Rais Samia kuzindua jengo la Mahakama ya Tanzania kesho

Habari Leo
Published: Apr 04, 2025 10:32:21 EAT   |  News

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua jengo la makao makuu ya Mahakama ya Tanzania kesho. Mtendaji Mkuu wa…

The post Rais Samia kuzindua jengo la Mahakama ya Tanzania kesho appeared first on HabariLeo.

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua jengo la makao makuu ya Mahakama ya Tanzania kesho.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante ole Gabriel amesema jengo hilo ni sehemu ya miradi ya ujenzi inayojumuisha majengo matatu zikiwemo nyumba za majaji 48 za Iyumbu, Dodoma.

Alitaja mingine ni jengo hilo na jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Kwa mujibu Profesa Ole Gabriel majengo hayo yamegharimu Sh bilioni 416.46.

Profesa Ole Gabriel ameishukuru serikali kutokana na uwekezaji inayofanya kwa upande wa mahakama ambao unasababisha kuboresha miundombinu mbalimbali ya mahakama.

“Naipongeza sana serikali kutokana na kazi kubwa wanayofanya na kusababisha uwekezaji mkubwa unaofanywa na mahakama wa kuboresha miundombinu mbalimbali ya majengo,” alisema.

Akizungumzia kuhusiana na changamoto za nyumba za majaji, Profesa Ole Gabriel alisema kwa upande wa Dodoma wameshakamilisha, imebaki kukamilisha changamoto ya nyumba za mahakimu katika mikoa mbalimbali nchini.

Hata hivyo alizungumzia kuhusiana na upekee wa jengo hilo, alisema litakuwa likifanya kazi nyingi kwa kutumia masuala ya Tehama ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI) ambazo zitasaidia kurahisisha utendaji wa kazi za kimahakama.

Alisema pia, katika jengo hilo kutakuwa na uwanja wa ndege za helkopta ambazo zitakuwa zikitumika na majaji katika shughuli za kimahakama, ikiwemo uwezekano wa majaji kusikiliza kesi katika mikoa tofauti kwa siku moja.

 

The post Rais Samia kuzindua jengo la Mahakama ya Tanzania kesho appeared first on HabariLeo.