani ya mazao hayo. Inafanya hivyo kuhakikisha wabanguaji hao wanaendelea kusaidiwa hata kwa kupatiwa elimu ya namna bora ya kubangua na kusimamia ubora. Aidha, inafanya hivyo kuwawezesha …

SERIKALI inaendelea kuwainua wabanguaji wadogo wa zao la korosho nchini katika mazingira mbalimbali.

Mazingira hayo ni pamoja na suala la masoko, uwekezaji wa viwanda na mengine ili kuongeza thamani ya mazao hayo. Inafanya hivyo kuhakikisha wabanguaji hao wanaendelea kusaidiwa hata kwa kupatiwa elimu ya namna bora ya kubangua na kusimamia ubora.

Aidha, inafanya hivyo kuwawezesha kupata teknolojia bora zaidi na kupitia umoja wao, wapate mikopo kutoka taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Mikopo mingine ni ile ya asilimia 10 inayotolewa kutokana na mapato ya ndani ya kila halmashauri kwa vikundi vya wajasiliamali wakiwemo  wanawake (asilimia nne), vijana (asilimia nne) na watu wenye ulemavu (asilimia mbili) pamoja na taasisi nyingine.

HabariLEO limezungumza na baadhi ya wakulima na wabanguaji wa korosho mkoani Mtwara kufahamu namna jitihada hizo za serikali zinavyowanufaisha ikilinganishwa na ilivyokuwa awali. Mbanguaji na mkulima wa Mtaa wa Kiyangu, Manispaa ya Mtwara Mikindani katika Kikundi cha Jipange, Zainabu Saidi anasema kupitia kazi hiyo wanapata mafanikio mengi makubwa.

Anasema mafanikio hayo ni pamoja na kusomesha watoto, kulimisha mashamba ya mikorosho na mengine. “Tunashukuru biashara inafanyika na tunapata pesa kuendeshea majukumu ya kifamilia kwa sababu kwa siku biashara ikichanganya unaweza kupata Shilingi 50,000 na wakati mwingine mtu akapata Shilingi 30,000 kutegemea Mungu atavyokuwezesha siku hiyo,” anasema.

Kuhusu mazingira ya biashara, anasema awali ilikuwa ‘haijachanganya’ kwa kuwa ubanguaji ulikuwa ukifanywa na wajasiriamali wachache. Anasema kwa sasa mtandao umekuwa mkubwa kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kuboresha sekta hiyo na kuwawezesha wakulima wa korosho na wabanguaji kwa ujumla.

Naye Hafsa Husein ambaye ni mbanguaji wa korosho na mkazi wa Mtaa wa Ufukoni, anazungumzia suala la teknolojia. Anasema awali walikuwa wakifanya kazi hiyo ya kubangua korosho kupitia teknolojia ya zamami kama vile vijiti na mawe.

Hafsa ambaye kikundi chake kinachofanyia shughuli zake katika Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoani Mtwara anasema, “Tuna takribani miaka minane sasa; serikali imeweza kutuangalia kwa jicho la pekee hasa sisi wabanguaji wadogo maana tumewezeshwa vitendea kazi bora na vya kisasa kama vile mashine.”

Anaongeza: “Pia, tuliweza kubangua korosho kwa kipindi hicho tani 78,000 ndani ya miezi mitatu kupitia umoja wetu na tukaanza kupata masoko ya nje.”

Hafsa ambaye pia ni mwanakikundi wa Mikindani Food Processing anasema, “Serikali inaendelea na jitihada za kutupatia mafunzo mbalimbali wabanguaji wadogo ya namna tunavyopaswa kufanya kazi hii kwa tija na kwa ubora unaotakiwa ili tuendelee kukidhi viwango na mahitaji ya soko.”

Hata hivyo imebainika kuwa, korosho hizo zinauzwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo kwa wateja wakubwa na wadogo.

Kwamba, soko lao si tu kwa wateja wa mkoa huo pekee, bali hata nje ya mkoa katika mikoa kama Dar es Salaam na maeneo mengine. Mbanguaji mwingine mkazi wa Mtaa wa Lilungu ambaye ni mwanakikundi wa ‘Mama Vitu Super Cashewuts,’ Mwajuma Issa anasema licha ya mafanikio hayo, zipo changamoto kadhaa wanazokumbana nazo katika kazi hiyo.

Changamoto hizo anasema ni pamoja na mlolongo mrefu wanaposafirisha mzigo kwenda nje ya Mtwara.

“Mazingira haya yanatupa changamoto sisi wabanguaji wadogo kwa sababu unakuta kwa mfano, mtu ana kilo zake kumi tu za korosho, ili usafirishe kutoka hapa (Mtwara) kwenda Dar es Salaam, mlolongo unakuwa mwingi kwa hiyo suala hili linaturudisha nyuma wafanyabiashara wadogo hasa akina mama,” anasema Mwajuma.

Mwingne ni Zaibau Chivalavala. Huyu ni mkazi wa Mtaa wa Sokoni katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba. Anatoka katika kampuni ya Tanzania Delicious Cashews Ltd. Anasema katika tasnia hiyo wamehamasisha wakulima wenzao kushiriki kazi ya kubangua korosho na kufanikiwa kuwaingiza kazi hiyo muhimu kiuchumi.

“Kupitia tasnia hii, tumekuza ubanguaji nchini kupitia jitihada za serikali kwani tumekuwa tukiuza koroshoghafi pekee huko nyuma, lakini sasa tumeingia katika hatua ya kuuza korosho karanga kwa hiyo tumekuza mnyororo wa thamani katika mazao hayo ya korosho,” anasema.

Anaongeza: “Tulioanza zamani hii kazi tumepitia changamoto nyingi, lakini sasa tunajionea mafanikio ya uwepo wa viwanda vingi vya kubangua korosho.” “Hivi vimeanzishwa baada ya serikali kuona kuwa ni njia pekee na
muhimu kumkomboa mkulima wa korosho ili anufaike zaidi na kilimo chake,” anasema Zainabu.

Kuhusu bei, anasema awali walikuwa wanauza korosho-karanga nyeupe ambazo bado hazijaandaliwa kwa bei ya Sh 9,000 kwa kilo kutoka kwa mbaguaji, lakini sasa inauzwa kati Sh 15,000 mpaka Sh 18,000 na ikishaandaliwa inauzwa Sh 20,000 mpaka 22,000.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Jipange, Hawa Selemani anasema kikudi hicho kimeanzishwa mwaka 2009 na kina wanachama 31 na baadhi yao wanamiliki mashamba ya mikorosho.

“Tunashukuru kutokana hili zao la tunapata mahitaji yetu… Naishukuru serikali kwani hadi hapa tulipofikia mara nyingi tumekuwa tukipatiwa mafunzo kuhusu kazi hii kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo Bodi ya Korosho Tanzania (CBT),” anasema.