Mtakomaa! Bodi ya Arsenal yakataa ombi la kutimua Arteta baada ya msimu mwingine tasa

Taifa Leo
Published: May 09, 2025 05:55:41 EAT   |  Sports

BODI ya Arsenal haiko tayari kuachilia kocha Mikel Arteta licha ya mashabiki kusikitika kumaliza msimu mwingine bila taji.

Kuna sehemu ya mashabiki walio na imani kuwa Arsenal inaweza kufanya vizuri zaidi bila kocha huyo Mhispania ikiajiri kocha mwingine mtajika.

Mnamo Jumatano, Arsenal walibanduliwa na Paris Saint-Germain kwenye Klabu Bingwa Ulaya kwa jumla ya mabao 3-1 katika nusu-fainali na kuacha mashabiki wakiwa na huzuni kwa kumaliza msimu mwingine bila taji.

Wanabunduki wa Arsenal sasa hawana taji tangu wabebe Kombe la FA mwaka 2020.

Iliaminika kuwa Arsenal itakuwa imeshinda taji kubwa kufikia msimu unaotamatika wa 2024-2025, lakini duru nchini Uingereza zinasema kuwa hazina tashwishi kuwa timu hiyo inakaribia kabisa kushinda kombe na kuwa bado bodi inaunga mkono kocha huyo mwenye umri wa miaka 43.

Duru zinasema kuwa bodi ya Arsenal inahisi kuwa ni muda tu kabla ya Arteta kutwaa taji na kuwa atapokea uungwaji mkono unaofaa kuleta taji Kaskazini mwa London.

Kufuatia hayo, Arteta anatarajiwa kuendelea kuwa usukani ugani Emirates na pia kupata usaidizi anaohitaji. Uamuzi wa bodi kuendelea kuunga Arteta mkono kunazima uvumi unaosambaa kuwa kazi yake imo hatarini.

Bodi hiyo tayari inasemekana inashirikiana na Arteta kuhusu wachezaji wanaoweza kununuliwa mara tu soko litafunguka mwezi ujao, ikiamini kuwa hayuko mbali kuibuka bingwa wa Ligi Kuu ama Klabu Bingwa Ulaya.

Duru zinasema kuwa mchango wa Arteta unaonekana ndani na pia nje ya uwanja tangu atwikwe majukumu ya kocha mkuu mwaka 2019.