Sababu upotevu wa mapato ya ndani Tanzania

UKUSANYAJI wa mapato ya ndani ni moja ya vipengele muhimu katika kufadhili Mipango ya Maendeleo Endelevu (SDG) namba17,…
The post Sababu upotevu wa mapato ya ndani Tanzania appeared first on HabariLeo.
UKUSANYAJI wa mapato ya ndani ni moja ya vipengele muhimu katika kufadhili Mipango ya Maendeleo Endelevu (SDG) namba17, katika kutoa huduma bora kwa umma, kuongeza usawa na uhimilivu wa uchumi.
Ukusanyaji wa mapato Tanzania unahusisha kodi, tozo, ushuru na fedha zinazotolewa na mashirika ya umma kwa serikali kama gawio.
Shirika lisilo la kiserikali la Policy Forum, limekuwa likifanya kazi ya kuboresha michakato ya sera ili kupunguza umaskini, kuongeza usawa na demokrasia.
Katika hilo, wamekuwa wakihakikisha masuala mbalimbali hususan haki kodi, ukusanyaji wa mapato na kuzuia utoroshwaji wa fedha, Tanzania iweze kunufaika kwa kutumia rasilimali zake.
Kwa mujibu wa Policy Forum, wanaeleza kuwa utulivu wa ndani ya nchi na uhamasishaji wa ukusanyaji wa mapato unatoa ishara kwamba nchi ina misingi ya uchumi imara hivyo kuvutia mtiririko wa rasilimali.
Pia wanaeleza kuwa utoroshaji wa fedha kwa lugha ya Kiingereza ‘Illicit Financial Flow (IFFs)’ ni moja ya vikwazo vikuu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani Tanzania licha ya kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kudhibiti vitendo hivyo.
Mwaka 2006, serikali ilitunga Sheria ya Kuzuia Utakatishaji fedha kifungu cha 12, miongoni mwa vipengele vinavyohusika na sheria hiyo ni endapo mtu yeyote atakayeficha ukweli na kuzuia upatikanaji wa ukweli kuhusu chanzo cha fedha, umiliki na anapopeleka fedha zake, anatafsiriwa kuwa ametakatisha fedha.
Vitendo vya utoroshaji wa fedha hapa nchini hufanyika kwa njia mbalimbalki ikiwemo upotoshaji wa thamani za miamala kwenye ankara au malipo, kutoa ankara nyingi kwa muamala unaofanana na kutolingana kwa wingi wa bidhaa zinazolipiwa ankara dhidi ya kiasi cha bidhaa halisi zinazosafirishwa.
Njia nyingine ni kutorosha fedha ni kuundwa kwa mfumo usio rasmi wa uhawilishaji thamani na kughushi ili kupotosha ubora, aina ya bidhaa au huduma ili kuchezea thamani ya uhawilishaji.
Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2023 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, katika mwaka 2023/24, serikali ilitarajia kukusanya na kutumia jumla ya Sh bilioni 44.388 kutoka vyanzo vya ndani na nje.
Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri yalitarajiwa kuwa Sh bilioni 31,381.0 wakati mapato ya kodi yalikadiriwa kuwa Sh bilioni 26,725.4 na yasiyo ya kodi kutoka wizara, idara zinazojitegemea, wakala na taasisi za serikali yalikadiriwa kuwa Sh bilioni 3,511.7 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri Sh bilioni 1,143.9.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa sababu za kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato ya ndani kumetajwa kutokana na baadhi ya walipakodi kutotoa risiti wakati wanapouza bidhaa zao, kuwepo kwa udanganyifu wa kuripoti mauzo kwa baadhi ya walipakod na uwepo wa mianya ya upotevu wa mapato hasa maeneo ya mipakani.
Vilevile, ufanisi mdogo wa mifumo inayotumika kukusanya ada na tozo za ardhi na baadhi ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kutowasilisha michango stahiki kwa wakati.
Kwa mujibu wa Global Financial Integrity ushahidi unaonesha kuwa nchi inapoteza takriban Dola za Marekani bilion 3.5 sawa na Sh…… kwa mwaka kutoka katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uziduaji kupitia njia tofauti tofautii za utoroshwaji fedha.
Aidha, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya mwaka 2022/23 ilibainisha kuwa changamoto ya kushindwa kukusanya mapato yasiyotokana na kodi kama ilivyopangwa imekuwa ikijirudia kwenye taasisi zilizopewa dhamana ya kukusanya mapato hayo.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa kwa mwaka 2021/22 kodi za pango kiasi cha Sh bilioni 13.1 hazikukusanywa na taasisi zilizopewa dhamana ya kukusanya kodi hizo.
‘’Mwaka 2020/21 sekta ya ardhi ilishindwa kukusanya Sh bilioni 77.5 na Halmashauri 121 zilikusanya mapato chini ya makadirio ya bajeti kwa kiasi cha Sh bilioni 83.13,’’ inaeleza ripoti hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wajibu, inayojihusisha na kukuza mazingira ya uwajibikaji wa umma nchini Tanzania, Ludovic Utouh, anasema kuwa ukusanyaji mdogo wa mapato ya serikali ni kiashiria cha vitendo vya rushwa na ukosefu wa umakini katika usimamizi wa mapato ya serikali ambavyo husababisha uwepo wa nakisi ya bajeti.
