Msikiti Mkuu, Kasri la Usuni vyanogesha utalii Kilwa Kisiwani

Habari Leo
Published: Apr 29, 2025 11:51:11 EAT   |  Travel

LINDI; WIKI iliyopita katika mfululilizo wa makala za utalii mkoani Lindi, tulizungumzia vivutio vya utalii vilivyoko katika Wilaya…

The post Msikiti Mkuu, Kasri la Usuni vyanogesha utalii Kilwa Kisiwani appeared first on HabariLeo.

LINDI; WIKI iliyopita katika mfululilizo wa makala za utalii mkoani Lindi, tulizungumzia vivutio vya utalii vilivyoko katika Wilaya ya Kilwa.

Tulianza na historia na hadithi za magofu ya kale katika Kisiwa cha Kilwa kisha, tukagusia historia ya kisiwa hicho na hadithi za Kasri la Makutani na Kisima cha Mahandaki. Leo tutajikita katika hadithi ya Msikiti Mkuu, makaburi ya masultani na Ngome ya Mreno.

   Msikiti Mkuu na Jumba Kuu
Hayo ni magofu ya majengo mawili yaliyojengwa kwa kukaribiana katika Karne ya 13 eneo la Makutani Kilwa Kisiwani.
Magofu hayo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii vilivyopo Kilwa.

Jumba Kuu linaelezwa kutumika kama makazi ya wageni waliokuwa wakiingia katika mji wa Kilwa Kisiwani wakati wa utawala wa Sultani Sayyid Said wa Zanzibar ambaye pia alimiliki Kasri la Makutani Kilwa Kisiwani.

Aidha, viongozi wa Msikiti Mkuu kama mashehe, maimamu na masharifu waliishi katika jumba hilo.

 

Jumba hilo na msikiti vyote vinaelezwa kuwa vilihudumia wanafamilia na wageni wa Sultani Sayyid Said katika kasri hilo.
Mwongoza Watalii, Daudi Gidion anasema jumba hilo lilikuwa na vyumba 100 likiwa na uwezo wa kupokea mamia ya wageni walioingia kisiwani humo.

Kuhusu Msikiti Mkuu, Gidion anasema msikiti huo umeunganisha misikiti miwili iliyojengwa kwa nyakati tofauti.

Msikiti wa kwanza ni ule uliojengwa katika Karne ya 11 na baadaye ukaonekana hautoshi kuchukua watu wote wa eneo hilo na hivyo, ukaongezwa ukubwa na kujengwa jengo la pili katika Karne ya 13.

“Msikiti huu ni misikiti miwili kwa pamoja, kuna wa kwanza wa Karne ya 11, uliotumika kwa siku za Ijumaa na siku za sikukuu lakini ulionekana hautoshi ukaongezwa, ukaingia kwenye rekodi ya msikiti mkubwa kuliko yote chini ya Jangwa la Sahara,” anasema Gidion.
“Ulijengwa kwa nakshi na kuufanya uwe wa kipekee, una kibla mbili kwa sababu unajumuisha misikiti miwili, hiyo ilifanya upewe jina la Masjid Kibla Tain Niara Hain, inamaanisha msikiti mmoja wenye kibla mbili,” anasema.

Kwa mujibu wa Gidion, historia inaeleza kuwa msikiti huo ulikuwa umefukiwa kabisa na mchanga na haukuweza kuingilika mpaka pale mwanaakiolojia, Nevile Chittick alipoingia visiwani humo mwaka 1958 na kuufukua hadi kuwa ulivyo sasa.

Aidha, anasema msikiti huo ni moja ya misikiti 90 iliyowahi kujengwa katika kisiwa hicho na kwamba ulikuwa na nguzo 90 zilizousimamisha.

Watalii wanaokwenda kutembelea msikiti huo wanapata nafasi pia fursa ya kuona kiberenge kilichotumiwa na Chittick kuzoa mchanga kutoka kwenye kifusi kilichofunika msikiti huo.

Mbali na Msikiti Mkuu, pia upo msikiti mdogo uliotumiwa na Sultani na familia yake (Wanaume) katika siku nyingine za wiki isipokuwa Ijumaa na siku za sikukuu.

Watalii wanapofika katika eneo la Makutani wanapata nafasi ya kutembelea makaburi ya Masultani yanayoelezwa kuwa yalitumika kuzika wanafamilia ya Sultani Sayyid Said katika Kasri la Makutani .

“Wakati masultani wakiishi hapa Kilwa Kisiwani, walianzisha familia. Walipokufa walizikwa kwenye eneo hili la makaburi lililopewa jina la makaburi ya masultani, kwa hapa kaburi kongwe kabisa lilijengwa katika Karne ya 16,” anasema.

