Mufti aombwa kuingilia migogoro ya ukewenza

Habari Leo
Published: Feb 16, 2025 11:19:48 EAT   |  Educational

OFISI ya Mufti imetakiwa kutoa elimu zaidi kwa wanaume kuhusu ndoa za wake zaidi ya mmoja kuepusha migogoro…

The post Mufti aombwa kuingilia migogoro ya ukewenza appeared first on HabariLeo.

OFISI ya Mufti imetakiwa kutoa elimu zaidi kwa wanaume kuhusu ndoa za wake zaidi ya mmoja kuepusha migogoro inayojitokeza mara kwa mara na kusababisha maafa makubwa.

Rai hiyo imetolewa kutokana na tukio la hivi karibuni la wanawake wawili, wake wenza kushambuliana na mmoja kumjeruhi mwenzake hadi kumsababishia ulemavu wa kudumu.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wawakilishi Wanawake (UWAWAZA), Dk Saada Mkuya Salum wakati akichangia hoja ya dharura iliyowasilishwa katika baraza hilo juzi, alisema changamoto za ukewenza zimeibua migogoro mingi sana.

Alisema suala la ukewenza lipo kwa mujibu wa sheria za Dini ya Kiislamu, lakini wahusika wakuu (wanaume) wanapaswa kupewa mafunzo zaidi ili kuishi katika mazingira hayo bila kusababisha malalamiko, chuki na baadaye ugomvi.

Alitoa mfano akisema kuwa wapo wanaume wenye wake zaidi ya mmoja lakini hawatimizi majukumu yao kwa mujibu wa sheria ya ndoa, ikiwemo matunzo na huduma muhimu.

Alisisitiza kuwa wakati umefika kwa ofisi ya mufti kutoa elimu zaidi kwa wanaume wanaoingia katika ndoa za wake wawili, ikiwemo kuwafanyia usaili kubaini kama kweli wana uwezo wa kumudu mazingira hayo, hususani kwa upande wa uchumi.

“Leo hii wapo wanaume wanaooa mke wa pili kwa kificho bila ya kuwepo kwa taarifa sahihi kwa wazazi au familia… hili halikubaliki, ndoa si siri,” alisema.

Hoja ya dharura kuhusu masuala ya ukewenza iliwasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Uwawaza, Mwantatu Mbaraka Khamis baada ya tukio la wakewenza kushambuliana.

Katika tukio hilo, Khadija Shaaban Ali (34) anadaiwa kumshambulia na kumsababishia majeraha makubwa mwilini mke mwenzake, Maimuna Said Suleiman (38).

Wakati huohuo, Mahakama Kuu ya Zanzibar imemnyima dhamana Khadija na kesi imeahirishwa hadi wiki ijayo. Anashitakiwa kwa kumjeruhi vibaya mke mwenzake, Maimuna.

Akisoma shitaka hilo, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Anuwar Saaduni alidai anashitakiwa kwa kosa la kujaribu kuua kinyume na sheria kifungu namba 193 (b) cha sheria namba 6/2018.

Saaduni alidai Februari 9, 2025 saa 7 mchana, Chukwani Unguja, Khadija anadaiwa kumchoma kisu kwenye paji la uso, shingoni na nyuma ya bega na kwenye vidole vya mikono, Maimuna ambaye ni mke mwenziwe.

Upande wa utetezi uliomba dhamana kwa mteja wao jambo ambalo upande wa mashitaka ulipinga.

Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Zanzibar chini ya Jaji Aziza Iddi Suwedim aliahirisha shauri hilo hadi Machi 12, 2025 kwa ajili ya uamuzi wa ombi la dhamana kwa mtuhumiwa.

The post Mufti aombwa kuingilia migogoro ya ukewenza appeared first on HabariLeo.