RC amtaja Msuya kwa unyenyekevu, uchapakazi

Habari Leo
Published: May 13, 2025 06:01:54 EAT   |  News

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema taifa litamkumbuka Cleopa Msuya kwa unyenyekevu, uchapakazi na hakuwa na majivuno. Babu alisema hayo wilayani Mwanga jana wakati akitoa salamu za mkoa kwenye misa ya kuaga mwili wa Cleopa Msuya aliyekuwa Mbunge wa Kwanza wa Mwanga. Alisema Mkoa wa Kilimanjaro utamkumbuka kwa kuupigania katika maeneo mbalimbali ya …

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema taifa litamkumbuka Cleopa Msuya kwa unyenyekevu, uchapakazi na hakuwa na majivuno.

Babu alisema hayo wilayani Mwanga jana wakati akitoa salamu za mkoa kwenye misa ya kuaga mwili wa Cleopa Msuya aliyekuwa Mbunge wa Kwanza wa Mwanga.

Alisema Mkoa wa Kilimanjaro utamkumbuka kwa kuupigania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo hasa katika Wilaya ya Mwanga.

Babu alisema Msuya alikuwa mnyenyekevu asiyekuwa na majivuno na mfuatiliaji wa mambo ya maendeleo.

“Sisi wengine tulipata bahati ya kukaa na Mzee Msuya, alipenda kufuatilia jambo mpaka ukamilifu wake, alithamini maisha ya kila mtu. Hakuwa na majivuno na mfuatiliaji wa masuala ya maendeleo,” alieleza Babu.

Alisema maendeleo ndani ya Mwanga yanaonesha uwezo na utashi wa Msuya katika kuwapigania wananchi wake na taifa kwa ujumla.

Aliongeza kuwa katika siku zake za mwisho alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan aukamilishe Mradi wa Maji wa Mwanga – Same – Korogwe ili wananchi wa Mwanga waondokane na adha ya maji.

Aliongeza kuwa Msuya alishiriki kikamilifu katika uzinduzi wa mradi huo ambako wananchi wa Mwanga na jirani zao Same wanapata maji safi.

“Serikali ya mkoa inaahidi kuwa yale yote aliyoahidi na kuyaelekeza itayatekeleza kwa ukamilifu mkubwa,” aliongeza Babu.

Aliwataka viongozi wa kitaifa kuiga mfano wa uzalendo aliokuwa nao Msuya kwa wananchi wake hali iliyomfanya kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wake.

Msuya aliyezaliwa Januari 4, 1931, alifariki dunia Mei 7, mwaka huu katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam kwa maradhi ya moyo na atazikwa leo kijijini kwao alikozaliwa Chomvu, Kata ya Chomvu Usangi wilayani Mwanga.

Alikuwa Mbunge wa Kwanza wa Mwanga kuanzia mwaka 1980 hadi alipostaafu Oktoba 29, 2000.