Nyuki; huzaliwa hadi kufa bila mapenzi

Habari Leo
Published: May 23, 2025 08:24:21 EAT   |  Travel

AKIWA Dodoma Mei 17, 2025 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana alitoa taarifa kuhusu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Nyuki Dunia. Akasema maadhimisho hayo ni sehemu ya uzingatiwaji wa Azimio la Bazara Kuu la Umoja wa Mataifa kutambua umuhimu na mchango wa nyuki katika maisha ya …

AKIWA Dodoma Mei 17, 2025 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana alitoa taarifa kuhusu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Nyuki Dunia.

Akasema maadhimisho hayo ni sehemu ya uzingatiwaji wa Azimio la Bazara Kuu la Umoja wa Mataifa kutambua umuhimu na mchango wa nyuki katika maisha ya mwanadamu.

“Sote tunatambua kuwa nyuki na wadudu wengine wachavushaji wana mchango mkubwa katika usalama wa chakula, pamoja na uhifadhi bioanuai na asilimia 80 ya mazao yote ya chakula hutegemea kuchavushwa na mdudu nyuki,”anasema Dk Chana.

Ndipo Mei 20, 2025 wakati akifunga Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika kitaifa Chinangali Dodoma, Majaliwa anawataka Watanzania kuendelea kutunza na kuhifadhi nyuki. Anasema hilo litasaidia kuwa na taifa lenye uhakika wa chakula na uchumi imara kwa kuwa takribani asilimia 80 ya mimea ya chakula  inayozalishwa duniani huchavushwa na nyuki.

Majaliwa pia anaripotiwa kuzindua Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki kwa Tanzania Iliyo Bora (Achia
Shoka, Kamata Mzinga) utakaoleta mageuzi makubwa katika sekta nyuki.

Anatoa mwito kwa wadau wa masuala ya nyuki kushirikiana na Serikali kuwezesha utekelezaji wa mpango huo. “Nyuki wana umuhimu mkubwa katika ustawi wa maisha ya binadamu, hususani katika uchavushaji wa mimea, uzalishaji wa chakula, uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu,” anasema.

Kupitia maadhimisho hayo, Majaliwa anasema jamii hukumbushwa umuhimu wa kipekee wa nyuki katika mnyororo wa maisha na umuhimu wa kuwalinda dhidi ya changamoto mbalimbali kama uharibifu wa mazingira, matumizi ya viuatilifu hatarishi, mabadiliko ya tabianchi na magonjwa.

Inaelezwa kuwa, Tanzania inazalisha tani 34,000 za asali na tani 1,918 za nta. Kwamba, kiwago hicho kinaiweka nchi katika ramani ya dunia kwa kuwa ya kwanza kwa uzalishaji wa asali kwa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nchi ya pili kwa Afrika na ya 14 duniani.

Dk Chana anasema mpango huo unalenga kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali kutoka tani 34,861 za sasa hadi kufikia tani 75,000 ifikapo Juni, 2035 na kuongeza mauzo ya mazao ya nyuki katika masoko ya kikanda na kimataifa. “Aidha, kupitia mpango huo takribani ajira mpya 43,055 zinatarajiwa kuzalishwa hasa kwa vijana na wanawake.”

Maisha ya nyuki

Licha ya kuwa na faida lukuki katika maisha ya binadamu na mifumo ya kiikolojia, nyuki anatajwa na vyanzo mbalimbali kuwa anapozaliwa hadi kufa hajihusishi na suala la mapenzi isipokuwa majike wanaochaguliwa rasmi na kuandaliwa hadi kuwa malkia pamoja na dume mmoja ambaye baada ya ‘kumfikia’ malkia, hiyo ndiyo huwa siku yake ya mwisho duniani.

Kimsingi, nyuki ni wadudu wadogo wanaosifika kwa uchevushaji wa maua katika mimea mbalimbali na huchangia katika uwepo wa mimea inayotupatia hewa safi pamoja na chakula. Nyuki hutegemea chakula chao kutoka katika nta zinazopatikana katika maua ya mimea. Maisha ya nyuki yana muundo wa kijamii na kazi zao zimegawanywa kati ya malkia, wafanyakazi na madume.

Kwa mujibu wa makala iliyoandikwa katika tovuti ya https://wildlifetanzania.co.tz chini ya kichwa cha habari: ‘Mfahamu Nyuki na Umuhimu Wake Kiuchumi na Kiikolojia,’ jukumu kuu la malkia ni kutaga mayai. Makala inasema malkia wa nyuki anaweza kutaga maelfu ya mayai kila siku na mayai hayo ndiyo huzalisha wafanyakazi, nyuki wa kiume (dume), au malkia wengine wa nyuki.

“Malkia wa nyuki ni muhimu sana katika kuhakikisha kuendelea kwa koloni. Kwa kuzalisha mayai mengi, anahakikisha kuwepo kwa idadi ya kutosha ya nyuki wa kufanya kazi na kuimarisha koloni dhidi ya hatari za kufa kwa malkia au vifo vya nyuki wengine wazee,” tovuti inaandika. Inaongeza: “…Bila malkia, koloni litapoteza uwezo wake wa kuzalisha nyuki wapya na hatimaye kuathiriwa katika utendaji wake.”

Kuhusu nyuki dume na majukumu yake, makala inasema ni kuzalisha kwa kurutubisha malkia. “Wao huzaliwa na kazi ya kuzaliana na malkia wa nyuki. Hata hivyo, nyuki wa kiume hawawezi kufanya kazi zinazohusiana na ujenzi wa sega, ulinzi wa koloni, kuvuna chakula au kuchukua majukumu ya kawaida ya nyuki wa kike.” inasema.

