Murkomen alala kazini!

Taifa Leo
Published: Mar 24, 2025 15:12:08 EAT   |  News

SERIKALI inaonekana kuanza kulemewa na kibarua cha kudhibiti usalama kutokana na ongezeko la maafa yanayosababishwa na Al Shabaab katika maeneo ya Kaskazini Mashariki na majangili Kaskazini mwa Bonde la Ufa. Hii ni licha ya hakikisho la kila mara kutoka kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kwamba wizara yake imepiga hatua kubwa katika mpango wa kumaliza visa vya utovu wa usalama katika maeneo hayo. Katika kisa cha Jumapili, Machi 23, 2025, wahalifu wanaoshukiwa kuwa magaidi wa Al Shabaab waliwaua Polisi sita wa Akiba (NPR) na kuwajeruhi wengine wanne katika Kaunti ya Garissa. Shambulio hilo lilitokea katika eneo la Biyamadhow, Kaunti-ndogo ya Fafi, Jumapili asubuhi. Naibu Kamishna wa Kaunti-ndogo hiyo, Bw Naphtali Koojo alitaja kisa hicho cha saa kumi na moja unusu alfajiri kama cha kusikitisha. “Tumekuwa tukiendesha doria za usalama katika eneo hilo kwa ushirikiano na vikosi maalum vya walinda usalama lakini jambo lililotokea leo (jana - Jumapili) ni la kusikitisha mno,” Bw Koojo akaambia Taifa Leo kwa nji ya simu. Kulingana na kamishina huyo, wavamizi hao walishambulia kambi ya polisi hao kwa kutumia gruneti ya kurushwa kwa roketi (RPG) na kuwaua maafisa sita na kuwajeruhi wengine wanne. “Huwa tunaendesha doria za usalama kwa kutegemea habari za ujasusi zilizokusanywa. Wapiganaji hao wamo humu humu na huendesha operesheni zao kwa ustadi mno. Wao hushambulia na kujificha,” Bw Koojo akaeleza. Usaidizi wa kipekee kwa maafisa hao wa NPR ungetoka katika kambi ya usalama ya Yumbis iliyoko umbali wa kilomita 20 licha ya kwamba eneo hilo limetambuliwa kama lenye hatari ya kushuhudia mashambulio ya kigaidi. Haieleweki ni kwa nini NPR waliojihami kwa bunduki aina ya AK47 pekee ndio walioruhusiwa kukita kambi ya usalama katika eneo la Biyamadhow. “NPR hawana silaha za kisasa na hupokea malipo duni. Mtu aliye na bunduki ya AK47 hawezi kupigana na adui mwenye RPG na silaha nyingine za kisasa,” Ali Gubow, mkazi wa Garissa akasema. Matukio haya yanajiri siku chache tu baada ya Waziri Murkomen kutangaza kuwa operesheni Maliza Uhalifu imeleta utulivu katika maeneo ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki. Jumapili, tulipotafuta ufafanuzi kuhusu ongezeko la visa hivi vya uhalifu hasa ikizingatiwa kuwa vimeongezeka mno tangu Bw Murkomen ashike hatamu za wizara ya Usalama mnamo Desemba 2024, afisa mmoja wa ngazi ya juu aliyechelea kutajwa kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya wizara hiyo, alisema ipo mipango ya kuwawezesha zaidi polisi wa akiba katika maeneo yenye utovu mkubwa wa usalama. “Kuna mipango ya kuwapa polisi wa NPR silaha zenye nguvu zaidi ili kutekeleza kazi yao vyema na kujilinda dhidi ya wahalifu wenye silaha kali,” alisema afisa huyo. Polisi hao wa akiba wameuawa wiki moja baada ya kushambuliwa na kuuawa kwa mhudumu wa bodaboda na abiria wake katika Kaunti ya Mandera wiki jana. Aidha, kisa hicho cha  Jumapili kinatokea mwezi mmoja baada ya machifu watano kuvamiwa na kutekwa nyara na wahalifu waliodaiwa kuwa wanachama wa Al Shabaab katika eneo la Elwak, siku moja kabla ya ziara ya Rais William Ruto katika eneo hilo. Maafisa hao wa utawala walikuwa wakisafiri kwa gari aina ya Alton Wagon, nambari ya usajili KDC 128C wakielekea mjini Garissa mnamo Februari 4, kufanya maandalizi ya ziara ya Dkt Ruto. Walishambuliwa kati ya Bamba Owla na Ires Suki huku ikidaiwa kuwa walivukishwa mpaka hadi nchini Somalia na wahalifu hao. Licha ya Rais kutoa hakikisha la kujitolea kwa serikali yake kuwakomboa machifu hao, bado wanazuiliwa na mateka hao wanaitisha mamilioni ya pesa kama fidia kabla ya kuwaachilia. Wiki jana, machifu wawili waliuawa ndani ya saa 48 katika kaunti za Baringo na Samburu. Katika kisa cha kwanza, naibu chifu wa Kata-ndogo ya Kong’asisi, eneobunge la Tiaty, Baringo aliuawa na majangili wenye bunduki mnamo Ijumaa. Na mnamo Jumamosi Parara Lekiyierie ambaye alikuwa naibu wa chifu wa kata ndogo ya Pura, Samburu ya Kati aliuawa kwa kupigwa risasi na majangili waliovamia boma lake. Isitoshe, mapema wiki jana watu sita waliuawa na wengine wanane wakajeruhiwa na wezi wa mifugo katika kijiji cha Kelipoi, eneo la Baragoi, Samburu.