Samia ahimiza wanawake umuhimu elimu kwa watoto wa kike

Habari Leo
Published: Feb 21, 2025 14:06:54 EAT   |  Educational

Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wanawake waliobahatika kupata fursa ya elimu na kuwa viongozi kwenye…

The post Samia ahimiza wanawake umuhimu elimu kwa watoto wa kike appeared first on HabariLeo.

Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wanawake waliobahatika kupata fursa ya elimu na kuwa viongozi kwenye maeneo mbalimbali kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu ili kuongeza imani na amani kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.

Rais Dk Samia ametoa wito huo leo Februari 21 kwenye maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanza kwa Mafunzo ya Uongozi kwa Wanawake Tanzania (Female Future Program) sambamba na Mahafali ya Wahitimu wa Awamu ya 10 ya Mafunzo hayo na Mkutano wa 7 wa Uongozi, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Aidha, amewataka wahitimu hao kuwa chachu ya maendeleo katika jamii na kutumia elimu na stadi za uongozi walizopata kunufaisha jamii kwa ujumla.

Vilevile, Rais Dk Samia amewarai wanawake kudhihirisha ushupavu wa uongozi kwenye Mashirika na Taasisi mbalimbali na kuwataka kuwa wabunifu kwenye kazi zao na kuwa waaminifu katika kulipa kodi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa maisha ya mwananchi.

Pia, katika kuhakikisha ustawi wa jamii, amewahusia kuwa pamoja na elimu na nafasi za uongozi walizonazo, wasiache wajibu wao wa kijamii wa malezi na makuzi ya watoto ili kuwaepusha kujiingiza kwenye mienendo isiyofaa.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, Rais Dk Samia amewahamasisha wanawake wenye sifa na uwezo kujiandikisha kupiga kura na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali.

The post Samia ahimiza wanawake umuhimu elimu kwa watoto wa kike appeared first on HabariLeo.