Kwamba, nyuki wafanyakazi wao wana majukumu makubwa ya kukusanya chakula. “Nyuki wa kike huondoka kwenye mzinga ili kukusanya nekta, poleni na maji. Hupaa umbali mrefu na kutembelea maua mengi, wakikusanya rasilimali za chakula kwa ajili ya kundi la nyuki.”

Kazi nyingine ni uchavushaji wa mimea. Makala inasema, “Wakati wanakusanya nekta, nyuki wa kike kwa bahati huhamisha poleni kutoka ua hadi ua, wakisaidia katika uchavushaji wa mimea.” “Mchakato huu ni muhimu kwa uzazi wa mimea na uzalishaji wa matunda na mbegu. Hivyo basi kutoweka kwa nyuki ni kutoweka kwa maisha ya mimea pamoja na wanyama, ikiwemo binadamu.”

Kwa mujibu wa makala hiyo iliyoandikwa na Leon Hermenegild na kuhaririwa na Hillary Mrosso, mambo ya kushangaza kuhusu nyuki ni pamoja na kwamba, takribani theluthi moja ya chakula cha binadamu ni matokeo ya shughuli za nyuki wa asali.

Inaandika, “Katika kipindi cha maisha yao wiki 6-8, nyuki wa kike hufanya safari sawa na umbali wa mara 1½ ya mzunguko wa dunia na malkia anayefanya kazi kwa ufanisi anaweza kutaga mayaiya hadi 2,500 kwa siku.”
Inalezwa pia kuwa, nyuki wa asali hawazaliwi wakijua namna ya kutengeneza asali, bali hufundishwa na nyuki wazee kwenye mzinga. Makala inasema, “Nyuki dume hufa baada ya kujamiiana na malkia…”

Tovuti ya nyukitz.blogspot.com/p/hudumazetu.html inasema, “Nyuki wafanyakazi ni wakazi wengi wa mzinga na wote ni wa kike. Ni hao wanaofanya kazi zote kama kukusanya mbelewele, kusafisha mzinga, kutengeneza nta,
kujenga sega na hata kumlisha malkia na wadogo (nyuki).”

Inaongeza: “Nyuki dume ni wachache na kazi yao ya pekee ni kuzaa na malkia, baadaye wanafukuzwa kwenye mzinga na hawapewi chakula tena…” Makala ya ‘Nyuki Dume Akijamiiana na Malkia Anakufa’ katika globalpublishers.co.tz ya Juni 29, 2023 inaelezea mchakato wa uzazi wa nyuki.

Inasema, “Tafiti za kisayansi kuhusu viumbe hai zinaeleza kuwa, malkia wa nyuki ambaye hajawahi kukutana na dume (bikra) akiwa tayari kupata kizazi huhitaji dume. “Hupaa kuelekea sehemu yalipo madume, hapo hukutana na dume la kwanza ambalo akijamiiana nalo, sehemu za siri za dume hilo hubaki kwa malkia ili kurutubisha mayai ya malkia.”

Anasema kitendo cha sehemu za siri za dume kubaki kwa malkia husababisha tumbo la dume huyo kupasuka na kufa muda mfupi baada ya kujamiiana na malkia. “Baadaye huja dume lingine ambalo nalo huzitoa sehemu za siri za dume la kwanza kisha naye kumpanda malkia, vivyo hivyo na kwa wengine watakaofuata… Malkia anao uwezo wa kujamiiana na madume 7 hadi 10.

“Nyuki malkia anao uwezo wa kutunza mbegu za kiume zaidi ya milioni 100 kwenye mirija yake ya uzazi.” Makala hiyo imeandika, “Ni mayai milioni 5 mpaka milioni 6 pekee ndiyo huyatunza kwenye ‘spermatheca’ (mfuko wa mayai baada ya kujamiiana) na haya hutumika kurutubisha mayai yake polepole (kwa awamu) na kupata watoto katika maisha yake yaliyosalia.”

Chanzo kinasema mayai yaliyorutubishwa hutoa nyuki malkia na wafanyakazi wa kike, mayai ambayo hayajarutubishwa hutoa madume kwa ajili ya kujamiiana na malkia pekee ambao hawawezi hata kula mpaka wapate msaada wa kulishwa.

Malkia wapya (atakaowazaa) nao hukutana na madume, hupata watoto na kutengeneza makoloni yao. Nyuki wafanyakazi wa kike hawajamiiani, lakini wanao uwezo wa kutaga mayai ambayo hayajarutubishwa na kutoa nyuki dume.

Chanzo hicho mtandaoni kinasimulia kikisema baada ya malkia kutaga mayai yake, nyuki wafanyakazi wanao uwezo wa kuhisi na kutambua hivyo, huyazungushia mayai hayo mafuta kuyalinda (kuyakinga dhidi ya maadui) lakini pia ni chakula kwa malkia na viumbe hao baada ya kuzaliwa.

Kinaandika, “Mayai yatakayotoa nyuki wa kiume na wafanyakazi huzungushiwa mafuta ya kawaida, lakini yale yatakayotoa malkia huzungushiwa mafuta maalumu. Malkia anahitaji siku 16 tu kukomaa, majike (wafanyakazi) huhitaji siku 21 na madume huhitaji siku 24 tu.”

Kimsingi, nyuki ni muhimu kwa utunzaji wa mazingira. Kupotea kwa aina za nyuki kunaweza kusababisha athari kubwa kwa ikolojia na mifumo mingine ya viumbe. Kwa hiyo, kwa kuwalinda na kuwahifadhi nyuki, tunahakikisha
kuwa tunadumisha usawa na utajiri wa viumbe hai duniani.