Ngorongoro yavuna bil 694/ utalii miaka minne

MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imevuna Sh bilioni 694 zilizotokana na kuingiza watalii milioni 2.9 kati ya…
The post Ngorongoro yavuna bil 694/ utalii miaka minne appeared first on HabariLeo.
MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imevuna Sh bilioni 694 zilizotokana na kuingiza watalii milioni 2.9 kati ya Julai 2021 na Februari 2025.
Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Dk Elirehema Dorie alisema hayo Dodoma jana akieleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika eneo la utalii na uhifadhi ndani ya miaka minne tangu mwaka 2021 mpaka sasa.
Dk Dorie alisema katika mwaka wa fedha 2021/2022 walipokea idadi ya watalii 425,386 wakiwemo wa nje 228,810 na wa ndani wakiwa ni 196,576. Alisema mapato yaliyokusanywa kwa muda huo ni Sh bilioni 91.13.
“Hifadhi ya Ngorongoro ni moja ya maeneo yanayotembelewa na watalii wengi nchini Tanzania kutokana na vivutio vyake vya kipekee, vikiwemo mandhari ya kuvutia, wanyamapori wengi na historia ya kipekee ya kiutamaduni na kiakiolojia. Hali hii imepelekea hifadhi hii kuwa moja ya vivutio vinavyochangia asilimia kubwa ya watalii wanaokuja nchini,” alisema.
Dk Dorie aliongeza kuwa katika mwaka 2022/2023, idadi ya watalii walikuwa 752,232 na watalii wa nje ni 458,351 huku wa ndani wakiwa 293,881 na kiwango cha makusanyo kikiwa ni Sh bilioni 171.257.
Katika kipindi cha 2023/2024, Dk Dorie alisema idadi ya watalii nchini ni 908,627 ambao wa nje ni 553,875 na wa ndani wakiwa 354,752 na wakachangia mapato Sh bilioni 219.547.
Kwa mwaka huu wa fedha tangu Julai 2024 hadi Februari 2025, idadi ya watalii ni 830,295. Watalii wa nje ni 509,610, wa ndani 320,685 na wameingiza Sh bilioni 212.
Kwa 2024/2025, mwenendo unaonesha mamlaka itapata watalii zaidi ya milioni moja na mapato zaidi ya lengo ambalo iliweka ambalo ni kukusanya bilioni 230. Hadi sasa, katika mapato hayo, imeshakusanya asilimia 92.
Kwa mujibu wa Dk Dorie, takwimu hizo zinaonesha kuwa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu za The Tanzania: Royal Tour na Amazing Tanzania zimechangia kutangaza nchi na kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vya utalii.
Mambo mengine yaliyochangia ongezeko ni pamoja na mikakati ya shirika pamoja na ushirikiano kati ya sekta binafsi na mamlaka za utalii.
Wakati huo huo, Dk Dorie alitangaza mikakati sita ya kuimarisha sekta ya utalii ambazo ni matumizi ya teknolojia ya kidijiti kuimarisha mitandao ya kijamii na tovuti rasmi kwa maudhui bora na mfumo wa kuhifadhi tiketi mtandaoni.
“Mikakati mingine ni kutumia teknolojia ya Livestreaming kuonesha vivutio vya utalii, kutengeneza kampeni maalumu za kidigitali kwa masoko mbalimbali, ushirikiano na wadau wa utalii, kushirikiana na mashirika ya usafiri, hoteli na kampuni za watalii na kushiriki maonyesho ya kimataifa kama WTM London na ITB Berlin,” aliongeza Dk Dorie.
The post Ngorongoro yavuna bil 694/ utalii miaka minne appeared first on HabariLeo.