Ngome ya Mreno
Hii inatambulika pia kama Gereza la Mreno. Historia ya ngome hii ilianza katika Karne ya 9 baada ya uvamizi wa Wareno kuwafukuza Washirazi.

Ngome hii ilijengwa ili kutumika kufundishia dini ya Kikristo.

“Walilijenga na kuliita ‘Igreja’ neno la Kireno linalomaanisha kanisa. Lilitumika kwa mafundisho ya dini,” anasema na kuongeza kuwa, baada ya mafundisho kuisha lilibadilishwa na kuwa eneo la jeshi.

Gidion anasema, “Askari walikaa juu ya kuta za jengo wakiwa na silaha kulinda kisiwa.”

Anasema katika Karne ya 19, Wareno waliposhindwa kutawala kisiwa hicho, Waarabu waliingia na biashara ya watumwa hivyo wakalitumia kama gereza la kufungia wafungwa kabla ya kuwapeleka kwenye masoko.

Kwa sasa hilo ndilo gofu pekee ambalo limebaki likitumika kama makumbusho ya historia ya kisiwa hicho likiwa na vyumba viwili vinavyotumika kuhifadhi picha za michoro, vifaa mbalimbali vya utamaduni na mabaki ya sarafu za kilwa zilizotumika kwenye biashara wakati wa utawala wa Washirazi.

Kwa upande wa nje kwenye uwanja wa ngome hiyo kuna mizinga miwili, mmoja ukiwa ni wa Karne ya 16 uliotumika na Wareno na mwingine ni wa Karne ya 18 uliotumiwa na Waarabu.

Sambamba na hayo, kipo kiberenge kilichotumiwa na Chittick kuzoa vifusi kutoka kwenye magofu hayo kupeleka baharini.

  Msikiti na Makaburi ya Malindi
Msikiti na makaburi hayo yako meta chache kutoka Ngome ya Mreno na yalitumiwa na Waarabu wenye asili ya Malindi Kenya.

Msikiti huo ulitumika na wanaume peke yao. Hii ina maana kuwa, wanawake hawakuruhusiwa na ndani yake kulikuwa na chumba cha madrasa kwa ajili ya kujifunza Dini ya Uislamu.

Mhifadhi wa Malikale Kilwa Kisiwani na Songomnara, Zamoyo Mfikilwa anasema tofauti na makaburi ya masultani ambayo yalitumika kuzika familia ya masultani pekee, makaburi ya malindi yalitumika kuzika mashehe, masharifu na wenyeji wa Kilwa Kisiwani (Waswahili) na yalitofautiana muundo kuzingatia hadhi ya mtu.

“Makaburi haya yalitofautiana; yenye minara yalikuwa ni ya mashehe na masharifu, yasiyo na minara yalikuwa ya wanawake Malindi. Makaburi ya Waswahili yaliwekewa mawe…” anasema.

    Kasri la Usuni
Hili ni Kasri la Sultani Hassan bin Suleiman lililojengwa na Washirazi katika Karne ya 14 nalo pia lilikuwa na vyumba 100.
Ndani ya Kasri hilo kulikuwa na vyumba vya kulala, ukumbi wa wageni, bwawa la kuogelea na ukumbi wa mahakama ambao, Gidion anasema ulitumika kusikiliza kesi mbalimbali za watu waliofanya makosa kwenye kasri hilo na kutolewa hukumu.

“Hukumu zilikuwa na aina mbili yaani kubwa na ndogo. Watu waliopewa hukumu kubwa walitoswa kwenye kisima maalumu kilichowekwa kwa kazi hiyo,” anasema Gidion.

“Pia, kulikuwa na ukumbi wa maonesho mbalimbali, uwanja wa kufanyia biashara na ofisi za wafanyabiashara,” anaongeza.

Kimantiki, Kilwa ni wilaya yenye vivutio vingi vya utalii, tena utajiri utalii unaovutia na kuibua mambo mapya.
Ndiyo maana, kwa anayetembelea wilaya hii, hutoka bila majuto kwa kuwa hutoka akiwa na maarifa na taarifa za kutosha; za kusimuliwa na za kuona.

Ndiyo maana ninasema, Msikiti Mkuu na Kasri la Usuni ni mambo makuu ya kitalii yanayonogesha utalii Kilwa Kisiwani.

The post Msikiti Mkuu, Kasri la Usuni vyanogesha utalii Kilwa Kisiwani appeared first on HabariLeo.