Msuya alitaka chuo kikuu cha IT Mwanga

Habari Leo
Published: May 14, 2025 07:45:25 EAT   |  Educational

MTOTO wa hayati Cleopa Msuya, Job Msuya amesema Januari 4, mwaka huu katika siku ya kuzaliwa, baba yake alieleza nia yake ya kujengewa Chuo Kikuu Mwanga kinachohusu mambo ya Bioteknolojia au Teknolojia ya Habari (IT). Job alisema hayo alipozungumza kwa niaba ya familia wakati wa ibada ya maziko ya baba yao Usangi wilayani Mwanga mkoani …

MTOTO wa hayati Cleopa Msuya, Job Msuya amesema Januari 4, mwaka huu katika siku ya kuzaliwa, baba yake alieleza nia yake ya kujengewa Chuo Kikuu Mwanga kinachohusu mambo ya Bioteknolojia au Teknolojia ya Habari (IT).

Job alisema hayo alipozungumza kwa niaba ya familia wakati wa ibada ya maziko ya baba yao Usangi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro jana.

Alisema baba yake hakupenda kufanyika sherehe ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwake lakini mwaka huu aliagiza ifanyike.

“Baada ya sherehe kuisha nikamfuata… nikamuuliza, akasema nia yake ni kujengewa chuo kikuu Mwanga ambacho sio kitakachotumia vitabu vingi, lakini kitakachotumia nguvu ya akili ambacho alisema ni bioteknolojia au IT,” alisema Job.

“Pia, alisisitiza Benki ya Mwanga, hakika benki ambayo alikuwa moja ya waasisi wake kuwa tuitunze kuwa sawa kama benki zinginze za CRDB na NMB,” aliongeza.

Alisema baba yao alitanguliza masilahi ya jamii kuliko ya familia yake kwani bila kujali hali yake alikuwa akijikita katika mambo ya kumwezesha kutimiza ndoto yake vile anavyotaka bila kusubiri.

Job alisema anashukuru kwa baba yake kuishi katika umri mrefu kufikia miaka 94 na katika miaka 54 ambayo aliishi na baba yake, alijifunza jinsi ya kupambana ili kusimama na kujisaidia katika mambo binafsi.

Aliishukuru serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia matibabu ya Mzee Msuya alipokuwa akiugua hadi pale alipofikwa na umauti wake na wote waliohusika kwa namna mbalimbali.