Oscar apewa mwongozo wa maadili

: MSANII na mwanahabari maarufu, OscarOscar, amepewa Mwongozo wa Maadili katika Kazi za Sanaa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kufuatia mjadala ulioibuka kuhusu wimbo wake mpya, "Mniombee".
DAR-ES-SALAAM : MSANII na mwanahabari maarufu, OscarOscar, amepewa Mwongozo wa Maadili katika Kazi za Sanaa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kufuatia mjadala ulioibuka kuhusu wimbo wake mpya, “Mniombee”, ambao umetafsiriwa na baadhi ya wadau kuwa hauna maadili.
Katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi za BASATA jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dkt. Kedmon Mapana, alimkabidhi Oscar mwongozo huo na kusisitiza wajibu wa wasanii kuzingatia maadili na weledi wanapotekeleza kazi zao za kisanaa.
“Wasanii wanapaswa kutumia Mwongozo huu kama rejea ya kila siku ili kuhakikisha kazi zao zinaakisi maadili ya Kitanzania,” amesema Dkt. Mapana.
Pia ameongeza kuwa wimbo wa Osca Osca unaruhusiwa kupigwa usiku kuanzia saa 6 watoto wakiwa wamelala na sio mchana. Tukio hili limejiri siku moja tu baada ya Oscar kunukuliwa na vyombo vya habari akisema, “hip hop ya Tanzania haina maudhui, nimekuja kuirudisha,” kauli iliyozua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Oscar anatarajiwa kuwa mfano wa msanii anayeendeleza ubunifu, ujumbe wenye maudhui, na kuzingatia misingi ya maadili katika kazi za sanaa, huku wadau wakisubiri kwa hamu kuona mwelekeo mpya atakaochukua.
SOMA: Basata yamfungia Babu wa Tiktok