Anasema kutokana na hali hiyo, serikali hulazimika kukopa zaidi ili kukidhi mahitaji ya bajeti na wakati mwingine kusababisha ongezeko la kodi kwa wananchi ambalo limekuwa ni chanzo cha migogoro.
‘’Kuongezeka kwa mianya ya kuvuja kwa mapato kunasababisha uwepo wa viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu wa fedha za umma. Kukosekana kwa taarifa sahihi za mapato yaliyokusanywa, huisababishia serikali kushindwa kutoa huduma stahiki kwa wananchim,’’ anaeleza.
Utouh ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEIT), anasema kuwa upotevu wa mapato hufanyika pia katika sekta ya uziduaji kwani katika ripoti yao ya 14 imeonesha kuwa kati ya kampuni zilizolinganishwa kwa mwaka wa fedha 2021/22 kuna upotevu wa Sh milioni 402.4 sawa na asilimia 0.21.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kampuni za uziduaji ziliripoti malipo ya Sh bilioni 1.391 kwa serikali wakati mapato kutoka serikalini yalionesha kiasi cha Sh bilioni 1.909.
Mapato yaliyoripotiwa na serikali yalikuwa juu zaidi ya Sh milioni 517 ikilinganishwa na malipo yaliyoripotiwa na kampuni.
Utouh anasema baada ya marekebisho, malipo ya mwisho yaliyofanywa na kampuni yalikuwa Sh bilioni 1.878 wakati mapato ya mwisho yaliyopokelewa na serikali ni Sh bilioni 1.877na kusababisha tofauti ya Sh 402,411,069.73 sawa na asilimia 0.021.
‘’Makosa kama haya ya upotevu wa fedha yanaendelea kufanyika, tunahitaji uwazi katika malipo yanayofanywa na kampuni na serikali ili wananchi waone uwajibikaji,’’ anaeleza
Anasema kuwa utofauti wa fedha hizo unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo vitendo vya rushwa na kutokuwajibika ipasavyo kwa pande hizo kwa kuhakikisha wanaripoti kila muamala unaofanyika.
Anasema kuwa pamoja na kiasi cha fedha chini ya asilimia moja kutopelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), bado uchunguzi zaidi unahitajika ili kujua upotevu huo wa fedha unatokana na sababu zipi.
Kwa upande wake, Profesa Abel Kinyondo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Jiografia na Uchumi, anasema kuwa utoroshaji wa fedha ni chanzo kikuu cha upotevu wa mapato ya ndani hivyo ili kudhibiti ni vema kuongeza uwajibikaji, uwazi na usimamizi wa sheria.
Akizungumza katika semina ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na Policy Forum, Profesa Kinyondo anasema wakati mwingine deni la taifa linaweza kuathiri ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa sababu ni lazima lilipwe na mapato ya ndani ndio hutumika kulipa deni hilo ambalo kwa sasa limefikia Sh trilioni 98.
Pia anasema kuwa bunge ndilo lina nafasi ya juu ya kusimamia uwajibikaji kwa kuiwajibisha serikali pale panapotokea changamoto mbalimbali hususan upotevu wa mapato ya ndani hivyo, lihakikishe linasimamia wajibu wake, kusemea kero za wananchi na kutoa taarifa.
‘’Tunapobuni vyanzo mbalimbali vya kodi na ukusanyaji wa mapato ya ndani, tunahitaji uwajibikaji kutoka kwa kampuni, wafanyabiashara na serikali ili mapato yanayokusanywa yaonekane na yatumike kwa ajili ya maendeleo,’’ anaeleza Profesa Kinyondo
Hedrick Mapunda anasema uwajibikaji ni nguzo muhimu katika kujenga Tanzania tuitakayo kwa kuanzisha mifumo ya kudumu ya ufuatiliaji kwa kuweka mifumo thabiti ya kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya CAG, kuhakikisha kuwa hatua zinazochukuliwa zinawasilishwa kwa umma mara kwa mara.
Pia anasema kuwa ni muhimu kuunda programu maalum zinazoweza kutumiwa na wananchi kufuatilia matumizi ya fedha za umma na kuripoti ubadhirifu kwa urahisi.
‘’Kampeni za uhamasishaji kuhusu umuhimu wa uwajibikaji na athari za ubadhirifu zinapaswa kufanyika kitaifa ili kuelimisha wananchi na kuhimiza ushiriki wao katika kudai uwajibikaji,’’ anaeleza.
Pia anasema kuongeza uwazi, kutoa elimu, kuimarisha mifumo ya udhibiti, na kutumia teknolojia ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo, kila mwananchi anapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa kudai uwajibikaji.
‘’Tunapochukua hatua hizi, tutaweza kujenga taifa lenye haki, usawa, na maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo,’’ anasisitiza.
Aidha, moja ya nukuu za Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alisema kuwa “Mapato ni damu ya maendeleo. Bila ya mapato hakuna maendeleo. Nchi maskini siyo maskini kwa sababu hazina maliasili, zana, au watu hodari. Zipo nchi tajiri duniani ambazo hazina haya pia. Maskini ni maskini kwa sababu mapato yake ni madogo” akimaanisha kuwa mapato yanapaswa kukusanywa kwa ufanisi ili kuwezesha maendeleo endelevu na kutoa huduma bora kwa wananchi.
The post Sababu upotevu wa mapato ya ndani Tanzania appeared first on HabariLeo.