NFRA yatoa uhakika upatikanaji sukari

WAKALA ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA) umesema umejipanga vizuri kukabiliana na upungufu wa sukari nchini endapo…
The post NFRA yatoa uhakika upatikanaji sukari appeared first on HabariLeo.
WAKALA ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA) umesema umejipanga vizuri kukabiliana na upungufu wa sukari nchini endapo kutajitokeza upungufu wa bidhaa hiyo kwani serikali imeshatoa kibali kwao kuagiza na kusambaza sukari.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Dk Andrew Komba amesema
imepewa jukumu la ununuzi wa sukari nje kwa ajili ya kutosheleza soko la ndani uhaba utakapojitokeza kwa lengo la
kuwa na akiba ya kutosha kwa kipindi cha miezi miwili kama sheria ya sukari inavyosema.
Sheria ya sukari inasema, “Endapo NFRA itagundua kuna uhaba wa sukari itatoa sukari yake iliyoihifadhi na
kuiingiza sokoni.”
Dk Komba naye amesema, “Lakini pia endapo mojawapo ya kiwanda au viwanda vyote vikashindwa kuzalisha, basi
NFRA itatoa sukari yake iliyoiagiza na kuiingiza sokoni.”
Dk Komba alibainisha kwamba Bunge la Tanzania lilipitisha sheria hiyo na kuipa nguvu taasisi hiyo kuwa na sukari ya kutosha muda wote na si kusubiri mpaka kunapokuwa na uhaba wa bidhaa hiyo muhimu.
“Malengo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona Watanzania wanapata mahitaji muhimu na kuhakikisha uwepo kwa akiba ya chakula cha kutosha ikiwemo sukari kwa usalama wa nchi,” ameeleza mtendaji huyo wa NFRA.
Amesema ndiyo maana baada ya kujengewa uwezo wa kutosha na serikali, NFRA imeweza kuwa na akiba ya kutosha
ya chakula ikiwemo sukari katika kukabiliana na upungufu wowote utakaojitokeza.
Dk Komba amesema kwa upande wa nafaka, wakala umehifadhi akiba ya kutosha ya chakula cha ziada na kuuza nje ya nchi.
Alisema serikali imeipa taasisi yake mamlaka ya ununuzi na kuhifadhi sukari kutokana na changamoto ya uhaba wa bidhaa hiyo kujitokeza mara kwa mara miaka iliyopita na kuleta usumbufu kwa wananchi.
Mwaka jana, wakati Rais Samia alipokuwa ziarani Morogoro, alifungua Kiwanda cha Sukari cha Mkulanzi kinachomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza.
Amesema lengo la uwepo wa kiwanda hicho ni kuongeza kiasi cha uzalishaji sukari nchini.
Wakati wa ziara hiyo, Rais Samia alisema kati ya Machi mpaka Mei (mwaka jana), kulikuwa na upungufu wa sukari, hivyo serikali iliagiza sukari nje ya kutosha na kuwezesha bei yake kushuka ili kuwasadia wananchi kuipata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.
Pamoja na hayo, Dk Komba amesema serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ilisema katika kukabiliana na upungufu wa sukari uliokuwa unajitokeza, ipo tayari kufanya kazi na taasisi binafsi kuhakikisha sukari inapatikana kwa uhakika nchini na kuwataka wafanyabiashara wawe waaminifu na wasipandishe bei ya sukari.
Viwanda vinavyozalisha sukari nchini ni pamoja na Kilombero, Mtibwa, Bagamoyo, TPC Limited na Kiwanda cha
Serikali cha Mkulazi.
Katika hotuba yake ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 bungeni, Bashe alisema uzalishaji wa sukari umefikia tani 392,724 ikilinganishwa na tani 460,048.94 mwaka 2022/2023 sawa na asilimia 85.4 ya lengo la kuzalisha tani
445,000.
Aidha, Bashe alieleza uzalishaji wa miwa umefikia tani 4,215,555.27 ambazo zimezalisha sukari tani 392,724 sawa
na asilimia 88.25 ya lengo.
Vilevile, Bodi ya Sukari kwa kushirikiana na halmashauri imetambua maeneo yanayofaa kuwekeza katika miradi
mipya ya sukari ikiwamo Rufiji mkoani Pwani na Kasulu, Kigoma.
The post NFRA yatoa uhakika upatikanaji sukari appeared first on HabariLeo.