Qatar yatangaza ajira 400 madereva mabasi, malori

QATAR kupitia Kampuni ya Mowasalat imetangaza fursa za ajira kwa Watanzania 400 wenye fani ya udereva. Taasisi ya…
The post Qatar yatangaza ajira 400 madereva mabasi, malori appeared first on HabariLeo.
QATAR kupitia Kampuni ya Mowasalat imetangaza fursa za ajira kwa Watanzania 400 wenye fani ya udereva.
Taasisi ya Benjamin Mkapa kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X, imetangaza madereva wanaohitajika huko ni wa mabasi na malori.
Akizungumza na HabariLEO jana Dar es Salaam, Mkuu wa Programu ya Ajira za Kimataifa katika taasisi hiyo, Evelyine Jackson alisema ni mara ya kwanza Qatar inatoa fursa hiyo kwa Tanzania.
“Awali walikuwa wakitafuta wafanyakazi kutoka mataifa kama Ufilipino, Kenya na mataifa mengine, ila sasa wamevutiwa na nguvukazi kutoka Tanzania,” alisema Evelyine.
Alisema kupitia kampuni yao tanzu inayohusika na masuala ya ajira ya Imarahorizon, wamepata zabuni ya kutangaza, kufanya mchujo na usaili wa wafanyakazi hao 400 madereva ambao watagharamiwa kufika kwenye vituo vyao vya kazi.
Evelyine alisema kutokana na kukua kwa diplomasia baina ya mataifa hayo mawili yaani Tanzania na Qatar, na kupata mrejesho wa jinsi Watanzania wanavyofanya kazi vizuri katika nchi za ughaibuni hususani Oman na nchi nyingine za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), walishawishika na wao kuja.
“Sisi si mara ya kwanza kuwaunganisha na ajira Watanzania, taasisi yetu inashughulika na masuala ya afya na tulipata ombi la kupeleka wauguzi zaidi ya 500 Saudi Arabia, wanafanya kazi vizuri hao wamekuwa mabalozi wetu na hata kampuni iliyotuomba wanaendelea kutusemea vizuri Watanzania ndio maana hata hawa wamekuja,” alifafanua Evelyine.
Alisema katika fursa hizo 400 za madereva wanapaswa kuomba nafasi hizo kupitia mfumo wa mtandao uliowekwa kwenye tovuti ya taasisi hiyo ya Mkapa na kuwa sifa kuu nne za mwombaji ni uzoefu wa udereva kwa miaka miwili hadi mitatu.
Pia, awe na leseni ya udereva wa kuendesha mabasi ya abiria na malori ya mizigo, awe anajua kuandika na kuzungumza vizuri Lugha ya Kiingereza na awe na umri wa kati ya miaka 25 hadi 45.
Evelyine aliwataka Watanzania wenye sifa hizo watume maombi yao kabla ya mwisho wa kupokea maombi ambao ni Aprili 15, mwaka huu.
“Watanzania wasiogope hii ni fursa ya kweli, na si uzushi kama baadhi ya watu wanasambaza, lakini pia hakuna biashara ya kusafirisha binadamu… hili ni tangazo la kweli la fursa za ajira na sisi ndio wahusika, hivyo niwasihi wenye uhitaji wajitokeze,” alisema Evelyine.
Alisema serikali ina taarifa za fursa hiyo na Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar pamoja na taasisi za serikali zinazohusika na ajira na vibali vya kazi ndani na nje ya nchi.
Akitaja faida kwa watakaopata fursa hiyo ni kuwa watalipiwa viza, nauli ya ndege na gharama zote muhimu, mafunzo ya kitaalamu ya udereva, malazi, matibabu na bima ya maisha.
“Katika kufanya maombi ya fursa hii hakuna gharama zozote za malipo, hivyo Watanzania msikubali kutapeliwa ombeni bure kwa kufuata maelekezo, kisha usaili utafanywa na watakaopata watajulishwa,” alisema Evelyine
The post Qatar yatangaza ajira 400 madereva mabasi, malori appeared first on HabariLeo.